tz_coa
The United Republic Of Tanzania
The Judiciary Of Tanzania
Timely And Accessible Justice To All
Post Details
MAHAKAMA YA KENYA YAWASILI NCHINI KUJIFUNZA UBORESHAJI HUDUMA ZA UTOAJI HAKI
Post Media
post-media

·        Wavutiwa zaidi na maboresho ya matumizi ya TEHAMA ndani ya Mahakama ya Tanzania

·        Jaji Kiongozi awashauri juu ya matumizi ya 'ADR' kutatua migogoro

·         Awashauri pia juu ya umuhimu kufanyia kazi ongezeko la  'imani ya wananchi' kwa Mhimili huo

 

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya umewasili nchini Tanzania lengo likiwa ni kuitembelea Mahakama ya Tanzania ili kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu uboreshaji wa huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

Ujumbe huo ambao umeongozwa na mkuu wa msafara ambaye ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Winifrida Mokaya umewasili Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 20 Mei, 2025 na kupokelewa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya na Maafisa wengine wa Mahakama nchini.

Aidha, baada ya kuwasili katika viunga vya Makao Makuu wa Mahakama, wageni hao walipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.

Akizungumza na ugeni huo, Mhe. Dkt. Siyani amesema kuwa, ni muhimu kufanya maboresho ndani ya Mahakama kwakuwa Mahakama nyingi ikiwemo za barani Afrika na hata Ulaya zimekuwa zikilalamikiwa kufuatia ucheleweshaji wa utoaji  haki.

Kazi zetu kama Mahakama, kazi za kutoa haki zimekuwa zikilalamikiwa, kote Kenya, Tanzania na karibu kila nchi duniani, wakati fulani nilikuwa nikifanya tafiti nikifikiri kwamba wenzetu katika nchi zilizoendelea hakuna ucheleweshaji wa utoaji haki lakini hali haiko hivyo, kuna milundikano pia tuna matatizo yanayofanana karibu kila mahali, amesema Mhe. Dkt. Siyani.

Amesema kuwa, ili kuleta maboresho katika huduma ya utoaji haki kuna umuhimu wa kuangalia upya michakato/ taratibu za utoaji haki katika kila eneo (business process re-engineering).

Ametoa rai kwa ugeni huo kuhakikisha wanajua wanachofanya ili kutekeleza jukumu la msingi ambalo Wakenya wamewapa la utoaji haki kwa haraka. Ameongeza kuwa, eneo la matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni muhimu kuzingatiwa katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.

Hakuna namna yoyote tunaweza kuendesha au kubadili taratibu za utoaji huduma bila kuhusisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), michakato yetu ya utoaji haki ndio iliyofanya kuwa na ucheleweshaji pamoja na mambo mengine, lakini kama tunaweza kubadili namna tunavyotoa haki tunaweza kuharakisha upatikanaji wa haki, amesisitiza Jaji Kiongozi.

Aidha, Jaji Kiongozi amesema kuwa, jambo lingine ambalo linapaswa kuangaliwa ili kuharakisha huduma ya utoaji haki ni matumizi ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala/ usuluhishi (Alternative Dispute Resolution) kwa kuwa inasaidia kupunguza muda wa kusikiliza mashauri kama ilivyo katika usikilizaji wa mashauri kwa njia ya kawaida.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Siyani amewakumbusha wageni hao kutoka Mahakama ya Kenya juu ya umuhimu wa Mahakama kupata imani ya wananchi, ambapo amesisitiza kwa kusema kuwa, kwa Mahakama imani ya wananchi ni mtaji, chochote mtakachofanya hakikisheni wananchi wanawaamini.

Ameongeza kwa kuueleza ujumbe huo kwamba, ili kuboresha huduma ya utoaji haki kuna umuhimu wa wao kuweka malengo yanayokubalika ili kuwapima Maafisa Mahakama wakiwemo Majaji na Mahakimu waliokasimiwa jukumu la kusikiliza mashauri ili waweze kusikiliza kwa wakati.

 Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Winifrida Mokaya amesema kuwa, ziara yao imelenga katika kujifunza kuhusu maboresho mbalimbali ikiwemo matumizi ya TEHAMA, masuala ya ushirikishwaji wa wadau katika masuala ya Mahakama, Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) na kadhalika.

Mahakama tuna mipango kadhaa ya maboresho ya utoaji huduma ya haki kwa kuondoa vikwazo vinavyozuia upatikanaji wa haki kwa wakati, ambayo hivyo ziara yetu imejikita kujifunza kuhusu maboresho mbalimbali ambayo Mahakama ya Tanzania mmefanikiwa kufanya ambayo ni pamoja na matumizi ya TEHAMA, utoaji huduma katika Mahakama zinazotembelea (Mobile Court Services), Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs), amesema Mhe. Mokaya.

Aidha, Mhe. Mokaya amesema kuwa, eneo lingine ambalo wanatamani kuliona na kujifunza jinsi linavyofanya kazi ni Chumba maalum cha kutolea taarifa za Mahakama (Judiciary Situation Room) kwakuwa nao wana mpango wa kuanzisha chumba hicho muhimu.

Kwa upande wake Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Nkya ameuhakikishia ujumbe huo kuwa, kile walichokusudia kukipata kutoka Mahakama ya Tanzania watapata kwakuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatoa majibu ya maswali yao kupitia mawasilisho mbalimbali yaliyoandaliwa kwa ajili ya ujumbe huo.

Aidha, Msajili Mkuu ameueleza ujumbe huo kuwa, historia ya maboresho ya Mahakama nchini ilianza miaka ya nyuma na ripoti za Kihistoria, kama vile Tume ya Msekwa ya 1977 na Ripoti ya Bomani ya 1986, ziliangazia masuala muhimu ambayo yanazuia ufanisi wa Mahakama, ambapo zilipendekeza juu ya  marekebisho ya kimuundo na ufadhili wa kutosha.

Mabadiliko makubwa yalikuja mwaka 2011 kwa kupitishwa kwa Sheria ya Utawala wa Mahakama, ambayo ilianzisha ofisi za Msajili Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, pamoja na Mfuko wa Mahakama, hii iliashiria mwanzo wa Mpango wa Mageuzi unaoongozwa na Mahakama ambao unasisitiza kuboresha upatikanaji wa haki, kuongeza ufanisi wa mahakama, kuhakikisha uwazi, na kukuza ushiriki wa raia, amesema Mhe. Nkya.

Aidha, amewaeleza wajumbe kutoka Mahakama ya Kenya kuwa, Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA katika shughuli zake na hivyo kuwezesha upatikanaji wa haki kwa haraka.

Baada ya hafla fupi ya kuwakaribisha wageni hao, walipata wasilisho kutoka Mkurugenzi Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hawa Mnguruta ambaye aliwasilisha kuhusu namna ambavyo Mahakama ilivyofanya marekebisho katika mchakato mzima wa kuendesha shughuli zake (business process re-engineering) na mada kuhusu Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) ambapo wamepata nafasi ya kuuliza maswali na kujibiwa.

Programu ya ujumbe huo kutoka Mahakama ya Kenya ni ya siku tano. Siku ya kwanza ya ziara yao tarehe 19 Mei, 2025 ujumbe huo ulipata fursa ya kutembelea Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam.