Post Details

JAJI MKUU AZINDUA MAJUZUU YA TAARIFA ZA SHERIA TANZANIA

Published By:LYDIA CHURI

Na Faustine Kapama – Mahakama, Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, leo tarehe 24 Januari, 2022 amezindua Majuzuu ya Taarifa za Sheria Tanzania kwa Mwaka 2007 hadi 2020 yanayojumuisha maamuzi ya Mahakama Kuu (Tanzania), Mahakama Kuu (Zanzibar) na Mahakama ya Rufani, tukio ambalo ni muhimu katika utoaji haki kwa wananchi.

Hatua hiyo ilienda sambamba na uzinduzi wa Faharisi (Index) ya Sheria Mama na Sheria ndogo za kuanzia Mwaka 1961-2020, vyote vikiwa katika mfumo wa nakala laini na nakala ngumu, jambo ambalo limelenga kuwasaidia maafisa wa Mahakama na Wadau kutumia vitabu vya taarifa hizo za sheria katika kusimamia utoaji haki.

Sanjali na tukio hilo muhimu, Mhe. Prof. Juma pia alizindua mfumo wa kielektroniki (e-Wakili Management System) mara baada ya kupokea maelezo mafupi kutoka kwa Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Shamillah Sarwatt, mfumo mpya ambao umeanzishwa mahususi kwa ajili ya kusajili, kutunza kumbukumbu na kuratibu leseni za Mawakili pamoja na taratibu zote zinazowahusu, mara baada ya mfumo uliokuwa unatumika hapo awali kuwa na changamoto kadhaa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mkuu alibainisha kuwa hiyo ni mara ya tatu machapisho hayo yameweza kutolewa na Mahakama ya Tanzania ambapo Chapisho la kwanza lilikuwa la mwaka 1980-1996 na Chapisho la pili lilikuwa la mwaka 1997-2006. Amesema kuwa uamuzi wa mashauri mengi katika Chapisho la tatu utaonekana kuwa ni wa Mahakama ya Rufani ikiwa ni muendelezo wa kutoa nakala zingine za uamuzi wa Mahakama Kuu (T) na Zanzibar katika kila mwaka husika kuwa na chapisho la pili (Volume II - Supplementary Volume).

“Hii inatokana na Mahakama ya Tanzania kupiga hatua kubwa ya upatikanaji wa uamuzi katika nakala laini kupitia Maktaba Mtandao na TanzLII, hivyo kuwezesha kuilisha Bodi ya Uhariri uamuzi katika mashauri mengi kwa mwezi ikiwa ni takribani ya uamuzi wa mashauri 600 hadi 700,” amesema.

Hata hivyo, Mhe. Prof. Juma alieleza kuwa machapisho ya mwanzo kabla ya uhuru yalianza Mwaka 1921 wakati Mahakama Kuu ya Tanganyika inaanza shughuli zake tarehe 3 Januari, 1921 ambapo uamuzi katika mashauri mengi katika kipindi hicho ulitolewa taarifa kati ya mwaka 1921 hadi 1952 ambayo iliitwa (Tanganyika Territory Law Reports), hii ikiwa ni chapisho la kwanza.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, mwaka 1953 hadi 1957 kulikuwa na chapisho la pili na baadae kuwa na chapisho la tatu mwaka 1958 hadi 1966. Amesema kuwa katika mwaka 1967 hadi mwaka 1972 machapisho ya makusanyiko ya uamuzi wa Mahakama Kuu ulitolewa (High Court Digests 1967-1972) na mwaka 1973 hadi mwaka 1979 Taarifa za Majuzuu zilitolewa (The Law Reports of Tanzania 1973-1979) kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mhe. Prof. Juma ameendelea kueleza kuwa baadae kuanzia mwaka 1980, Bodi ya Uhariri wa Majuzuu ya Taarifa za Sheria ilibadilika na kuwa na uenyekiti kupitia Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Barnabas Samatta na kuanzia kipindi hicho Mahakama ya Tanzania iliendelea na shughuli za uchapaji wa machapisho yote.

