Na LUSAKO MWANGONDA, Mahakama-Iringa
Mahakimu wa Mahakama Kanda ya Iringa wamepata semina maalum kuhusu matumizi ya Mfumo wa Kidigitali wa Tathimini na Mapitio ya Utendaji kwa Maafisa wa Mahakama (e-JOPRAS) na maadili.
Mafunzo hayo yalifunguliwa tarehe 15 Machi, 2025 na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Angaza Mwipopo katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Mwipopo aliwasihi Mahakimu kuwasikiliza kwa makini wataalamu wa Teknolojia ya Habari, Elimu na Mawasiliano (TEHAMA) wanaofundisha kuhusu Mfumo wa ‘e-OPRAS, kwakuwa ni Mfumo muhimu kwao maana ndiyo utakaotumika kufanya tathmini ya utendaji kazi wao wa siku kwa siku.
“Tumeitana hapa kwa ajili ya mambo mawili kwa wakati mmoja, tunataka wataalamu wetu wa TEHAMA watupitishe kwenye mfumo wa ‘e-JOPRAS’ ambao ni muhimu sana kwa kila Afisa wa Mahakama maana ndio utakaotuma kufanyiana tathimini ya utendaji. Kadhalika tumewaita wataalamu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) watupitishe na kutukumbusha kwenye suala la Maadili kwakuwa ni muhimu mno kwetu kufanya kazi zetu kwa kuzingatia maadili na kuikataa rushwa kwakuwa ni mbaya, mla rushwa anakuwa amenunuliwa akili na baadaye hutoa maamuzi yasiyo ya haki,” alisema Mhe. Mwipopo.
Kuhusu suala la maadili, Jaji Mwipopo aliwahimiza Mahakimu hao kuwasikiliza kwa makini wataalamu wa TAKUKURU ambao watakuwa wanafundisha kuhusu mada ya Maadili.
Naye, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku alisisitiza juu ya matumizi ya TEHAMA katika usikilizaji wa mashauri na kuzingatia nyaraka mbalimbali zilizotelewa na Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi na Msajili Mkuu na kuwaomba watumishi kuendelea kusimamia mikakati iliyowekwa ambayo itasaidia kupunguza mlundikano wa mashauri.
Wakizungumza baada ya mafunzo hayo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mufindi, Mhe. Sekela Kyungu na Mhe. Hassan Mlanga ambaye ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo ya Bomani waliushukuru uongozi wa Mahakama kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo wanaamini yataleta tija katika utendaji wa kazi za Mahakimu wa Kanda ya Iringa.
Mafunzo haya yaliratibiwa na uongozi wa Mahakama Kanda ya Iringa, ambapo Mada kuhusu mfumo wa utendaji kazi wa mfumo wa e-JOPRAS ilifundishwa na Wataalamu wa TEHAMA wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa huku mada kuhusu Maadili kwa Maafisa wa Mahakama ikifundishwa wa Wataalamu kutoka TAKUKURU Mkoa wa Iringa.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)