tz_coa
The United Republic Of Tanzania
The Judiciary Of Tanzania
Timely And Accessible Justice To All
Post Details
JAJI KIONGOZI AANZA ZIARA MAHAKAMA KUU KANDA YA TABORA
Post Media
post-media

• Awasisitiza watumishi wa Mahakama kujipanga thabiti kurejesha Imani ya wananchi kwa Mahakama

Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani ameanza ziara ya kikazi katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora lengo likiwa ni kukagua shughuli za Mahakama na kukutana na watumishi kuwasikiliza, kutatua changamoto zao, kuwapa motisha sambamba na kuhimiza utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia maadili ya kazi. 

Katika siku ya kwanza ya ziara yake jana tarehe 24 Machi 2025, Mhe. Dkt. Siyani alitembelea katika Wilaya za Igunga, Nzega na Uyui na kufanya mazungumzo na watumishi wa Mahakama hizo.

Akiwa katika ziara hiyo, Jaji Kiongozi aliwataka watumishi kufanya kazi kwa moyo na kujenga utamaduni wa kujituma katika utendaji wao huku akisisitiza juu ya umuhimu wa kuweka malengo ya kazi na kuyafikia, kuzingatia viwango vya juu vya maadili katika utendaji kazi. 

“Ni muhimu kwa watumishi wa Mahakama kufanya kazi kwa moyo na kujenga utamaduni wa kujituma katika utendaji wao, kila mtumishi anapaswa kuweka malengo ya kazi ya wazi na kuyafikia kwa ufanisi, huku akizingatia viwango vya juu vya maadili katika utendaji wake. Vilevile viongozi wa Mahakama na Kamati za Maadili wanapaswa kusimamia nidhamu kwa ukamilifu na kuchukua hatua stahiki dhidi ya maofisa watakaobainika kukiuka maadili ya kazi. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba Mahakama inabaki kuwa chombo cha kuaminika kinachotoa haki kwa usawa na kwa kuzingatia maadili,” alisema Mhe.Dkt. Siyani.

Kadhalika, Jaji Kiongozi aliwahimiza Viongozi wa Mahakama na Kamati za Maadili kusimamia nidhamu na kuchukua hatua stahiki dhidi ya maofisa watakaobainika kukiuka maadili ya kazi.

Aidha, Jaji Kiongozi pia alikumbusha juu ya umuhimu wa kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama, huku akisisitiza kuwa hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa ili kurejesha imani kwa wananchi ili kuhakikisha utoaji haki unaenda sambamba na wananchi kuiamini Mahakama na mfumo wa mzima wa utoaji haki.

“Ni muhimu sana, tunapaswa kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama. Sisi watumishi wa Mahakama lazima tuchukue hatua thabiti ili kurejesha imani hiyo kwa kuhakikisha kwamba utoaji haki unakwenda sambamba na wananchi kuiamini Mahakama pamoja na mfumo mzima wa utoaji haki, Mahakama inapaswa kuwa ni chombo cha haki kinachozingatia uwazi, usawa na maadili ili wananchi wawe na imani katika mfumo wetu wa haki," alisisitiza Mhe. Dkt. Siyani.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)