tz_coa
The United Republic Of Tanzania
The Judiciary Of Tanzania
Timely And Accessible Justice To All
Post Details
TANZIA; HAKIMU MKAZI MKUU MAHAKAMA YA WILAYA MOROGORO AFARIKI DUNIA
Post Media
post-media

Mahakama ya Tanzania inasikitika kutangaza kifo cha Mtumishi wake Mhe. Richard Robert Kasele  aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya Morogoro.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo tarehe 12 Agosti, 2025 na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng'eni marehemu Richard alifikwa na umauti Siku ya Jumapili tarehe 10 Agosti, 2025 saa 4:00 usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Bw. Ng'eni amesema kuwa, ibada ya kumuaga marehemu kwa upande wa Dar es Salaam itafanyika Muhimbili Siku ya Jumatano tarehe 13 Agosti, 2025 saa 4:00-5:00 Asubuhi.

Mtendaji huyo amesema kuwa, safari ya kwenda Morogoro itaanzia Muhimbili mara baada ya ibada ya kumuaga marehemu. Aidha tarehe hiyohiyo 13 Agosti mwaka huu saa 10 jioni itafanyika ibada nyingine ya kumuaga katika Kanisa la KKKT Usharika wa Majengo. 

Bw. Ng'eni amesema kuwa,  mazishi yanatarajia kufanyika siku ya Alhamis tarehe 14 Agosti, 2025 mchana katika makaburi ya barabara ya Mwanza (Mwanza road) Mtaa wa Cheyo A Manispaa ya Tabora. 

Marehemu Richard alizaliwa Mpanda tarehe 16 Desemba, 1974 na aliajiriwa na Mahakama ya Tanzania mwaka 2003 kwa Cheo cha Hakimu Mkazi - Moshi ambapo alihudumu hadi mwaka 2006, kuanzia mwaka 2006 hadi 2013 marehemu Richard alihudumu Mahakama ya Wilaya Mpanda kama Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo. Mwezi Aprili 2013 hadi Aprili 2018 marehemu alifanya kama Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa akihudumu kwa nafasi ya Hakimu Mkazi.

Mahakama ya Tanzania inaungana na ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza msiba huo mzito wa kuondokewa na Mpendwa wetu Richard Robert Kasele.