· Jaji Mkuu ataja kuwa hatua hiyo ni mafanikio makubwa katika historia utawala wa sheria nchini
· TLS nayo yapongeza uboreshaji huduma za Mahakama hususani matumizi ya TEHAMA
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kuondoa Mahabusu wote wa Mahakama za Mwanzo waliokuwa katika Magereza mbalimbali nchini kufuatia kupatiwa dhamana ya makosa wanayotuhumiwa nayo.
Hayo yalibainishwa jana tarehe 11 Agosti, 2025 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju alipokuwa akifanya mazungumzo na Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) waliomtembelea ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Mnamo tarehe 10 Julai, 2025 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Masaju alifanya ziara katika Gereza la Isanga mkoani Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine alielekeza Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kutowaweka Mahabusu watuhumiwa wa Mahakama hizo na kupunguza masharti ya dhamana katika ngazi zote za Mahakama nchini.
“Hakuna sababu za msingi za kuwa na mahabusu wa Mahakama za Mwanzo, kwa sababu makosa yote ya jinai yanayosikilizwa na Mahakama za Mwanzo yanadhaminika, maana yake Bunge lilikusudia kwamba hawa watu wasiwe mahabusu, halafu sheria hiyohiyo inatoa pia fursa ya mtu kujidhamini,” alisema Jaji Mkuu wakati wa ziara yake katika Gereza la Isanga.
Mhe. Masaju alibainisha kuwa, tangu alipotoa maelekezo hayo, Mahakama imeendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha kuwa suala hilo linatekelezwa na jambo mojawapo lililofanyika ni yeye Jaji Mkuu kumuomba Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini kumpatia taarifa ya kila siku ya Magereza yote nchi nzima ili kujua takwimu za mahabusu wa Mahakama za Mwanzo.
“Ilipofika tarehe 17 Julai, 2025 taarifa ilionesha kuwa kuna jumla ya Mahabusu 1,411 wa Mahakama za Mwanzo kwenye Magereza yote nchini lakini tangu tarehe 30 mwezi wa 7 hadi kufikia jana tarehe 10 Agosti mwaka huu hakukuwa na mahabusu yoyote wa Mahakama za Mwanzo kwenye Magereza,” alieleza Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju alisema kuwa, hatua hiyo ni mafanikio makubwa kwa Mahakama ya Tanzania na utawala wa sheria kwa ujumla na kukiri kuwa, hatua hiyo ina faida kadhaa ambazo ni pamoja na kuongezeka kwa Imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama, kuharakisha utoaji wa haki, kupunguza mahabusu ambao itawezesha rasilimali zilizopo ndani ya magereza kusaidia kuboresha huduma nyingine na kusaidia kupunguavitendo vya ukiukwaji wa maadili.
Aidha, Jaji Mkuu alitoa rai kwa wananchi kutoa taarifa Mahakamani kama kuna mahabusu yoyote ambaye yupo gerezani ili taratibu stahiki za kumpatia dhamana zifanyike.
Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju alitoa rai kwa TLS kushirikiana na Mahakama ili kuendeleza jukumu la utoaji haki kwa wananchi, ambapo amesisitiza kwa kusema, “Mawakili msiwe chanzo cha baadhi ya matukio ya kichochezi badala yake tusaidie wananchi.”
Akirejea kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, Jaji Mkuu aliwaeleza Mawakili hao kuisoma Dira hiyo kuona mambo ambayo Mahakama inapaswa kufanya katika eneo la uboreshaji wa huduma za haki nchini ili wao kama Maafisa Mahakama waweze kuwasilisha mapendekezo au maoni ya namna gani Mahakama inaweza kufanya mambo yote yanayoigusa jamii kwa mustakabali wa ustawi wa haki .
Mhe. Masaju aliueleza ugeni wa TLS kuwa, Mahakama ya Tanzania itaishirikisha TLS katika maandalizi ya kuandaa Mpango Mkakati wa Mahakama wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 hususani katika eneo la haki.
