Post Details

JAJI MKUU AWAONYA MAWAKILI

Published By:LYDIA CHURI

Na Faustine Kapama na Innocent Kansha - Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaonya Mawakili kote nchini kuacha kutumia majina ya Majaji na Mahakimu ili kujipatia kipato kikubwa kutoka kwa wateja wao wanapokuwa wanawawakilisha mahakamani.

Akizungumza katika sherehe ya kuwapokea na kuwakubali Mawakili wapya 313 katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Desemba, 2021, Mhe. Prof. Juma amebainisha kuwa wamekuwa wakipokea malalamiko kuwa Mawakili wanapotoza malipo kutoka kwa wateja wao hujumuisha na mgao wa Majaji na Mahakimu wanaosikiliza mashauri mbalimbali kutoka kwa wateja.

“Tumepokea malalamiko kuwa baadhi ya Mawakili huwatoza wateja wao pesa zaidi kwa madai kuwa sehemu yake hupelekwa kama mgao kwa Jaji au Hakimu. Sisi hatuchukui mgao hata siku moja. Majaji na Mahakimu hawachukui mgao hata siku moja. Lakini wapo Mawakili ambao wanataka fedha zaidi ya sheria inavyotamka na kusema kiasi hiki ni kwa ajili ya kamati yake ya ufundi ili kupelekwa kwa Jaji au Hakimu. Napenda kuwaambia wananchi, ukikutana na Wakili wa aina hiyo tuletee, tutamfuta katika orodha ya Mawakili dakika hiyo hiyo. Nawaomba sana Majaji tutumie mamlaka tuliyonayo ili kurudisha nidhamu,” Jaji Mkuu ameonya.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, rushwa na utovu wa maadili ni changamoto ambayo inachafua imani, hadhi na taswira ya mfumo mzima wa utoaji wa huduma za uwakili ambazo zitawanyima fursa ya ushindani sio tu katika eneo huru la biashara la Afrika, bali hata katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro.

“Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda haina nafasi kwa Mawakili wasio na maadili na pia wale wanaotoa huduma zilizo chini ya viwango. Katika zama hizi za utandawazi na teknolojia ya habari, unahitaji Wakili mmoja tu asiye na maadili au asiye na viwango, kuweza kuchafua sifa za Mawakili wote wa Tanzania,” amesema.

Mhe. Prof. Juma ameeleza pia kuwa baadhi ya Mawakili wanashindwa kutambua kuwa wao ni maafisa wa Mahakama na ni nguzo muhimu ya utetezi wa uhuru wa Mahakama na kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama, lakini kwa bahati mbaya, badala ya kukosoa uamuzi wa Mahakama kwa haki, wanajificha nyuma ya majina ya bandia katika mitandao ya kijamiii na kupotosha uamuzi huo.

“Wengine wanatumia mitandao ya kijamii kuwashambulia Majaji na Mahakimu kwa jina na kwa picha kwa lengo la kuwafedhehesha na kuwadhalilisha. Hii haikubaliki. Huyo Wakili hastahili kabisa kuwa kwenye orodha ya Mawakili. Najua Mawakili kama hao hukimbilia kusema ni haki za binadamu, lakini haki za binadamu zinapande zote, zinaheshimu uhuru wa Mahakama, zinaheshimu utawala wa sheria na kufuata taratibu. Unapochafua taswira ya Mahakama, kumbuka unachafua taaluma yako ya uwakili, hivyo nawaomba sana msiwe Mawakili kama hao. Bahati nzuri wote tunawafahamu, siku zao zimekwisha,” aliwaeleza Mawakili hao wapya.

Jaji Mkuu alieleza kuwa asilimia kubwa ya Mawakili ambao hulalamikiwa mbele ya Kamati ya Maadili ya Mawakili wanakuwa hawana mikataba ya kazi na wateja wao. Alieleza kuwa athari za kutoandikishiana mikataba hujitokeza malalamiko yanapofikishwa mbele ya Kamati ya Mawakili na inakuwa vigumu kwa mteja kuthibitisha madai yake.

