Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama Kuu Dodoma
Watumishi wanawake wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jana tarehe 07 Machi, 2025 wametoa msaada wa bidhaa mbalimbali kwa wafungwa Gereza la Isanga lililopo jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kilele chake ni tarehe 08 Machi, 2025.
Akizungumzua wakati wa makabidhiano hayo Afisa Utumishi Mkuu Kitengo cha Rasilimali Watu, Bi. Sharifa Ahmad alisema Mahakama inatambua umuhimu wa kuwatia moyo wanawake walioko gerezani hivyo, wameona umuhimu huo na kuamua kufika kuwaona na kujumuika nao.
“Tumekuja kuwaona na kuzungumza na wanafunzi hawa walioko kwenye mafunzo ya marekebisho hapa gerezani, tumefanya maombi kwa pamoja na tumewapatia bidhaa mbalimbali ikiwa ni ishara ya upendo, kuwajali lakini pia na kuwaunga mkono,” alisema Bi. Sharifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la Isanga, Kamishna Msaidizi wa Magereza Zephania Neligwa aliwashukuru Mahakama kwa msaada huo akisisitiza kuwa unawapa wafungwa na mahabusu faraja kubwa na kuwafanya wajione kuwa na wao bado ni sehemu ya jamii.
“Nawashukuru sana kwa msaada huu hakika mnatupa faraja sana tukiona mnakuja kutuona lakini pia tunafurahi sana kuona mnatukumbuka, ni matumaini yangu kuwa taasisi nyingine zitaiga mfano huu wa kutembelea wafungwa na mahabusu wetu,” alisema SCP Neligwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Gereza wa upande wa wafungwa wanawake Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza Sifa Aminyike aliwashukuru watumishi hao kwa kuja kuwaona na kuwapa faraja.
Watumishi wanawake walioshiriki katika zoezi hilo walikuwa watumishi wa kada tofauti tofauti kutoka Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Kilele cha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani kitaifa kitafanyika jijini Arusha ambapo Mgeni Rasmi wa shughuli hiyo anatarajiwa kuwa ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)