Vilevile; Jaji Mkuu alitoa rai kwa Mawakili wa Kujitegemea nchini kuwa na utaratibu wa kufuatilia masuala au maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Viongozi wa Dola ikiwemo Serikali, Bunge na Mahakama kwa kupitia hotuba na vyanzo vingine kwa vile yanaweza kujibu baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju aliwakumbusha Mawakili hao kuwa, wao kama Maafisa Mahakama ambao wanachangia katika kutekeleza majukumu ya utoaji haki wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia uadilifu, ubunifu, uwajibikaji, uwezo wa kufanya kazi na kuweka mbele uzalendo na maslahi ya Taifa ambayo pia ni maslahi ya umma.
Akizungumza katika kikao hicho, naye Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi alisema, “tunatoa shukrani za pekee kwa ushirikiano wa karibu na wa tija kati ya Mahakama na TLS, hususani katika uboreshaji wa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo kwa sasa TLS na Mahakama zinafanyia kazi suala la usomaji wa mifumo baina ya pande hizo kwa lengo la kurahisisha taratibu muhimu zinazohitajika.
Aidha, Wakili Mwabukusi alitaja mapendekezo kadhaa yanayolenga kuimarisha zaidi mfumo wa utoaji haki ambayo ni pamoja na kuanzishwa kwa Mahakama ya Upeo (Supreme Court), kuanzisha utaratibu wa kuwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani Wakazi kwa kila Kanda, kuwepo kwa Jaji wa zamu katika kila Mahakama Kuu kwa ajili ya kushughulikia masuala ya dharura kila siku ili kuhakikisha kuwa, haki na nafuu zinazohusu haki za msingi za binadamu zinaamuliwa kwa haraka.
“Vilevile tunapenda kupendekeza kuwepo kwa mafunzo maalum kwa Waandishi wa Habari kwakuwa upo umuhimu mkubwa kwa Mahakama kushirikiana na TLS kuandaa mafunzo maalum kwa Waandishi wa Habari hususani wali wa “online TVs” na majukwaa ya kidijitali, ili kuwajengea uwezo wa kuripoti kwa usahihi na kwa weledi mwenendo wa mashauri na taarifa zinazohusu Mahakama,” alisema Rais huyo wa TLS.
Kadhalika, Wakili Mwabukusi alitaja changamoto zinazoikabili sekta ya sheria ambazo zimekuwa zikikwaza ufanisi wa kazi zao na kuiomba Mahakama isaidie kufanya uoanifu wa maamuzi mbalimbali yanayokinzana (conflicting decisions) ambayo yamekuwa yakitolewa na Mahakama.
“Kumekuwa na changamoto ya uwepo wa hukumu za Mahakama za juu zinazokinzana kwenye jambo moja suala linalosababisha ugumu katika utendaji wa kila siku wa kazi za Mawakili kutokana na kutokujua kwa usahihi ni maamuzi yapi yatakayokuwa sahihi kwenye jambo fulani linalobishaniwa,” alisema Mwabukusi.
Aliongeza kuwa, kuwepo na kipaumbele katika kuheshimu misingi ya haki, usawa na hadhi ya kila mtu mbele ya sheria. Wakili Mwabukusi alibainisha kuwa, kumejitokeza matendo ambayo sio ya kiungwana yanayofanywa na baadhi ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama (Jeshi la Polisi na Magereza) kwenye vyumba vya Mahakama au viunga vya Mahakama wakati wa uendeshaji wa mashauri mahakamani.
Aidha mara baada ya kupokea taarifa ya TLS, Jaji Mkuu alisema, “sisi mahakamani hadi sasa tunatambua na tunashukuru na kuthamini mchango wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Chama cha Wanasheria Tanganyika. Jaji Mkuu alieleza kuthamini mkutano huo na hoja ambazo TLS iliziwasilisha katika maandishi na kuwaomba kama yapo mambo mengine basi yajumuishwe kwenye taarifa yao na kisha yawasilishwe katika ofisi yake ili iwe rahisi kuzishughulikia zote kwa pamoja.