Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Uboreshaji wa Sera na Sheria unapaswa kutokana na wananchi wenyewe hapa nchini, kwa kuzingatia mahusiano ya kijamii, kiuchumi na kisiasa [social, economic and political relations] na siyo kwa shinikizo au ushawishi wa namna yoyote.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 10 Agosti, 2025 jijini Dodoma na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju alipokuwa anafungua Mkutano wa Mwaka wa Majadiliano baina ya asasi za kiraia na Serikali.
Mkutano huo ulibeba dhima ya “Majadiliano ya Kitaifa kuhusu Maboresho ya Sera Sheria: Kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Asasi za Kiraia” na kuwaleta pamoja Watetezi wa Haki za Binadamu kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar.
Jaji Mkuu alibainisha kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 8(1)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na lengo kuu la Serikali, kwa mujibu wa Ibara ya 8(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni ustawi wa Wananchi.
Kwa mantiki hiyo, alisema, ili kufikia kwenye maamuzi lazima Serikali ishirikishe wananchi na pale ambapo kuna mabadiliko yanahitajika kufanyika katika sera na sheria kutokana na mabadiliko katika jamii, uboreshaji unapaswa kuzingatia Katiba, Sheria pamoja na tunu za taifa.
Jaji Mkuu alifafanua kuwa ‘Mataifa yanatofautiana national values [tunu za taifa] na unaweza kukuta wengine wapo mbali zaidi na sisi hatujafika huko. Sisi twende na ya kwetu, ambayo yana akisi uhalisia wa pale tulipofikia kwa sababu lengo ni wananchi. Tukianza kuendekeza mambo ambayo yatakuja kubomoa udugu na amani, Taifa hili litakuwa na changamoto.’ Aliongeza kuwa, ‘asasi za kiraia ni zetu wananchi na sisi tunaongozwa na tunu za taifa, hivyo tuzisimamie.’
Mhe. Masaju alibainisha kuwa Sera zinazopendekezwa kufanyiwa mabadiliko au kuja na sheria mpya au sheria zilizopo kubadilishwa sharti kuzingatia tunu za taifa ‘national values’ na maslahi ya Taifa.
‘Kabla ya kuridhia uboreshaji wa Sera au Sheria sharti Serikali kujiridhisha kama maslahi ya Wananchi, Umma na Taifa yamezingatiwa na uzingatiaji wa Katiba ipasavyo, ikiwemo Ibara ya 12 hadi ya 29 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayozungumzia haki na wajibu wa kila raia,’ amesema.
Jaji Mkuu alisema kuwa uboreshaji wa Sera na Sheria sharti uzingatie umuhimu wa utawala wa Sheria kama inavyoelezwa kwenye Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, malengo muhimu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za Serikali, kama vinavyopatikana kuanzia Ibara ya 6 hadi ya 11 ya Katiba.
Mhe. Masaju ametumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa ushirikiano na majadiliano kati ya Serikali na Asasi za Kiraia katika kuboresha Sera na Sheria ili kukidhi ustawi wa wananchi kama lengo la Serikali lilivyo.
Alitoa rai kwa asasi za kiraia ili kuleta tija ni muhimu kujikita katika kuisaidia Serikali kuleta uboreshaji kwa ajili ya maendeleo ya Taifa badala ya kuangukia katika mlengo wa kiuanaharakati ambapo mara nyingi huishia kubomoa badala ya kuleta ustawi wa wananchi.
Alisisitiza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 8(1)(b) ya Katiba, malengo ya Serikali ni kwa ajili ya ustawi wa wananchi, lakini wakati huo huo asasi za kiraia nazo zina malengo fulani, hivyo pande zote mbili zikikutana na kufanya majadiliano kunapatikana mawazo yenye msingi kwa maslahi ya Taifa,’ amesema.
Amesema kuwa katika kufikia malengo fulani, masuala ya mahusiano ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ni lazima uwashirikishe wananchi kwa sababu ni mambo yanayowahusu na wao ndio msingi wa mamlaka yote.
Jaji Mkuu amesisitiza kuwa timu za majadiliano zijumuishe Viongozi na Maofisa ambao wanauelewa wa kutosha kuhusu mada [subject matter] ya mashauriano kabla ya kufikia mwafaka.
Amesema kuwa timu za majadiliano kwenye mambo kama ya mapendekezo ya mabadiliko ya Sera na Sheria lazima yajumuishe pande zote mbili na wale wanaotoka serikalini na katika Asasi za Kiraia waje wanaojua vizuri jambo husika, Katiba ikoje na masuala ya mahusiano ya kijamii, kiuchumi na kisiasa yakoje.
‘Uboreshaji wa Sera na Sheria uliofikiwa na kupatikana baada ya mashauriano unadumu na kuheshimiwa kinyume na uboreshaji unaotokana na shinikizo au ushawishi usio rasmi,’ Mhe. Masaju amesema.
Jaji Mkuu alibainisha kuwa jamii inaundwa na wananchi, lakini miongoni mwa wananchi hao ndiyo wengine wanaunda Asasi za Kiraia ambazo zinaundwa na Ibara ya 20 [1].
Akipongeza hatua ya kutaka kuundwa kwa Bench – Bar Forum ili kujadili changamoto mbalimbali na kupendekeza uboreshaji pale panapohitaji kuboreshwa. Jaji Mkuu amegusia kuwa Muhimili wa Mahakama uko tayari kutoka ushirikiano kwa asasi za kiraia kupitia forum hiyo kwa dhamira ya kukuza ustawi wa wananchi.
‘Kwa upande wa Mahakama ya Tanzania, moja ya Mihimili ya Serikali, tupo tayari na tutaendelea kushirikiana na Asasi za Kiraia katika kuboresha huduma za kimahakama kwa kupokea ushauri, lakini kwa kuzingatia maadili ya Mahakama, Katiba, Sheria na Tunu za Taifa,’ Jaji Mkuu alisema.
Akizungungumza katika mkutano huo, Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Elimo Masawe ameeleza kuwa ameshiriki kwenye kikao kazi cha Watetezi wa Haki na amepata fursa ya kuwasikia Wadau hao wa haki nchini na kuona ni maeneo gani ambayo bado wanaweza kushirikiana nao.
Mhe. Masawe, ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Masjala Kuu, amesema ameona pia maeneo ambayo wanahitaji kukaa pamoja ili kueleweshana taratibu mbalimbali za usimamiaji wa haki nchini ili kuleta hitaji kubwa la kitaifa la kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi yenye haki, utulivu na usawa.’
‘Sisi kama Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania tutaendelea kushirikiana na Wadau kama ilivyotakwa la Katiba yetu, ikizingatia ule uhuru wa Mahakama ambao ndio uhuru wa wanachama wetu wote na kuhakikisha kwamba Tanzania inaendelea kusimamia haki, usawa ambao utasababisha utulivu na kuinua uchumi wa Taifa letu,’ amesema.