Post Details

MAONESHO YA WIKI YA SHERIA KUFANYIKA KITAIFA JIJINI DODOMA: KILELE CHA SIKU YA SHERIA FEBRUARI 06

Published By:JoT Admin

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Wasajili wa Mahakama nchini kuwa makini katika usajili wa mashauri kwa kuzingatia taratibu za kisheria zilizopo ili kuondokana na ucheleweshaji wa kesi hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema Januari 25 mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa endapo kesi zitasajiliwa bila kufuata taratibu za msingi ni dhahiri kuwa kesi husika zitaleta changamoto katika mwenendo mzima wa usikilizaji kit kinachoweza kpelekea kesi kufutwa na haki kupotea.
“Mahakama ni Mhimili ambao upo wazi na unafanya kazi zake kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo, kwahiyo ni vyema kufuata taratibu hizo ili haki itendeke kwa wakati,” alisema Mhe. Prof. Juma.

Mhe. Jaji Mkuu aliyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini kwa mwaka huu ambapo amewataka Wananchi ambao ndio Wadau wakuu wa Mahakama kutembelea Maonesho yatakayofanyika kote nchini ili kupata elimu ya Sheria.

“Katika kutimiza wajibu wake wa Kikatiba wa kutoa haki, Mahakama imekuwa ikikumbana na changamoto zinazohusiana na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu sheria na taratibu zinazoongoza mashauri hivyo ni wito kwa wananchi wenye malalamiko/dukuduku kutumia wiki hii kupata elimu badala ya kubeba mabango ya malalamiko kwenye kilele cha siku ya Sheria,” alisema. Mhe.Jaji, Prof. Juma.

Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa, kwa mwaka huu Maonesho ya Wiki ya Sheria nchini kwa upande wa Makao Makuu ya Mahakama yatafanyika kitaifa mkoani Dodoma, na Kanda nyingine zitafanya Maonesho hayo Kikanda.

“Maonesho ya utoaji wa elimu ya sheria na shughuli za Mahakama kitaifa yatafanyika katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ Jijini Dodoma kuanzia Januari 31, 2019 na kuhitimishwa na Siku ya Sheria itakayofanyika Februari 06 jijini Dar es Salaam katika kiwanja cha Mahakama, mtaa wa Chimala karibu na Hospitali ya ‘Ocean road’ kuanzia saa 03:00 asubuhi. Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.

Aidha, Mhe. Jaji Mkuu alibainisha kuwa Maadhimisho haya yanaashiria kuanza rasmi kwa mwaka mpya wa shughuli za Mahakama huku Maudhui ya mwaka huu yakiwa ni “Utoaji wa Haki kwa wakati; Wajibu wa Mahakama na Wadau.”

Aliongeza kuwa maudhui haya yana maana kubwa kwa kuwa pamoja na jitihada zote za maboresho zinazofanywa na Mahakama ni ukweli kuwa Mahakama haiwezi kutimiza wajibu wake na kufikia Dira iliyojiwekea pasipokuwa na ushirikiano kutoka kwa Wananchi na Wadau wengine wa Mahakama.

Mhe. Jaji Mkuu alisema katika Wiki ya Sheria, Mahakama itashirikiana na Wadau wake katika Sekta ya Sheria kutoa elimu juu ya taratibu za ufunguaji wa mashauri, sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri, taratibu za mashauri ya mirathi na ardhi, msaada wa kisheria, usikilizwaji wa malalamiko na kadhalika.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa Wiki ya utoaji wa elimu ya sheria kitaifa itazinduliwa rasmi jijini Dodoma Februari 02 kwa matembezi ya hisani yatakayoongozwa na Mhe. Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa.

Pamoja na utoaji elimu kwa umma, Mahakama itayatumia Maonesho ya Sheria kueleza hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (5) (2015/2016-2020/2021).

Maadhimisho ya Wiki ya utoaji Elimu ya Sheria na Siku ya Sheria nchini huadhimishwa kila mwaka kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika, kwa upande wa Dar es Salaam Maonesho hayo yatafanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia Januari 31 hadi Februari 05, 2019.

Comments (2)

  • Photo Loading... Joh

    Haya maadhimisho, kwa kanda ya Dar yatafanyika wapi.

    01-02-2019
  • Photo Loading... Administrator

    Habari Joh, Kwa Dar es salaam yanafanyika viwanja vya mnazi mmoja tangu tarehe 31/01/2019 mpaka tarehe 05/02/2019.Na kilele ni tarehe 06/02/2019.Karibu

    02-02-2019

Leave a Comment