tz_coa
The United Republic Of Tanzania
The Judiciary Of Tanzania
Timely And Accessible Justice To All
Post Details
JAJI MKUU AHIMIZA USHIRIKIANO KWA WADAU WA MAHAKAMA KUWEZESHA UTOAJI HAKI MAPEMA IPASAVYO
Post Media
post-media

 

·       Ni katika Mkutano wa Wadau kuhusu ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani

·       Asisitiza pia uwajibikaji wa wadau wa mnyororo wa haki

·       Ashauri mikutano hiyo kufanyika angalau mara nne kwa mwaka 

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju amewahimiza Wadau wa Mahakama nchini juu ya umuhimu wa kuendeleza na kuimarisha ushirikiano na mahusiano ili kutekeleza jukumu la utoaji haki mapema ipasavyo na kwa ustawi wa wananchi.

Akizungumza leo tarehe 24 Septemba, 2025 wakati akifungua Mkutano wenye ajenda kuu ya Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ya Jaji Mkuu- Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Masaju amesema ushirikiano na mshikamano ni wa lazima na ni takwa la kikatiba, kisheria na hata Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.

“Nawashukuru Viongozi kwa kutenga muda wenu kuja kushiriki katika mkutano huu muhimu, niseme tu kwamba ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu yetu Mahakamani umejengwa kwenye Katiba na kwenye sheria mbalimbali zinazoanzisha Taasisi zetu hizi, kwa hiyo ni ushirikiano wa kulazimika na wala sio wa hiari, na wote sisi nia yetu ni ustawi wa wananchi,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amesema kuwa, kila mdau wa mnyonyoro wa haki ni muhimu, kunapokuwa na ushirikiano na uhusiano wa namna hiyo kwa wadau, kuna umuhimu mkubwa ambao ni pamoja na kuyaimarisha, kutambua mafanikio yaliyofikiwa, changamoto zinazokabili ushirikiano na mahusiano hayo na kuziwekea mikakati ya kuzitatua.

“Kwahiyo mambo haya yanatuhusu sisi wote, sisi wote tumewekwa na wananchi kwa ajili ya kuwatumikia ili kufikia ustawi wao, tumepewa majukumu ya uwajibikaji, tunapotekeleza majukumu yetu na sisi sasa tunazungumza kwenye huu mnyororo wa haki ambao unaishia Mahakamani, Ibara ya 25 ibara ndogo ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema wajibu wa kushiriki kazini,” ‘Kazi pekee ndio huzaa utajiri wa mali katika jamii, ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na kipimo cha utu na kila mtu anao wajibu (a) kushiriki kwa kujituma na kwa uaminifu katika kazi halali na ya uzalishaji mali na (b) kutimiza nidhamu ya kazi na kujitahidi kufikia malengo ya uzalishaji mali ya binafsi na yale malengo ya pamoja na yanayotakiwa au yaliyowekwa na sheria,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju ameeleza kwamba, Taasisi zote ikiwemo Mahakama zimeanzishwa kwa mujibu wa sheria, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki kikamilifu kuimarisha ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki Mahakamani.

Aidha, Jaji Mkuu ameongeza kwa kushauri kuwa, vikao hivyo viwe endelevu na vifanyike angalau mara nne kwa mwaka (kila robo mwaka) ili kupata fursa ya kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu Mahakama na wadau wake na hatimaye kupata suluhisho ya changamoto mbalimbali kwa kuweka mikakati mbalimbali ya kuzitatua ili kusonga mbele.

Kadhalika, Mhe. Masaju amesema kwamba mkutano huo umekuja wakati muafaka, ambapo kuna Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ambapo msingi mkuu wa Dira hiyo ni Utawala, Amani, Usalama na Utulivu na moja ya kipaumbele cha kwanza ni Utawala Bora na Haki, kipaumbele cha pili ni Serikali za Mitaa Imara na zenye ufanisi na cha tatu ni Utumishi wa Umma unaowajibika na kipaumbele cha nne ni Amani, Usalama na Utulivu. Amesema wadau wote ni wahusika katika kusimamia na kutekeleza masuala hayo.

Aidha, Jaji Mkuu amesisitiza juu ya kipengele cha tatu cha Dira hiyo kinachohusu 'utumishi wa umma unaowajibika' kwa kutoa rai kwa wadau hao kuwa, kila mmoja anawajibika kutekeleza malengo ya kudumisha utawala bora kwenye utekelezaji wa upatikanaji wa haki Mahakamani na amani, usalama na utulivu.

