tz_coa
The United Republic Of Tanzania
The Judiciary Of Tanzania
Timely And Accessible Justice To All
Post Details
JAJI MKUU ASHIRIKI DUA KUMWOMBEA MAREHEMU MWANAISHA ATHUMAN KWARIKO
Post Media
post-media

  • Mamia wajitokeza kuomboleza kifo chake
  • Yumo Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 29 Desemba, 2024 amewaongoza Viongozi mbalimbali kushiriki katika dua maalum ya kumuombea na kumuaga Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Mwanaisha Athuman Kwariko aliyefariki Dunia tarehe 27 Desemba, 2024 nchini India alipokuwa anapatiwa matibabu.

Dua hiyo iliyohudhuriwa na Watumishi wa Mahakama na Viongozi mbalimbali wa Serikali imefanyika nyumbani kwa Marehemu maeneo ya Masaki Mwisho, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar-es-salaam.

Jaji Mkuu alipata wasaa wa kutoa salamu za pole kwa familia, huku akionesha hisia zake baada ya kuguswa na msiba huo ambao umeacha pengo kubwa kwa Mahakama ya Tanzania.

Mhe. Prof. Juma amemwelezea Marehemu Kwariko kuwa mtumishi aliyekuwa anatekeleza majukumu yake kuwa kuzingatia maadili na mchapakazi ambaye alitumia muda wake kuwasaidia wenzake kuliko kujiangalia yeye.

“Jana nilipofika hapa nilisaini kitabu cha maombolezo. Nilipata shida sana kumuelezea mtu ninayemfahamu kuanzia kusoma kwake kwa sababu ni Mwanafunzi wangu na pia Jaji tuliyefanya kazi kwa karibu, siyo rahisi kumuelezea mtu huyo kwa kuandika mistari miwili,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Prof. Juma amenukuu maneno katika kitabu yaliyoandikwa na Mwandishi wa Vitabu Danai Lama yanayosema, “Kama hatuwezi kuwasaidia wengine katika maisha yetu, tuhakikishe kwamba hatuwakwazi na hatuwaharibii maisha watu wegine.”

Viongozi wa Mahakama waliohudhuria dua hiyo ni Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wastaafu wa Mahakama ya Rufani, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wastaafu wa Mahakama Kuu, Viongozi Waandamizi wa Mahakama na watumishi wengine wengi.

Alikuwepo pia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Viongozi wengine wa kiserikali katika Mkoa na Wilaya.

Mwili wa Marehemu Kwariko utaswaliwa kesho tarehe 30 Desemba, 2024 baada Swalat Fajr katika Msikiti wa Maamour Upanga Jijini Dar-es-salaam, kisha utasafirishwa kupelekwa Wilaya ya Kondoa Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya mazishi.