tz_coa
The United Republic Of Tanzania
The Judiciary Of Tanzania
Timely And Accessible Justice To All
Post Details
MAJAJI KANDA YA DAR ES SALAAM WAKUTANA KUTATHMINI UTENDAJI KAZI
Post Media
post-media

Viongozi wa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam tarehe 22 Februari, 2025 walikutana kufanya tathmini ya malengo na mipango ya utendaji kazi waliyojiwekea kwa mwaka 2024 na kuweka malengo mapya ya mwaka 2025.

Kikao hicho ambacho ni cha tatu kutoka kuanzishwa utaratibu huo, kilifanyika katika ukumbi wa White Sand Hotel Jijini Dar-es-salaam kikihudhuriwa na Majaji nane, Naibu Wasajili wanne, Mtendaji wa Mahakama  na Maofisa wa kada za utumishi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka Kanda hiyo.

Akizungumza wakati anafungua kikao hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar-es-Salaam, Mhe. Salma Mussa Maghimbi aliwashukuru wajumbe kwa kuhudhuria na kuwasihi kushiriki kikamilifu kufanya tathmini katika mipango waliyojiwekea na kujiuliza nini cha kufanya kwa yale ambayo hawakufanikiwa.

“Sote tulikuwepo mwaka jana 2024 na bahati nzuri sote tupo kwenye kikao hiki, tumekuja kujitathimini katika mipango tuliyojiwekea na kupanga jinsi gani tunatoka hapa kwenda mbele zaidi…

“…Tufanye tathmini katika yale ambayo hayakufanyika vizuri na lazima tujiulize kwa nini. Tumefanyaje kazi na kama malengo yetu tumeyafikia, na kama yamefikiwa ni kwa kiasi gani, na kama hayakufikiwa ni kwa kiasi gani,” alisema.

Jaji Mfawidhi aliwapongeza wajumbe wa kikao hicho kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kwani wameweza kuvuka malengo waliyokuwa wamejiwekea kwa mwaka 2024. Alitaja mafanikio hayo kubwa ikiwa ni kuvuka mwaka 2024 na mashauri tisa tu ya mlundikano, sawa na asilimia 0.7, ikilinganishwa na mwaka 2023 ambapo mashauri 48 ya mlundikano, sawa na asilimia 3 ndio yaliyovuka mwaka.

Alieleza kuwa mwelekeo uliopo kwa sasa katika Kanda hiyo ni sawa na kushuka mlima, akitolea mfano upande wa mlundikano wa mashauri ambao umeendelea kuporomoka.

Ingawa alitahadharisha kwamba kama hakutakuwepo na usimamizi bora wa mashauri, upo uwezekano wa kurudi nyuma jambo ambalo hatapenda kuona hali hiyo ikitokea.

“Changamoto yetu ilikuwa kwenye mashauri ya mlundikano, lakini kwa kazi mliyoifanya,  mwaka 2025 hautakuwa na mashauri kama hayo. Tunachotaka kwa sasa mashauri yanayoamuliwa yawe mengi zaidi kuliko yanayosajiliwa, na kwamba tuzuie uwezekano wa mashauri kufikia hatua ya mlundikano” alisema.

Viongozi hao wa Kanda walijadiliana kuhusu usimamizi bora wa mashauri  ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Waraka Na.1 /2025 wa Jaji Mkuu wa Tanzania kuhusu matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa mashauri, mpango wa vikao vya mashauri ya jinai na mashauri ya madai kwa mwaka 2025.

Kadhalika, walijadiliana kuhusu mpango wa Ukaguzi wa Mahakama na Magereza na pia tathmini ya utekelezaji wa  bajeti ya mwaka 2024/2025 pamoja na maoteo ya mwaka 2025/2026.

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilitoka na maazimio yakiwemo kuongeza kasi ya matumizi ya mifumo mbalimbali ya TEHAMA ili kuboresha utendaji kazi na kuzuia uzalishaji wa mashauri mlundikano.