“Naomba nitoe pongezi na shukrani kwa Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa ufadhili kwa Mahakama ya Tanzania kwa kuwezesha na kufanikisha matoleo yote haya ya majuzuu (vitabu) vya miaka yote 14 na Faharisi  za Sheria Mama na Sheria ndogo za kuanzia Mwaka 1961-2020, vyote vikiwa katika mfumo wa nakala laini na nakala ngumu. Wao wamekuwa wadau wakubwa wa utoaji haki katika mashauri katika ngazi zote za Mahakama na wamekuwa wanasaidia Mahakama ya Tanzania katika mambo mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa utoaji haki,” amesema.

Jaji Mkuu amesema kuwa Mahakama itaendelea kuimarisha upatikanaji wa nakala za maamuzi na Taarifa za Majuzuu ya Sheria Tanzania kwa miaka ya nyuma kuanzia Mwaka 1980 hadi Mwaka 2006. Aidha ameomba Mahakama kupitia Idara ya Menejimenti ya Mashauri na Kitengo cha Maktaba kuendeleza utaratibu huo wa kuandaa Faharisi ya Sheria Mama na Sheria ndogo kwa Mwaka 2021 na kuendelea.

Kwa upande wake, Jaji kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe, Mustapher Siyani amesema kuwa Majuzuu ya Taarifa za Sheria ni nyenzo muhimu za kazi kwa kila mwana taaluma wa sheria ambapo kutoka katika taarifa hizo uamuzi wa mashauri mbalimbali yanayoakisi msimamo au mwelekeo wa sheria katika nchi yetu hupatikana.

Amesema kuwa taarifa hizo huwasaidia wananchi na Mawakili wanaofika mahakamani kila siku kutafuta haki kujua misimamo mbalimbali ya kisheria kupitia uamuzi ya Mahakama za juu. Aidha, amesema kuwa kwa Majaji na Mahakimu, Majuzuu hayo ya Taarifa za Sheria ni rejea ya kila siku kwani agalabu kwa maafisa hao wa Mahakama hufanya uamuzi bila kurejea uamuzi mwingine uliowahi kufanywa kwenye eneo husika, ikiwa upo.

“Umuhimu wa machapisho wa Majuzuu ya Taarifa za Sheria ulianza kuonekana tokea zama za ukoloni kabla ya uhuru wa nchi yetu ambapo kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 1961 kwa vipindi tofauti kulitolewa machapisho matatu yakifuatiwa na machapisho kadhaa yaliyorejewa kama High Court Digest, Law  Reports of Tanzania na baadaye Tanzania Law Reports,” amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Mratibu wa Bodi ya Uhariri wa Majuzuu ya Taarifa za Sheria Tanzania, Mhe Kifungo Mrisho amesema kuwa katika kupatikana kwa machapisho hayo kumekuwepo na mchakato mwingi, ikiwemo kuingia katika Mahakama Mtandao na masuala ya TEHAMA ili kuwezesha kupata uamuzi  wa mashauri mengi ya Mahakama Kuu (Tanzania), Mahakama Kuu (Zanzibar) na Mahakama ya Rufani, hatua ambayo imewezesha taarifa zote kuanzia mwaka 2007 hadi 2020, takribani miaka 14 kuweza kupatikana.

Alibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa iliyofanywa na Mwenyekiti wa Bodi ya Uhariri wa Majuzuu ya Taarifa za Sheria, Mhe. Jacobs Mwambegele, Jaji wa Mahakama ya Rufani, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na timu yote ya wajumbe iliyowezesha taarifa hizi kupatikana, bila kusahau ushirikiano walioupata kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel na kitendo cha uboreshaji wa huduma mbalimbali cha Mahakama ya Tanzania.

Comments (0)

Leave a Comment