Post Details

MAHAKIMU WAKAZI WAFAWIDHI WAPYA WAPATIWA NYENZO ZA KAZI

Published By:LYDIA CHURI

Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 13 Januari 2022 amewakabidhi nyenzo za kazi jumla ya Mahakimu Wakazi Wafawidhi wapya 10 baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.

Akizungumza na Mahakimu hao baada ya kuwaapisha katika Ukumbi wa Mahakama ya Rufani (T) jijini Dar es Salaam, Mhe. Prof. Juma aliwapongeza kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo huku akiwaasa kuwa wanyenyekevu katika utendaji wao wa kazi.

“Unapokuwa kiongozi katika chombo cha utoaji haki unatakiwa kuwa mnyenyekevu kwa kila mtu unayemhudumia kwakuwa sio wananchi wote wanaofahamu haki zao, hivyo inabidi kuwaelimisha,” alisema Jaji Mkuu.

Aidha, Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kwa kuwataka Mahakimu hao kuwa na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuendana na kasi ya matumizi ya TEHAMA ambayo Mahakama inatekeleza katika kufanikisha azma ya kuwa na Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’.

Mhe. Prof. Juma alisema, “Nafasi yenu kama viongozi mnatakiwa kuwa na ufanisi ili kuendana na zama za mapinduzi ya nne ya viwanda, muwe karibu sana na Maafisa TEHAMA mnapokwama ili kuwawezesha kwenda sambamba na kasi ya utandawazi.”

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha Maafisa hao wa Mahakama kuhusu matumizi ya adhabu mbadala ili kupunguza mlundikano wa wafungwa gerezani.

Naye, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani aliwataka Mahakimu Wafawidhi hao kutatua kero na malalamiko mbalimbali yanayochafua taswira ya Mahakama, ikiwemo mlundikano wa mashauri ya muda mrefu, lugha mbaya, kutowajibika kwa baadhi ya Watumishi wa Mahakama, upatikanaji wa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri pamoja na rushwa.

“Nyenzo za kazi mlizokabidhiwa leo zinawatofautisha na Mahakimu wengine, hivyo nendeni mkatatue kero na malalamiko ya wananchi, kero hizi zitawasilishwa kwa njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii ‘facebook’, ‘instagram’, ‘twitter’ na kadhalika na hata kama malalamiko yanayotolewa hayatahusu kituo chako, saidia katika kutatua kwa kuwa sote tunajenga nyumba moja,” alisema Mhe. Siyani.

Jaji Kiongozi aliongeza kwa kutoa rai kwa Maafisa hao wa Mahakama kuwa waadilifu na kuwakumbusha kuwa na ushirikiano na Wadau wa Mahakama pamoja na Viongozi wa Serikali ili kupiga hatua katika uboreshaji wa huduma za Mahakama na Taifa kwa ujumla.

Mahakimu Wakazi Wafawidhi waliokabidhiwa nyenzo za kazi ni wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Musoma-Mara, Moshi-Kilimanjaro, Sumbawanga-Rukwa, Katavi, Morogoro, Kigoma, Singida, Arusha na Tanga.

Baada ya hafla hiyo, Jaji Kiongozi aliwakabidhi Mahakimu Wakazi Wafawidhi hao kila mmoja kadi maalumu kama ishara ya kuwapongeza kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kukabidhiwa nyenzo zitakazowaongoza katika utendaji wao wa kazi.

Comments (0)

Leave a Comment