Post Details

MAHAKAMA KUU KANDA MPYA YA KIGOMA YAJIPANGA KUDHIBITI MLUNDIKANO WA MASHAURI

Published By:Mary C. Gwera

Mahakama kuu Kanda ya Kigoma imeendesha kikao chake cha kwanza cha mashauriano na wadau (caseflow management) tangu kuanzishwa kwake rasmi na Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Tanzania kwa tangazo la Serikali namba 112 la Februari 1, 2019.

Akifungua kikao hicho mapema Agosti 6, 2019 kilichofanyika katika Jengo la Hakimu Mkazi Kigoma, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Ilvin  Mugeta aliwasilisha maeneo makuu matatu katika kuhakikisha Kanda ya Kigoma inakuwa ya mfano kwa kumaliza mashauri kwa wakati ili kuondokana na mrundikano na kupunguza Idadi ya Mahabusu katika Magereza.

“Baadhi ya maeneo yenye changamoto ni pamoja na baadhi ya Wadau wetu kutotimiza wajibu ipasavyo, mawasiliano yasiyoridhisha baina ya mtu na mtu, Taasisi kwa Taasisi pamoja na uwezo mdogo wa wadau wetu katika upelelezi imekuwa ni changamoto inayokwamisha adhima yetu ya upatikanaji wa haki kwa wakati” alieleza Mhe. Jaji Mugeta

Mhe Jaji huyo Mfawidhi alitoa maelekezo juu ya kuwa na  mwelekeo sahihi wa kanda na namna bora itakayoleta matokeo chanya kwa kuwaeleza wajumbe kuhahakikisha wanaweka mfumo wa uwajibikaji wa pamoja na kuweka maazimio ya pamoja ikiwa sambamba na kuweka viwango vya kupimika katika utendaji kazi wa kila siku.

Aidha aliwasisitiza wajumbe kufungua milango ya mawasiliano ili kuhakikisha wanafikiana kwa wakati na kupeana taarifa stahiki ikiwa ni pamoja na kila mjumbe kutambua wajibu wake na kuongeza kuwa upelelezi unapochukua muda mrefu hupelekea kupotea kwa haki za watu.

Akisoma taarifa  ya Kanda hiyo, naye Naibu Msajili wa Kanda hiyo, Mhe. Hussein Mushi aliwaeleza wajumbe kuwa tangu kuanzishwa kwake mapema mwezi February, 2019 hadi mwezi Julai, 2019  masjala ya Mahakama kuu kanda ya Kigoma imesajili jumla ya mashauri 59 ya jinai pekee, mashauri 12 yaliamuliwa na mashauri 47 yamebaki.

Kamati ya kusukuma mashauri kanda ya Kigoma kwa pamoja walikubaliana kushirikiana katika kuhakikisha wanaondokana na mlundikano wa mashauri na Mahabusu kwa kila mjumbe kutimiza wajibu wake kikamilifu.

Aidha baada ya kikao wajumbe walipata fursa ya kutembelea Jengo la Mahakama Kuu lililopo katika eneo la Bangwe mkabala na shule ya Sekondari Kigoma ambako liko katika hatua za mwisho za ujenzi wake.

Wajumbe waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Jaji Mfawidhi wa Kanda, Naibu Msajili, Mtendaji wa Mahakama-Kigoma, Hakimu Mkazi Mfawidhi(M), Mkuu wa Mashtaka Kigoma (M), Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kigoma, Wawakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Polisi, Mkuu wa Upelelezi, Mkuu wa Gereza la Bangwe. na Katibu wa Jukwaa la Mawakili wa kujitegemea Kigoma (M).

Comments (0)

Leave a Comment