Post Details

WASAIDIZI WA SHERIA WA MAJAJI WAAPISHWA KUWA MAHAKIMU

Published By:JoT Admin

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo amewaapisha Wasaidizi wa Sheria wa Majaji kuwa Mahakimu Wakazi na kuwataka kutoa maamuzi yatakayoielimisha jamii.

Akizungumza baada ya kuwaapisha Mahakimu Wakazi 53 Juni 18 mwaka huu  Jaji Mkuu pia amewataka Mahakimu hao kuandika hukumu zinazoeleweka, zinazo someka, zenye lugha nyepesi, pamoja na kutoa hukumu hizo kwa wakati.

“Uamuzi wowote mtakaoutoa kuanzia siku ya kwanza Mahakamani utagusa Uhai, Mali na Hali ya wanadamu wengine, hivyo kosa lolote la kimaamuzi mtakalotoa litakuwa na gharama pamoja na gharama ya muda kwa nchi, kwa watu, na kwa familia kwa ujumla”, alisema.

Aidha, Jaji Mkuu amewataka Mahakimu wapya kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, umakini na unyenyekevu kwa kuwa kazi hiyo inahitaji uangalizi wa hali ya juu. Aliwataka Mahakimu hao pia kuwasaidia watanzania kuhusu masuala ya kisheria hususan wanawake na watoto.

Akizungumzia vitendo vya rushwa Mahakamani, Prof. Juma alisema bado Mahakama haizungumziwi vizuri katika suala hilo hivyo aliwataka Mahakimu hao kutoogopa kulizungumzia tatizo hilo, na kupanga mikakati ya kukabiliana nayo.

 “Rushwa ni kitu kinachojificha, pangeni mikakati ya kupambana nayo. Someni ripoti ya Jaji Warioba ya mwaka 1996 ili muelewe ni wapi rushwa imejificha”, alisema.

Aidha, Jaji Mkuu alivitaja viashiria vya rushwa ndani ya Mahakama kuwa ni katika maeneo ya kufungua mashauri, kupanga tarehe za mashauri, utafutahji wa majalada, na utoaji wa nakala za hukumu. Aliwataka Mahakimu hao kuhakikisha wanatoa nakala za hukumu kwa wakati ili wasihusishwe na dhana ya rushwa.

Alisema Mahakimu ni nyara ya Mahakama hivyo hawana budi kujenga taswira nzuri ya Mahakama kwani kwa kutofanya hivyo nchi nzima itachafuka. Aliongeza kuwa ni muhimu kwa Mahakimu kuheshimiana na kuheshimu kada nyingine kwa kuwa hakuna kada muhimu zaidi ya nyingine.

“Sauti yako ni sauti ya umma lazima itoke kwa juu, usimfokee mtu Mahakamani,” alisisitiza.

Nao Mahakimu walioapishwa kwa ujumla wao wameonyesha kufurahishwa na hatua hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa uadilifu na kuahidi kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kabla ya kuapishwa rasmi, Mahakimu hawa walikuwa wakihudumu katika ngazi ya Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu kama Wasaidizi wa Sheria wa Majaji kwa takribani miaka tisa (9).

Mahakimu hawa ambao tayari wameshapangwa katika vituo mbalimbali wataongeza nguvu ya kupunguza mlundikano wa mashauri.

Comments (1)

  • Photo Loading... Shotoli

    Nikweli kabisa alichosema Jaji Mkuu,sisi wananchi tunapotafta haki mahakamani hasa wananchi tulio nakipato cha chini tunapata taabu saana nawakati mwingine kulazimika kutoa rushwa ili kesi yako isajiriwe au isikilizwe , bila hivyo ujue kusajiriwa kesi itakuwa Shida nahata kusikilizwa itakuwa Shida, mfano Mimi nimemshinda kesi Mzungu tajiri MAHAKAMA Kuu ya MWANZA tangu tar.28/12/2018 lakini maombi yangu yakukaza hukumu yanapigwa tar. Tangia mwezi watatu mpaka Sasa, naanaefanya haya mambo nimsajiri na makarani wake christofa na baadae Edsoni aliekuja kuachiwa office na christofa, nimelalamika kwa Msajiri mpaka nimechoka ukizingatia natoka songea kwenda MWANZA ,ukitaka kumuona Jaji mfawidhi hawaniruhusu namzungu ameanza kufunga kampuni baada yakazi aliyokuwa anaifanya kuisha hii inaonyesha Msajiri na makarani wamepewa rushwa ili Mzungu aondoke nibaki naushindi wa makaratasi, ninaomba Jaji Mkuu unisaidie. Mimi Daniel shotoli 0767139634 lakini pia mbadirishe taratibu zakuwaona majaji wafawidhi badara yakupitia kwa MTU huyohuyo unaemlalamikia niwadhi kuwa hatakuruhusu kwenda kumshitaki. Nahitaji msaada zaidi kwani km nibarua napo nimeandika bila msaada nikijua zinapitia kwako kabla yakumfikia boss.

    07-07-2019

Leave a Comment