Post Details

MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA YA TANZANIA AWAONYA WAKANDARASI

Published By:innocent.kansha

Na Innocent Kansha – Mahakama.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Wakandarasi waliopewa kazi za ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Mahakama ya Tanzania kutimiza jukumu hilo kitaaluma kwa kuzingatia miiko ya mikataba yao waliosaini.

Akizungumza kwenye kikao kazi na Wakandarasi hao leo tarehe 24 Januari, 2022 katika Ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC)

Jijini Dodoma, Prof. Ole Gabriel alisema Mahakama itaendelea kuwafuatilia kwa jicho la karibu katika utendaji wao na haitovumilia mkandarasi atakae fanya kazi kwa mazoea.

“Nawaonya wakandarasi kutotoa rushwa wakati wa tenda na hata wakati wa kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Mahakama na kama kukitokea dalili ama kiashiria chochote uongozi ufahamishwe ili hatua stahiki zichukuliwemara moja”, alisisitiza Mtendaji huyo.

Prof. Ole Gabriel akawakumbusha Wakandarasi kufanya kazi kwa karibu na wasaidizi wake ili kutatua kero zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, mathalani masuala ya malipo halali ya wakandarasi.

Akiongelea suala la ujenzi, Prof. Ole Gabriel aliwataka wakandarasi kufanya kazi kwa muda uliopangwa kwa bidii na kujali utaalamu wa fani zao ili kazi zionyeshe umadhubuti na zizingatie ubora kwa ufanisi unaokubalika, kwani kilakitabu kina zama zake kwani Mahakama ya sasa ni ya watu waadilifu.

“Natamani kuona kila mkandarasi anakuja na hoja nzito zinazolenga kuboresha kazi, sitarajii kuona mkandarasi analeta maombi ya kuongeza muda wa kazi kwa hoja dhaifu, hatuta mvumilia na kila upande utimize wajibu wake kwa maslahi mapana ya kitasisi na ustawi wa Taifa”, aliongeza Mtendaji Mkuu huyo.

Aidha, Mtendaji Mkuu akakemea tabia ya baadhi ya wakandarasi kutokushirikiana kwa karibu na Watendaji wa Mahakama kwenye maeneoambayo wanatekeleza miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama, kwa kufanya hivyo changamoto zao hazitatatuliwa kwa haraka zaidi. 

“Kuna kasumba ya wakandarasi kutojalia taratibu sijui ni kwa makusudi ama kutofahamu taratibu

za kazi. Watendaji hao ndiyo wasaidizi wangu hivyo kabla hamjaanza kazi yawapasa kuripoti kwao ili shughuli zenu zifamike kuliko kuripoti kila kitu Makao Makuu”, alisema Mtendaji Mkuu. 

Akitolea ufafanuzi wa pesa za umma zinazotumika kwenye miradi ya ujenzi wamajengo ya Mahakama, Prof. Ole Gabriel akawakumbusha wakandarasi kuwa atakae chezea pesa za serikali hatoonewa haya, atachukuliwa hatua stahiki sio kwa kuvunjiwa mkataba bali kuchukuliwa hatua za kisheria kama itathibitika hivyo. Aliwataka kusimamia miradi yao kwa ukaribu na kwa kuzingatia thamani ya fedha za serikali.

Mtendaji Mkuu akawashauri wakandarasi wote kuajiri wataalamu wenye sifa katika kutekeleza majukumu yao ya kimikataba mfano; upande wa masoko, waasibu, mainjinia, washauri wa miradi wenye uzoefu wa kutosha ili kuimarisha kampuni zao na kuondoa kasumba ya kutolipa watumishi kwa wakati, hii itawajengea Imani kwa wateja wao.

“Natamani wote twende pamoja na tushirikiane kwa hali zote yaani Mahakama, Mkandarasi na Mkandarasi mshauri ili tuwe kitu kimoja na kutatua changamoto zetu kwa pamoja ili kukamilisha miradi hii ndani ya wakati unao kubalika”, aliongeza Mtendaji Mkuu.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama, akawakumbusha viongozi wa Mahakama wanaoratibu tenda kuangalia namna bora ya kuwapata wakandarasi wenye uwezo wa kutekeleza miradi ili imalizike kwa wakati na kwa haraka na kuangalia namna bora ya kuwatumia wakandarasi au wazabuni wenye gharama za chini ili kuendana na kasi ya ukamilishaji wa miradi kwa wakati.

Kwa upande wa matumizi ya TEHAMA, Prof. Ole Gabriel akawahimiza wazabuni au wakandarasi kuachana na matumizi ya kutuma nyaraka zao kwa njia ya nakala ngumu badala yake, watumie teknolojia ya habari na mawasiliano kama njia nyepesi ya kuwasilisha nyaraka zao kwani Mahakama imeshaondoka katika mfumo huo wa kutumiana nyaraka na sasa nyaraka zote zinawasilishwa kwa njia ya nakala laini kwa mfumo wa Ofisi mtandao ili kurahishisha mawasiliano.

 

Comments (0)

Leave a Comment