Na MARY GWERA, Mahakama-Cape Town
Mkutano wa 17 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) umehitimishwa huku wanachama wa Chama hicho wakisisitizwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.
Akifunga mkutano huo mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwakilishi wa Jaji Mkuu wa Afrika Kusini ambaye ni Jaji wa Mahakama Kikatiba ya Nchi hiyo, Mhe. Nonkosi Mhlantla aliwataka washiriki wa mkutano huo kujithamini na kujipenda sambamba na kutosahau waliyojifunza wakati wote wa mkutano huo.
“Nawasihi kutosahau kupitia mliyojifunza mtapata uzoefu mzuri, Majaji mbalimbali walipata nafasi ya kuchangia uzoefu wao juu ya namna wanavyoshughulikia mashauri yanayohusu vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na mauaji ya wanawake, hivyo ni muhimu kujifunza na kuyaishi yote mazuri tuliyoyapata,” alisema Mhe. Mhlantla.
Jaji huyo aliwakumbusha Majaji na Mahakimu wanawake kujipenda na kujithamini kwanza ambapo alisema, “ni muhimu kujipenda na kujithamini, kufanya hivyo sio ubinafsi bali ni muhimu kufanya hivyo ili tuwe katika nafasi nzuri ya kutekeleza vizuri majukumu yetu ipasavyo,” alisisitiza.
Aidha, Jaji Mhlantla alisema kuwa, bado Mahakama nyingi hazina mbinu za kiusalama katika kuwalinda wahanga wa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia huku na kusema kwamba kuna haja ya kuchukua hatua thabiti ili kuwalinda watu hao.
Mgeni Rasmi huyo alizikumbusha pia nchi wanachama wa IAWJ kufanya uanaharakati ndani ya Mahakama hususani unaohusiana na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hususani akili unde ili kushughulikia matatizo mbalimbali yaliyopo ndani ya Mahakama ambayo ni pamoja na mlundikano wa mashauri.
Wakati wa mkutano huo uliofanyika kwa siku nne mada mbalimbali ziliwasilishwa ambazo ni pamoja na Majaji wanawake wanaongoza kuleta mabadiliko katika Mahakama za Kimataifa, Wanawake katika Uongozi-Mahali pa Kazi Usalama kwa Maafisa wa Mahakama, Ubaguzi na biashara haramu ya binadamu na nyingine.
Mada nyingine iliwasilishwa na Mhe. Edith Mwalukasa, Hakimu kutoka Mahakama ya Mwanzo Bagamoyo Tanzania mada hiyo ilijikita kuzungumzia ‘Athari za teknolojia katika masuala ya ukatili wa kijinsia.’
Aidha, wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Chama hicho, wanachama wa IAWJ walifanya uchaguzi na kumchagua Rais mpya wa Chama hicho ambaye ni Mhe. Maria Filomena D. Singh kutoka nchini Morocco.
Mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili umeazimia kuwa, Mkutano ujao wa mwaka 2027 utafanyikia nchini Canada.