tz_coa
The United Republic Of Tanzania
The Judiciary Of Tanzania
Timely And Accessible Justice To All
Post Details
USIKILIZWAJI MASHAURI NA VIFAA VYA TEHAMA VYATAJWA KUWA VIPAUMBELE VYA BAJETI MAHAKAMA KIGOMA
Post Media
post-media

Mahakama ya Wilaya Kakonko yaibuka kidedea kwa usimamizi bora wa fedha na uzingatiaji wa vipaumbele hivyo

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Mwenendo wa matumizi ya fedha za kuendeshea shughuli za Mahakama imeelezwa kuwa zinatumika vema katika shughuli za Mahakama Kanda ya Kigoma kupitia vipaumbele muhimu vilivyowekwa katika Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania (2020/2021-2024/2025) kwenye nguzo ya pili ya Mpango huo isemayo Upatikanaji na Utoaji Haki kwa wakati.

Hayo yamebainishwa wakati wa Kikao cha Bajeti ya Kanda ya Kigoma kilichofanyika tarehe 28 Februari, 2025 kilichoongozwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Bw. Filbert Matotay katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu mkoani Kigoma. 

Akitoa neno la ufunguzi wa kikao hicho, Bw. Matotay alisema kuwa, Maafisa bajeti wa Mahakama za Wilaya zote wahakikishe usikilizwaji wa mashauri na vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vinapewa kipaumbele zaidi katika bajeti zao ili kuendana na Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2020/2021-2024/2025 ambao unataka kutotumia kabisa karatasi katika shughuli za utoaji wa huduma za kimahakama katika Mahakama zote.

“Wajumbe wa Kamati ya bajeti nawasisitiza kuwa wabunifu katika kutekeleza bajeti zetu zinazopatikana katika Mahakama zetu bila kutoka nje ya utaratibu sahihi uliowekwa katika matumizi ya fedha za Serikali ili kuhakikisha kazi za Mahakama yeyote hazikwami kwa namna yeyote ile,” alisema Mtendaji huyo.

Aidha, alisisitiza kuwa, matumizi ya TEHAMA yaendelee kushika kasi maana ndio mwelekeo wa Mahakama ya Tanzania, hivyo watumishi wote Kanda ya Kigoma wawe na bidii katika matumizi ya vifaa vya TEHAMA kwakuwa mwajiri anajitahidi kuhakikisha kila mtumishi anakuwa na kifaa chake cha kutumia katika majukumu yake ya kila siku.

Katika kikao hicho, Kamati ya Bajeti iliazimia kuhakikisha fedha za mirathi zilizopo katika akaunti ya Mahakama zinalipwa kwa wadaawa na jumla ya mirathi ya 39 zimetambuliwa na kulipa fedha hizo kwa wahusika wa mirathi hizo, na kwamba imebainishwa kuwa zoezi la utambuzi wa fedha za mirathi unaendelea ili kumaliza kabisa wingi wa fedha za mirathi zilizopo katika akaunti ya Mahakama Kanda ya Kigoma.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa manunuzi ya vifaa vya TEHAMA, Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Kibondo, Bi. Naomi Chawe alisema kwamba jumla ya kompyuta mpakato (laptops) sita zimenunuliwa na kugawiwa kwa watumishi wa kada zote ili kupunguza upungufu uliopo wa vifaa hivyo.

Kwa upande wake Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa amewapongeza Maafisa Bajeti wa Mahakama za Wilaya kwa taarifa nzuri za utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025, kwani imegusa vipaumbele vya Mahakama imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa kwa usikilizwaji wa mashauri na utatuzi wa changamoto kutumia rasilimali fedha ndogo inayopatikana.

Mhe. Mbelwa alitumia fursa hiyo kuwasisitiza Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Wilaya zote ndani ya Mkoa huo kuendelea kusimamia vema bajeti zao ili zifanye shughuli muhimu za Mahakama kama Mpango Mkakati wa Mhimili huo unavyoelekeza.

Msajili huyo aliwasisitiza kuwa, wajipange kufanya kazi kwa weledi na kujituma kwa kila shughuli walizoaminiwa kufanya kwa kuongeza ufanisi.

“Hivyo niwaalike kwa mwaka huu kuchapa kazi ili kuondoa kabisa baadhi ya changamoto ndogondogo za kiutendaji ili kuwa bora zaidi ya mwaka uliopita, hii ni kwa sababu Kanda ya Kigoma hatuna historia ya kuwa na mashauri ya mlundikano na shughuli zetu zinakwenda vizuri sana,” alisisitiza Mhe. Mbelwa.

Hata hivyo, alitoa pongezi kwa Mahakama ya Wilaya Kakonko kuibuka kidedea kwa usimamizi bora ya fedha zinazopatikana za kuendeshea shughuli za Mahakama yao kwa kujali vipaumbele na muda wa matumizi sahihi ya fedha hizo.

Wajumbe wa kikao hicho ni walikuwa Mahakimu Wafawidhi wa Wilaya, Wakuu wa Idara za Mahakama Kuu Kigoma na Maafisa Tawala kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mahakama za Wilaya Kigoma, Kibondo,  Uvinza, Kasulu, Buhigwe na  Kakonko.