Post Details

JAJI MKUU MSTAAFU: KIONGOZI ALIYELETA MABADILIKO NDANI YA MAHAKAMA

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemuelezea Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman kuwa ni Kiongozi aliyeleta mageuzi makubwa ndani ya Mahakama hasa katika kuongeza uwajibikaji kwa watumishi.

Akizungumza kwenye hafla maalum ya kumuaga kitaalum Mhe. Chande iliyofanyika Julai 02, 2019  jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu alisema, miongoni mwa mageuzi makubwa aliyoyaanzisha Jaji Chande ni pamoja na kuweka mkakati wa kuhakikisha kesi zinamalizika kwa wakati Mahakamani.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, vigezo hivyo ni pamoja na kupanga idadi ya mashauri yanayotakiwa kusikilizwa na kumalizwa na Wahe. Majaji na Mahakimu pamoja na muda wa mashauri hayo kukaa kwenye Mahakama mbalimbali. Alisema Majaji wanatakiwa kumaliza jumla ya mashauri 220 na Mahakimu mashauri 250 katika kipindi cha mwaka moja.

Aidha, shauri katika Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu linapaswa kumalizika ndani ya miaka miwili ambapo katika Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya shauri linatakiwa kukamilika  ndani ya miezi 12 na mahakama za Mwanzo shauri linapaswa kumalizika ndani ya miezi sita.

Mhe. Prof. Juma alisema Jaji Mhe. Chande ndiye aliyeanzisha mabadiliko ndani ya Mahakama kwa kuandaa Mpango Mkakati wa Miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania (2015/16 hadi 2019/20) mpango unaotatua changamoto mbalimbali zinazoukabili Mhimili huo ikiwemo uhaba na uchakavu wa majengo ya Mahakama nchini.

Alisema kuwa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania unatoa mwelekeo wa nini cha kufanya ili kufikia upatikanaji wa haki kwa wakati. Aliongeza kuwa mpango huo pia umewezesha Mahakama kuwa karibu zaidi na wadau wake na kusaidia mashauri kumalizika kwa wakati.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu Mstaafu amesema vitendo vya rushwa ndani ya Mhimili wa Mahakama huhatarisha uhuru wa Mahakama na hivyo kuwataka watumishi kujiepusha na vitendo hivyo ili kujenga taswira nzuri.

Alisema katika kipindi cha uongozi wake, Mahakama iliweza kufanya mabadiliko makubwa ikiwemo kuanzishwa kwa miradi mingi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama, na kuanzishwa kwa mfumo wa kuratibu malalamiko.

Hafla ya kumuaga rasmi Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Majaji wastaafu, Mkurugenzi wa Mashitaka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu Kiongozi, Mawaziri Wakuu wastaafu  Mawaziri, Manaibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama. 

Mhe. Mohamed Chande Othman aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania tarehe 16 Agosti 2004 na tarehe 6 Februari 2008 alipandishwa hadi Mahakama ya Rufani kuwa Jaji wa Rufani. Aidha, mnamo tarehe 2 Disemba 2010 aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, nafasi aliyoishika hadi alipofikia umri wa kustaafu kwa mujibu wa Katiba mnamo tarehe 17 Januari 2017.

Comments (1)

  • Photo Loading... konalaimakulata@gmail.com

    jsds 2 toka jana saa tisa mpaka leo Mahakama ya Kisutu haipatikani kulikoni?

    16-07-2019

Leave a Comment