Post Details

MAHAKAMA YA TANZANIA YAINGIA KWENYE MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO

Published By:Mary C. Gwera

Mahakama ya Tanzania  leo imeingia Mkataba na Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) utakaowezesha Mahakama kuingizwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano  ambapo majengo 157 ya Mahakama nchini yataunganishwa. 

Akizungumza kabla ya kusainiwa kwa Mkataba huo, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock, alisema  mkataba huo wenye thamani ya Sh. bilioni 4.1 utawezesha kuunganishwa kwa majengo ya Mahakama kuanzia Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu,   Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na baadhi ya Mahakama za Mwanzo zenye majengo ya kisasa.

Alizitaja Mahakama ambazo zitaunganishwa kwenye mtandao huo kuwa ni Mahakama ya Rufani 1, Mahakama Kuu  16, Mahakama Kuu Maalumu (Specialized Division 4, Mahakama za Mkoa 29, Mahakama za Wilaya 112 na Mahakama za Mwanzo 10.

‘Lengo kuu ni kuunda mtandao mpana wa Mahakama utakao unganisha Mahakama zote  nchini  pia kuunganishwa  pamoja na mtandao wa serikali yaani (Government Network (Gov Net) ili kuhakikisha huduma zote za serikali mtandao zinapatikana kwa urahisi pia kuiwezesha Mahakama kutoa huduma kwa wakati na wakati na  umadhubuti,’ alisisitiza.

Bw. Enock  alisema  faida ya mkongo huo ni kurahisisha upatikanaji wa huduma za mahakama kwa kupitia mifumo yake ya  kielektroniki kama vile Mfumo wa kuendesha na kuratibu Mashauri (JSDS2) na Mfumo wa kuratibu Mawakili (TAMS), mazingira wezeshi ya kubadilishana taarifa kati ya Mahakama na Taasisi, wadau katika mfumo mzima wa utoaji haki nchini.

Aliwataja wadau hao kuwa Magereza, Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka, TAKUKURU, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Chama cha Mawakili(TLS).

Faida nyingine ni kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi/haraka kupitia mifumo ya kielektroniki ya Mahakama wakati wote na kutoka mahali popote, kurahisisha upatikanaji wa taarifa mbalimbali hasa mwenendo wa mashauri na shughuli za Mahakama kwa wananchi na wadau wengine kwa ujumla.

Aliongeza kuwa faida nyingine ni kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za Mahakama, mfano, shahidi anaweza kuwasilisha ushahidi bila kulazimika kufika Mahakamani, wakili au wananchi anaweza kufungua shitaka au shauri kwa njia ya mtandao, na kuimarika kwa shughuli za kila siku za Mahakama kwa kuongeza ufanisi na weledi hivyo kuwezesha upatikanaji wa Haki kwa wakati.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw, Waziri Waziri Kindamba alisema Shirika lake litahakikisha wanafanya kazi kwa bidii ili kuwezesha Mahakama kuingia kwenye mtandao.

“Tutafanya kazi usiku na mchana ili tuweze kutekeleza hili kwa wakati, tena ikibidi kumaliza kabla ya muda uliopangwa katika mkataba wetu, alisisitiza Bw. huo.

Alisema tayari vifaa vimeshasambazwa katika baadhi ya Mahakama na ujenzi umeshaanza, hivyo watajitahidi kumaliza kazi kabla ya muda.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama  ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga alisema mkataba huo utakuwa ukiendeshwa kwa hatua, ambapo utaanza na wiki 14 za usambazaji wa vifaa na utakuwa endelevu kwa kipindi cha miaka miwili.

Mahakama ya Tanzania imesaini mkataba huo, ikiwa inatekeleza Mpango Mkakati wake wa Miaka Mitano ( Julai 2015 hadi Juni 2020), ambapo moja ya malengo  yake ni kuongeza ufanisi katika mtiririko mzima wa shughuli za Mahakama na hatua hii itafikiwa kwa kupanua matumizi ya Tehama katika ngazi zote za Mahakama ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wakati na pia kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi .

Comments (2)

  • Photo Loading... MSECHU.JAMES

    JAMANI MBONA JSDS UNAKATAA KU UP TO DATE KESI JE KUNATATIZO

    05-08-2019
  • Photo Loading... Administrator

    Bw. Msechu, tatizo hili limefikishwa kwa Idara husika, linafanyiwa kazi. Asante

    06-08-2019

Leave a Comment