"Ikiwa Serikali inapata mamlaka yake kutoka kwa wananchi na lengo lake kuu ni ustawi wa wananchi na inawajibika kwa wananchi, sisi ambao ni watumishi wa umma tuna wajibu mkubwa sana kuwajibika katika kutekeleza majukumu yetu," ameeleza Mhe. Masaju.

Aidha Mhe. Masaju amerejea ukurasa wa 63 wa Dira hiyo ambao unahimiza ushirikiano katika sekta mbalimbali, inasema ‘ili kuhakikisha Dira 2050 inatekelezwa kwa ufanisi, Serikali imeweka mfumo imara wa usimamizi unaozingatia malengo yake mahsusi, mfumo huu umekusudia kuhimiza uwajibikaji, ukihitaji uongozi mahiri na ulio makini katika ufuatiliaji, aidha mfumo unahimiza matumizi ya mbinu zinazotoa matokeo yanayopimika......’

‘.....msingi wa mkakati huu ni mabadiliko makubwa ya kifikra yakilenga vitendo badala ya maneno na matokeo badala ya ahadi, uongozi, taasisi pamoja na watendaji na wadau wote wanapaswa kuwajibika ili kutimiza malengo ya Dira kwa ufanisi, Taasisi imara na mifumo Madhubuti inayolenga kuondoa uzembe, inayohimiza uwajibikaji na kuchochea ufanisi itakuwa nguzo kuu ya utekelezaji wa Dira 2050...Dira imeweka mfumo madhubuti wa utawala unaohakikisha utekelezaji unafanyika kwa nidhamu, sera zinasomana, taasisi zinakuwa imara na sekta na wadau wote wanashirikiana.’

Amesema kwamba, mkutano huo utakuwa pia kichocheo kwa taasisi nyingine kuandaa mikutano kama huo na kuwashirikisha wadau muhimu kwenye Sekta ya Sheria inayohusu utoaji haki. 

Aidha, Jaji Mkuu amesisitiza juu ya umuhimu wa ushirikiano ili mashauri yaweze kukamilika mapema ipasavyo huku akigusia mashauri ya jinai, mashauri ya kodi, mashauri ya biashara, mashauri ya migogoro ya kibenki na mengine.

Kadhalika, Mhe. Masaju amewaomba Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kufuatilia utekelezaji na kutoa mrejesho kuhusu utekelezaji wa Kifungu cha 134 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai ambacho kinasema kwamba mashauri hayatafunguliwa Mahakamani isipokuwa kama upelelezi umekamilika isipokuwa kwa mashauri yanayosikilizwa na Mahakama Kuu na yaliyotajwa na kifungu hicho yanayoitwa 'Serious Offences' (Makosa Makubwa ya Jinai) ambayo yametajwa  kwa mujibu wa 'Criminal Procedure Act' (Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai). 

"Nawaomba Jeshi la Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) mtusaidie kufuatilia utekelezaji wa kifungu cha i (34) je inatekelezwa? tuleteeni taarifa hili ni kosa ambalo mtu anapaswa akamatwe wakati upelelezi umekamilika na kupelekwa Mahakamani, lakini pia tusaidieni kufuatilia na kutupatia taarifa za yale mashauri ambayo yanasikilizwa na Mahakama za Mahakimu isipokuwa Mahakama za Mwanzo ambayo Mkurugenzi wa Mashtaka na sisi mahakamani tumeshajiwekea utaratibu kwamba yamalizike ndani ya miezi sita, je yapo ambayo hayajamalizika ambayo yapo kwenye hatua ya 'trial'? au yapo kwenye upelelezi, tuleteeni taarifa hizo ndio ushirikishwaji huu ambao tunazungumza sisi Wadau wa Haki Mahakamani tukifanya hivyo tutapiga hatua," amesisitiza Jaji Mkuu.

“Nilipokutana na Taasisi za utatu tarehe 19 Agosti, 2025 jijini Dodoma, nilipokuwa nashiriki kwenye ule mkutano mengine niliyowashirikisha nitarejea kidogo hapa, nilisema nakusudia kutengeza Kanuni zitakazowezesha wale watu wanaoshtakiwa kwa makosa ya jinai kwenye Mahakama za Mahakimu ispokuwa Mahakama za Mwanzo na wao hao washtakiwa na Mahakama hizo wao nao wawe na ushahidi wa upande wa kesi za mashtaka ili wajue kesi zao, tumetengeneza sisi hapa rasimu ya hizo kanuni tumeziwasilisha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, tumeziwasilisha kwa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ili wazipitie, watuletee maoni yao kabla hatujazitangaza kwenye Gazeti la Serikali, ilikuwa ifikapo tarehe 19 Septemba, 2025 lakini tumechelewa kwakuwa tunasubiri maoni ya wadau,"  alisisitiza Jaji Mkuu.