“Ni muhimu kwa kila Wakili kuwa na mkataba na kila mteja anayemwakilisha mahakamani. Mawakili wengi wanapokea fedha kutoka kwa wateja wao lakini hawatoi risiti. Changamoto hii hujitokeza wakati wateja wakifikisha malalamiko katika Kamati ya Mawakili. Hofu tuliyonayo sasa hivi ni kwa kiasi gani Mawakili watakapoanza kutoa huduma Mahakama za Mwanzo watapeleka changamoto ambazo hivi sasa Mawakili wanalalamikiwa,” alibainisha.

Akizungumza katika sherehe hizo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi aliwakumbusha Mawakili hao wapya mambo mbalimbali ambayo wanapaswa kuyazingatia wanapotekeleza majukumu yao kwa Mahakama, kwa mteja, kwa umma, kwa Mawakili wengine na taaluma yenyewe ya sheria ili kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi, ikiwemo kuzingatia maadili ya kazi zao kwa kuwa uwakili ni taaluma adhimu.

Amesema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 66 cha sheria ya Mawakili, Sura ya 341, Mawakili kama maafisa wa Mahakama wana wajibu wa kuisaidia Mahakama kufikia uamuzi wa haki na kwa wakati ambapo Kanuni ya 92 (1) ya Maadili ya Mawakili inawataka kuheshimu Mahakama pamoja na uamuzi unaotolewa hata kama hawajaridhika nao, yapaswa kuchukua fursa ya nafuu zilizowekwa na sheria katika kuhoji uamuzi huo.

“Aidha, Kanuni ya 92 (2) ya Maadili ya Mawakili inakataza Mawakili kuhujumu wajibu wa Mahakama wa utoaji haki katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za uongo au kupotosha uamuzi wa Mahakama au taratibu za uendeshaji wa mashauri kwa njia yoyote,” alisema Dkt. Feleshi.

Akizungumzia mabadiliko ya sheria yaliyowaruhusu kuwakilisha wateja katika Mahakama za Mwanzo, Mhe. Dkt Feleshi aliwakumbusha Mawakili hao kuwa Mahakama hizo zitaendelea kutumia taratibu kama zinavyoainishwa katika Sheria na Kanuni zinazoongoza mienendo ya mashauri, hivyo wanapaswa kuzifuata.

“Naomba kuwaasa Mawakili wote mtakaowawakilisha wateja wenu katika Mahakama za Mwanzo kwamba, kuruhusiwa kwenu katika Mahakama hizo iwe chachu ya kuongeza kasi na ufanisi katika upatikanaji wa haki kwa wakati. Msiende kuibua masuala ya kiufundi yatakayosababisha ucheleweshaji wa mashauri kwa makusudi au dhamira ovu katika Mahakama hizo isiyozingatia maslahi ya haki,” alionya Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mhe. Prof. Edward Hosea, aliwaeleza Mawakili hao kuwa tasnia ya uwakili ni tasnia ya kipekee inayohitaji uadilifu mkubwa, kusoma, kujituma, kushirikiana na Mawakili wengine katika kuboresha tasnia hiyo na kufanya tafiti ili kuweza kufikia malengo yao na kutoa huduma bora kwa jamii.

“Wakati mnasherehekea mafanikio yenu ya kufikia hatua hii kubwa katika tasnia hii, ni muhimu kutambua kuwa, ukiwa Wakili, Sheria imekupa wajibu mkubwa kwa mteja, Mahakama, jamii na Mawakili wenzako. Ni nyema kutambua wajibu wako huu na kuutimiza,” alisema Rais huyo.

Prof. Hosea amesema kuwa katika kutekeleza wajibu wao Mawakili hao wanatakiwa kuzingatia viwango vya utendaji wa sheria na maadili yake ipasavyo kama  inavyoelezwa katika Sheria ya Mawakili Sura. 341 na Kanuni ya Mawakili, 2018.

Comments (0)

Leave a Comment