Msajili Mkuu apongeza juhudi za Majaji katika kuandika na kushirikisha maarifa
Na HALIMA MNETE, MAHAKAMA- DODOMA
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya amesema kuwa uandishi wa vitabu vya kisheria ni nyenzo muhimu katika kukuza taaluma ya sheria na kuimarisha utoaji wa haki nchini.
Mhe. Nkya aliyasema hayo jana tarehe 27 Machi 2026, jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kitabu kiitwacho “Hatia na Adhabu katika Makosa ya Jinai: Kwa Kadri ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana” kilichoandikwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Paul Joel Ngwembe.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Nkya alisema kuwa, kitabu hicho kinagusa moja kwa moja maisha ya jamii na kina mchango mkubwa katika kujenga uelewa wa masuala ya haki ya jinai, hususani katika makosa ya kujamiiana.
Alieleza kwamba, makosa ya kujamiiana yanahusiana moja kwa moja na utu na hadhi ya binadamu, hivyo kuwepo kwa maandiko ya kitaaluma kunasaidia kutoa mwanga kuhusu dhana muhimu za hatia na adhabu ambazo ni msingi wa sheria ya jinai duniani kote.
“Kitabu hiki kinakuja kutoa mchango wa kitaaluma katika eneo ambalo limekuwa na mashauri mengi mahakamani, pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wafungwa magerezani,” ameeleza Msajili Mkuu.
Aidha, amempongeza Jaji Ngwembe Mwandishi wa kitabu hicho kwa kuchangia maarifa yake kupitia maandishi, akibainisha kuwa uandishi unasaidia kuhifadhi maarifa na kuyaacha kama kumbukumbu ya kudumu kwa vizazi vijavyo.
“Sisi kama Mahakama tunajivunia juhudi hizi za Majaji na Mahakimu wanaoandika vitabu, kwani vinachangia kuendeleza taaluma ya Sheria na kuzalisha vyanzo vya maarifa,” ameongeza.
Mhe. Nkya pia alisema kitabu hicho kinatarajiwa kuwa rejea muhimu kwa wadau mbalimbali wa sheria wakiwemo Majaji, Mahakimu, Mawakili wa Serikali, Mawakili binafsi pamoja na Wanataaluma wa Sheria.
Vilevile alitoa shukrani kwa Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha dhamira ya Mahakama katika kukuza taaluma na utafiti wa sheria nchini.
Uzinduzi huo ni sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania kuhamasisha uandishi wa kitaaluma miongoni mwa watumishi wake na wadau wa sekta ya sheria kwa lengo la kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.

