Post Details

MAJAJI WAPYA WA MAHAKAMA YA RUFANI NA MAHAKAMA KUU WAAPISHWA JANUARI 29, 2019

Published By:JoT Admin

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Majaji wapya aliowaapisha kutenda haki kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza katika hafla ya kuwaapisha Majaji hao iliyofanyika Januari 29, Ikulu jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais amesema kazi ya kusimamia haki ni ngumu, hivyo inahitaji kumtanguliza Mwenyezi Mungu.

“Mna jukumu kubwa la kusimamia haki, lakini mkamtangulize Mwenyezi Mungu, mkasimamie haki iliyo ya kweli,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amempongeza na kumshukuru Mhe. Rais kwa kufanya uteuzi wenye idadi kubwa ya wanawake.

Mhe. Samia alisema kwa idadi hiyo ya Majaji wanawake anaamini masuala mbalimbali yaliyokubaliwa katika Mkutano wa Arusha kuhusu Mahakama na Jinsia pamoja na ule wa Zanzibar wa Majaji wanawake yatatekelezwa ipasavyo.

Awali kabla ya kumkaribisha Mhe. Rais, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma amesema uteuzi wa Majaji wapya umeongeza idadi yao kutoka 66 hadi kufikia 81.

Ametoa wito kwa Majaji wapya kufanya kazi kwa bidii na unyenyekevu wa hali ya juu huku akiwataka kujali na kulinda afya zao za mwili, akili na roho. Amesisitiza pia juu ya utayari wao wa kufanya kazi kwenye kituo chochote cha kazi watakachopangiwa.

Aidha Mhe. Jaji Mkuu ameonyesha kuwepo kwa hitaji la Majaji wengi Zaidi na kuainisha sababu za hitaji hilo.

“ Bado upo umuhimu wa Majaji kuongezeka hadi kufikia 100 au150 kwa kuwa uelewa wa haki umeongezeka na wanachi wanaijua haki na wanakwenda Mahakamani na pia ujenzi wa majengo ya Mahakama sehemu mbalimbali za nchi utaleta hitaji la kuwa na Majaji wengi zaidi,” alisema Jaji Mkuu.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli aliwaapisha Majaji sita wa Mahakama ya Rufani, ambao ni Mhe. Winfrida Korosso, Mhe. Barke Sahel, Mhe. Lugano Mwandambo, Mhe. Dkt. Mary Calorine Levira, Mhe. Ignas Kitusi na Mhe. Rehema Sameji.

Rais pia amewaapisha Majaji wa Mahakama Kuu, ambao ni Mhe. John Kahyoza , Mhe. Suzan Mkapa, Mhe. Fahamu Mtulya, Mhe Cyprian Mkeha, Mhe. Wilbard Mashauri, Mhe. Dustan Ndunguru, Mhe. Seif Kulita, Mhe. Upendo Madeha.

Wengine ni Mhe. Yohane Masara, Mhe. Mustapha Ismail, Mhe. Athman Kirati, Mhe. Zephrine Galeba, Mhe. Ntemi Kirikamajenga, Mhe. Juliana Masabo na Mhe. Lilian Mongela.

Katika hafla hiyo Majaji wapya, Wakuu wa Wilaya 2 na Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya 10 walikula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma.

Comments (0)

Leave a Comment