Ameongeza kuwa, msingi wa mabadiliko ya kanuni hizo umejengwa kwenye Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 'usawa mbele ya sheria'  ibara ndogo ya sita ya Ibara ya 13 (b) inasema kila anayeshitakiwa Mahakamani kwa kosa la jinai atachukuliwa kwamba hana hatia hadi itakapothibitishwa hivyo na Mahakama.

"Sasa hivi mtu anashtakiwa anaenda Mahakamani hajui kitu kitakachomtokea huko mbeleni, Mahakama inakuwa haina ushahidi, mshtakiwa naye hajui kwahiyo Mahakama inakuwa katika mazingira magumu sana ya kuweza kufanya maamuzi yanayostahili ni tofauti na ilivyo sasa Mahakama Kuu unakuta Mahakama ina ushahidi wote, mshtakiwa naye ana ushahidi wote, huu kwa ni mfumo shirikishi kwahiyo Mahakama inakuwa katika mazingira mazuri ya kufanya maamuzi sahihi," amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju ameeleza kuwa, kupatikana kwa kanuni hizo kutawezesha kuimarisha umakini katika upelelezi kwa kuwa upelelezi ukiwa mzuri na maamuzi yatafanyika vizuri, kupunguza ubambikizaji wa mashauri, itasaidia kuharakisha usikilizwaji wa kesi kwa haraka na hatimaye kutoa maamuzi mapema,  italeta pia umakini katika utoaji haki, itadhibiti vitendo vya rushwa, itaendana na Katiba ambayo inataka usawa mbele ya sheria na vilevile itasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani.

Mhe. Masaju amewaomba ushirikiano wadau hao, kuwa huru kutoa maoni yao katika mkutano huo na kuweka mikakati thabiti itakayoboresha utendaji kazi ya utoaji haki na hatimaye Mahakama ya Tanzania iwe moja kati ya mihimili yenye hadhi duniani.

Naye Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Abdi Kagomba amesema kufanyika kwa mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa Nguzo namba tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2020/2021-2024/2025 ya Kuimarisha Imani ya Wananchi na Ushirikishwaji wa Wadau.

“Kupitia nguzo ya Tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama, tumesisitizwa juu ya kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya haki kama mhimili muhimu unaoimarisha misingi ya utawala bora. Katika utekelezaji wa nguzo hii, hivi karibuni tumeshuhudia juhudi zako za dhati Mheshimiwa Jaji Mkuu juu ya kuimarisha dhana nzima ya ushirikishwaji wa wadau. Ushiriki wako katika matukio mbalimbali, ikiwemo ziara uliyofanya Gereza Kuu Isanga tarehe 10 Julai, 2025, ufunguzi wa mjadala wa kitaifa juu ya maboresho ya sheria na sera tarehe 19 Agosti, 2025, ufunguzi wa kikao kazi baina ya ofisi ya DPP, DCI, PCCB na DCEA tarehe 20 Agosti, 2025, ufunguzi wa mkutano wa tisa wa kamati ya utatu tarehe 25 Agosti, 2025, na mengineyo mengi, unathibitisha juhudi hizo,” amesema Mhe. Kagomba.

Kaimu Jaji Kiongozi huyo amesema, kupitia ushirikiano wa dhati baina ya Mahakama na wadau, ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, vyombo vya Ulinzi na Usalama, pamoja na wadau wote waliokusanyika katika mkutano huo, utajenga taswira moja ya utumishi wa haki na kuongeza imani ya wananchi kwa mfumo mzima wa utoaji wa haki. 

Mkutano huo wenye ajenda kuu ya Ushirikiano na mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki mahakamani umehudhuriwa na wadau mbalimbali ambao ni Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi Wa Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Inspekta Generali wa Polisi, Ofisi ya Kamishna wa Magereza, Ofisi ya Kamishna wa Uhamiaji, Ofisi ya Mkurugenzi wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi Ya Kamishna wa Mamlaka Kudhibiti na Kupambana na Dawa Za Kulevya, Ofisi ya Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali na Ofisi ya Rais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS).