· Asisitiza Utawala wa Sheria ni moja ya misingi ya mafanikio
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita itashirikiana kwa dhati na Mahakama ya Tanzania katika uboreshaji wa miundombinu ya majengo, vitendea kazi, watumishi na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuuwezesha Mhimili huo kutoa haki kwa wananchi mapema ipasavyo.
Rais Samia ameeleza hayo leo tarehe 14 Novemba, 2025 jijini Dodoma wakati akitoa hotuba ya Ufunguzi rasmi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Msingi mwingine wa mafanikio yote haya ni utawala wa sheria, ahadi yetu ni kuwa Serikali itashirikiana kwa dhati na Mahakama ya Tanzania kuhakikisha haki inapatikana kwa watu wote na kwa wakati,” amesema Mhe. Dkt. Samia.
Ameongeza kwamba, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili Mahakama iweze kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi.
Aidha, Rais Samia amesema, “tutasimamia utekelezaji kamili wa mapendekezo ya Tume ya Rais ya kuangalia namna ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai. Tutaendelea kufanya mageuzi na maboresho katika taasisi zote zinazoshughulikia masuala ya Haki Jinai ili ziweze kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu.”
Mhe. Dkt. Samia ameahidi pia, Serikali itakamilisha tafsiri ya sheria zetu zote kwa lugha ya Kiswahili, ikiwa ni hatua muhimu ya kuhakikisha kuwa wananchi wanaelewa kwa urahisi sheria za nchi.
Kadhalika, Mhe. Dkt. Samia ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika Sekta ya Sheria, ikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) pamoja na asasi zingine ili kuwezesha upatikanaji wa huduma na msaada wa kisheria kwa wananchi, na kusema kwamba manufaa ya huduma hiyo yameonekana bayana katika kipindi kilichopita katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Sekta nyingine ambazo Rais Samia amegusia katika hotuba yake na kuahidi kuboresha zaidi ni pamoja na Afya, Elimu, Madini, Kilimo, Uvuvi na nyingine.
Viongozi mbalimbali wa Serikali, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wabunge na wengine akiwemo Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju na Jaji Mkuu wa Mahkama Kuu ya Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdallah wameshiriki katika ufunguzi wa Bunge la 13.

