Post Details

RAIS WA TLS AKUTANA NA MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA YA TANZANIA

Published By:LYDIA CHURI

 Na Innocent Kansha - Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 22, Desemba 2021, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Prof. Edward Hosea ambapo wamekubaliana kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu kwa manufaa ya Taasisi hizo.

Akizungumza na Prof. Hosea ofisini kwake Jijini Dar es salaam, Mtendaji Mkuu wa Mahakama amemhakikishia kuendeleza ushirikiano uliopo miongoni mwa Taasisi hizo ili kuondoa kero na migogoro isiyo ya lazima kwa maslahi ya Taifa.

“Tutaendelea kubadilishana uzoefu mara kwa mara tutakapopata nafasi ya kufanya hivyo ili kutatua changamoto zitakazojitokeza kwenye utendaji kazi ikiwemo kupeana taarifa, hasa za matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuboresha utendaji na mawasiliano”, alisema Prof. Ole Gabriel.

Kwa upande wake Rais wa TLS alimshukuru Prof. Ole Gabriel na kumhakikishia kuendeleza ushirikiano uliopo baina yao ili kuhakikisha wananchi wanatatuliwa kero zao kupitia Mhimili wa Mahakama.

Aidha, Prof. Hosea aliupongeza uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa jitihada inazozifanya kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanafanikisha shughuli za utoaji haki kwa wakati kwa wananchi.

Comments (0)

Leave a Comment