tz_coa
The United Republic Of Tanzania
The Judiciary Of Tanzania
Timely And Accessible Justice To All
Post Details
MTENDAJI MKUU ATETA NA UJUMBE WA BENKI YA DUNIA
Post Media
post-media

Na INNOCENT KANSHA-Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel tarehe 18 Machi, 2025 amekutana na Ujumbe wa Banki ya Dunia na kufanya mazungumzo ya kina juu ya shughuli za maboresho yanayoendelea kutekelezwa na Mahakama kupitia ufadhili wa Banki hiyo.

Akizungumza na Ujumbe huo ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma, Prof. Ole Gabriel ameushukuru ujumbe huo kutoka Banki ya Dunia kwa namna unavyoendela kutoa ushirikiano na ushauri katika maeneo mbambali ili kufanikisha utekelezaji wa mradi ya uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma za haki nchini.

“Jambo la msingi ninalotaka kuwahakikishia ni kwamba, tutasimamia miradi yote kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu, kwa viwango vinavyokubalika, hatutayumbishwa katika kusimamia na tutahakikisha tunasimamia kwa kuzingatia ubora unaokubalika kitaalam, kwani wataalum wa ndani wapo wa kutosha kuhakikisha miradi tunayoiendesha yote inakamilika kwa kuzingatia thamani ya fedha,” amesisitiza Mtendaji Mkuu.

Vilevile Prof. Ole Gabriel ameuambia ujumbe huo kuwa Mahakama itahakikisha inasimamia ubora, usalama wa miradi na kuhakikisha kasi ya utekelezaji wa miradi inakwenda kama ilivyopangwa bila kuathiri ubora wa miradi ya miundombinu inayoendelea kutekelezwa.

Aidha, Mtendaji Mkuu ameuhakikishia ujumbe huo kwamba ni matarajio ya Mahakama ya Tanzania kuwa ndani ya kipindi cha miezi sita hadi kufikia Desemba 31, 2025 miradi yote ya ujenzi wa miundombinu itakayotumika kutolea haki itakuwa imekamilika kwa asilimia 100.

“Kukamilika kwa miradi hiyo itakuwa suluhisho la kudumu kwa wananchi hasa wale wenye mahitaji maalum wanaohangaika kuzifikia huduma za haki nchini. Aidha, amesisitiza kuwa Mahakama itaendelea na jitihada za kuboresha huduma hizo katika ngazi mbalimbali za kimahakama na kuhakikisha Mahakama inamfuata mwananchi badala ya mwananchi kuifuata Mahakama,” ameongeza Prof. Ole Gabriel.  

Akiongoza Ujumbe kutoka Banki ya Dunia uliomtembea Mtendaji Mkuu wa Mahakama ofisini kwake, Meneja Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa Mashariki mwa Afrika Bw. Manuel Vargas amesema, “ni fahari kubwa kwa Banki ya Dunia na timu nzima ya ushauri iliyoko hapa kuwa sehemu ya mafanikio haya yaliyofikiwa na Mahakama ya Tanzania katika hatua nzuri za kuboresha ya mifumo ya utoaji haki kwa wananchi,” Bw. Vargas.

Meneja Mtendaji huyo Bw. Vargas ameongeza kuwa, Miradi ya Mahakama inayotekelezwa ambayo Banki ya Dunia imekuwa mshirika inaonyesha taswira ya utengamano na ushirikiano imara hasa katika kutekeleza malengo ya pamoja yaliyokusudiwa ya kumsongezea mwananchi huduma ya utoaji haki karibu zaidi.

“Ikiwa mradi huu wa maboresho ya miundombinu na matumizi TEHAMA unaelekea ukingoni ni matarajio ya Banki ya Dunia kuona unakamilika na kutimiza adhima iliyokusudiwa na kuacha alama kubwa kwa Jamii, Taasisi na Serikali ya Tanzania,” amesema Bw. Vargas.

Vilevile, Bw. Vargas amefafanua kuwa, Benki ya Dunia na timu nzima itaendelea kutoa ushirikiano na kupanua wigo katika ufadhili kwa maeneo mengine muhimu kama vile kukuza masuala ya usuluhishi (ADR), matumizi ya akili mnemba (IA) na matumizi ya TEHAMA kwa ujumla ili kuongeza ufanisi katika shughuli za utoaji haki.

“Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika kuhakikisha inaimarisha miundombinu ya kuwezesha urahisi wa utoaji haki kwa wananchi, mathalani tumeona ujenzi wa kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kisiwani Pemba huko Zanzibar. Banki ya Dunia inaona fahari ya kuendelea kufanya kazi na Mahakama ili kuboresha zaidi sekta hii,” ameongeza Bw. Vargas.