tz_coa
The United Republic Of Tanzania
The Judiciary Of Tanzania
Timely And Accessible Justice To All
Post Details
JAJI MAMBI AWANOA WADAU WA HAKI JINAI TABORA KUHUSU MAKOSA YA MTANDAO NA AKILI-UNDE
Post Media
post-media

 
 
  • Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora apongeza ushirikiano wa Mahakama na wadau wa sekta ya haki

Na AMANI MTINANGI, Mahakama - Tabora

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imeendesha mafunzo maalum kwa wadau wa haki jinai kuhusu makosa ya kimtandao yanayolenga kuwajengea uwezo wadau hao kukabiliana na uhalifu unaohusisha teknolojia ya kisasa na namna ya kutumia teknolojia kuzia uhalifu.

Mafunzo hayo yalifanyika jana tarehe 14 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma mkoani Tabora chini ya uongozi wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi ambaye pia alikuwa Mwezeshaji mkuu wa mafunzo hayo.

Mgeni rasmi wa mafunzo hayo ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Rogath Mboya alitumia fursa hiyo kumpongeza Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Tabora kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha uelewa wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na jinsi ya kukabiliana na makosa ya mtandaoni.

“Ninampongeza sana Mhe. Dkt. Mambi ambaye ni mbobezi mkubwa katika masuala ya Teknoljia na Sheria za TEHAMA kwa juhudi zake binafsi na kwa kujitolea kutoa elimu hii muhimu kuhusu akili bandia na teknolojia za kisasa zinazosaidia ukusanyaji wa ushahidi na kuzuia uhalifu wa kimtandao,” alisema Dkt. Mboya huku akiongeza kuwa Mhe. Dkt. Mambi amekuwa akionesha ushikiano mkubwa kwa wadau wa haki jinai.

Kwa mujibu wa Mhe. Jaji Dkt. Mambi, lengo la mafunzo hayo ni kuhamasisha matumizi ya teknolojia zinazoibuka kwa kasi kama akili unde (AI) na mifumo ya kiteknolojia katika upelelezi wa makosa ya mtandao, kudhibiti ujangili katika hifadhi za taifa, ukusanyaji wa ushahidi wa kielektroniki, pamoja na kulinda taarifa binafsi na haki za binadamu katika mazingira ya kidijitali.

Kwa mujibu wa Mhe. Dkt. Mambi, lengo la mafunzo hayo ni kuhamasisha matumizi ya teknolojia zinazoibuka kwa kasi kama Akili Unde (AI) na mifumo ya kiteknolojia katika upelelezi wa makosa ya mtandao, kudhibiti ujangili katika hifadhi za taifa, ukusanyaji wa ushahidi wa kielektroniki, pamoja na kulinda taarifa binafsi na haki za binadamu katika mazingira ya kidijitali.

Washiriki wa mafunzo hayo walijifunza namna ya kutumia mbinu za teknolojia ya Akili Unde katika kusimamia uhalifu wa majangili katika hifadhi za Taifa, usimamiaji wa rushwa, makosa ya mtandao pamoja na mbinu ambazo wahalifu wanatumia teknolojia ya Akili-Unde katika kutenda uhalifu. 

Mafunzo hayo yatafanyika kwa siku ya pili ambapo wadau wa Haki Jinai  watapata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu utaratibu wa kisheria wa kukusanya ushahidi wa kielektroniki na utaratibu wa kuwasilisha ushahidi wa kilektroniki mahakamani kabla Mahakama haijatoa uamuzi.

Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ofisi ya Mashtaka Kanda ya Tabora yaliwaleta pamoja wadau kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Ushirikiano huo ni mfano wa namna Mihimili ya Dola na Taasisi nyingine za Umma zinavyoweza kushirikiana katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu vinavyokua kwa kasi.