- Miradi ya ujenzi Mahakama za kisasa yasambaa nchi nzima
- Jengo la Makao Makuu utalii wa majengo ya Mahakama kimataifa
Na FAUSTINE KAPAMA, INNOCENT KANSHA-Mahakama, Geita
Mahakama ya Tanzania inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa majengo, kupitia Mpango Mkakati wake wa Miaka Mitano unaotekelezwa sambamba na Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu (2020/21-2024/25).
Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 21 Mei, 2025 alipokuwa anazungumza na Waandishi wa Habari kupitia Vyombo mbalimbali mkoani hapa kuhusu maboresho ya miundombinu ya Mahakama katika kipindi maalum cha kila mwezi.
‘Miradi hii inatekelezwa kwa ngazi zote za Mahakama kuanzia Mahakama ya Rufani hadi Mahakama za Mwanzo, kupitia fedha za maendeleo kutoka Serikali Kuu pamoja na ufadhili wa Benki ya Dunia,’ amesema.
Mtendaji Mkuu amewaeleza Waandishi wa Habari kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unapitia katika hatua mbalimbali ambapo usanifu wake umejikita katika kuzingatia vipaumbele vitano.
Amevitaja vipaumbele hivyo kama mazingira bora ya kufanyia kazi katika ofisi mbalimbali na urahisi wa kufikika miundombinu wezeshi kwa makundi maalum,’ amesema.
Mtendaji Mkuu amebainisha vipaumbele vingine kama matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma na uendeshaji wa shughuli za Mahakama, ulinzi na usalama kwa watumiaji wa jengo na muonekano na taswira pekee ya Mahakama.
Prof. Ole Gabriel ametaja miradi ya ujenzi kwa mwaka wa fedha 2024/25 kama ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama-Dodoma na ujenzi wa nyumba za Majaji-Dodoma, ambao umeshakamilika. Majengo hayo yalizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 5 Aprili, 2025.
‘Jengo hili la Makao Makuu ni jengo la kifahari, jengo ambalo ni la kihistoria, jengo ambalo ukubwa wake wa sakafu ni mita za mraba 63,424. Ni jengo la sita kwa ukubwa duniani na la kwanza barani Afrika, ni jengo la heshima na tayari sasa tumeshaanza utalii wa majengo ya kimahakama,’ amesema.
Miradi mingine ni ujenzi wa nyumba ya Jaji Mkuu-Dodoma, ujenzi wa Vituo Jumuishi Tisa vya Utoaji Haki (IJCs) katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Visiwani Pemba, ujenzi wa Mahakama 15 za Wilaya na ujenzi wa Mahakama za Mwanzo katika Wilaya mbalimbali nchini.
Mtendaji Mkuu ameishukuru Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali kutoa mkopo wa gharama nafuu ili kufanikisha baadhi ya ujenzi wa miundombinu. Amebainisha kuwa awamu ya kwanza walipata Dola za Kimarekani million 65 na awamu ya pili Dola za Kimarekani milioni 90.
Kwa mujibu wa Prof. Ole Gabriel, katika awamu ya kwanza walifanikiwa kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita katika Mikoa ya Dar es Salaam (Temeke na Kinondoni), Morogoro, Dodoma, Mwanza na Arusha ambavyo vilizinduliwa kwa pamoja na Mhe. Dkt. Samia terehe 6 Octoba, 2021 jijini Dodoma.
Aliwaeleza Waandishi wa Habari kuwa baada ya kukamilika kwa miradi hiyo, Mahakama ya Tanzania ilifanya upimaji wa kile kilichofanyika na kufanikiwa kuokoa kiasi cha Shilingi za Kitanzania bilioni 3.6 ambazo zilitumika kufanya kazi zingine.
Mtendaji Mkuu ametaja miradi ya ukarabati inayoendelea na utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2024/25 ni jengo la Mahakama Kuu – Musoma, jengo la Mahakama Kuu – Dodoma, jengo la Mahakama Kuu Iringa, nyumba ya Jaji Kiongozi – Dodoma na nyumba ya Jaji Iringa.
Prof. Ole Gabriel ametaja miradi iliyopo katika hatua za usanifu kama nyumba za Majaji Mikoa ya Geita, Tabora na Sumbawanga, majengo ya Mahakama za Wilaya Handeni, Kiteto, Igunga, Mlele, Lushoto na Rufiji na jengo la Mahakama ya Mwanzo Mkomazi.
Ametaja pia ukarabati wa nyumba za Majaji Mkoa wa Mbeya, majengo ya Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi-Dar es Salaam, Mahakama Kuu Mbeya na Mwanza na jengo la Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi – Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa juhudi za kusogeza huduma hizo za Mahakama kwa Wananchi ni katika kutekeleza Dira ya Mahakama, yaani ‘Upatinakanaji wa Haki kwa Wakati na kwa Wote.’
Kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari, Prof. Ole Gabriel alimtembelea Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina na kufanya naye mazungumzo mafupi. Kadhalika, Mtendaji Mkuu alisalimiana na Watumishi wanaohudumu katika Mahakama hiyo.