• Kikao chakamilisha usikilizaji wa mashauri yote 10 yaliyopangwa
Na HUBERT MAANGA, Mahakama-Mtwara
Kikao cha Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara kilichofanyika kuanzia tarehe 24 Februari hadi 13 Machi, 2025 kikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Martha Mpaze kimekamilisha usikilizaji wa mashauri yote 10 yaliyopangwa.
Imebainishwa hivi karibuni kuwa, kati ya mashauri hayo, nane yamekwisha kutolewa uamuzi huku mashauri mawili yakiwa bado yanangoja uamuzi wake.
Mhe. Mpaze alitoa pongezi kwa wadau wote waliohusika, wakiwemo Mahakama, Ofisi za Taifa ya Mashtaka za Mikoa ya Lindi na Mtwara, Mawakili wa Kujitegemea, Magereza na Polisi kwa ushirikiano wao, kujituma na kuzingatia muda katika mchakato mzima wa usikilizaji wa mashauri uliowezesha kukamilisha usikilizaji wa mashauri kabla ya muda uliopangwa.
Akizungumza na wadau, Jaji Mpaze alisema, "napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu alietupa uzima na afya njema ya kusimama na kusikiliza mashauri yote haya mwanzo mpaka mwisho kwani ni kwa kudra zake tumefanikiwa kwa kiasi hiki. Nipende kuwapa pongezi Ofisi za Mashtaka Mkoa, Uongozi Magereza pamoja na Mawakili kwa kuwajibika ipasavyo.”
Aliongeza kwa kuwashukuru, Mawakili kwani waliweza kujiratibu vizuri na kuandaa mashahidi ambao waliweza kufika ndani ya muda na pia uongozi wa Magereza nao waliwafikisha watuhumiwa mapema kwa kuzingatia muda uliopangwa wa kusikiliza mashauri kwakuwa juhudi hizo ziliwezesha kumaliza mashauri yote mapema.
Viongozi mbalimbali walioshiriki katika kikao hicho walimpongeza Jaji Mpaze kwa uongozi wake thabiti na mipango madhubuti iliyowekwa tangu mwanzo wa kikao.
Mhe. Mpaze alihitimisha kikao hicho kwa kuhimiza wadau wote kuendeleza ushirikiano huo katika vikao vijavyo huku akisisitiza kuwa kwa ushirikiano, wanaweza kufanikisha mengi kwa wakati mfupi.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)