Post Details

MAJAJI WASTAAFU WAWANOA NAIBU WASAJILI NA WATENDAJI WA MAHAKAMA

Published By:LYDIA CHURI

Na Faustine Kapama na Lydia Churi, Mahakama

Mafunzo elekezi yanayotolewa kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yameendelea leo tarehe 30 Novemba, 2021 ambapo Jaji Mkuu mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman na Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. January Msoffe wamewakumbusha viongozi hao mambo muhimu ambayo wanapaswa kuzingatia wanapotekeleza majukumu yao ya kimahakama.

Aliyekuwa wa kwanza kuwanoa viongozi hao alikuwa Mhe. Chande, ambaye aliwapitisha katika Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama (the Judiciary Administration Act) ya mwaka 2011, ambayo imekuwa nguzo muhimu katika kuwawezesha viongozi na watendaji mbalimbali wa Mahakama katika kutimiza wajibu wao bila kutegemea Mhimili mwingine wa dola.

Jaji Mkuu huyo mstaafu alifafanua madhumuni makubwa ya kuanzishwa kwa sheria hiyo ikiwemo kuimarisha uhuru wa Mahakama, kuongeza uhuru wa kitaasisi na watumishi wa Mahakama katika kutekeleza majukumu yao, kuimarisha utawala wa haki na kurahisisha utawala wa Mahakama.

Kwa mujibu wa Mhe. Chande, kutungwa kwa sheria hiyo pia kuliondoa ubishi wa madaraka ya Jaji Mkuu ambapo katika kutekeleza majukumu yake, sheria hiyo inampa mamlaka ya kudai matokeo ya utendaji kazi kwa kila kiongozi, wakiwemo Majaji na Mahakimu, mfano kujua ni mashauri mangapi yaliyosikilizwa katika kipindi kilichowekwa na kupima utekelezaji wa shughuli za kimahakama.

Alibaisha pia kuwa kutokana na sheria hiyo, shughuli zote za kiutendaji, ikiwemo kuajiri watendaji na kuchukua hatua za kinidhamu hufanywa na Mahakama yenyewe badala ya shughuli hizo kufanywa na taasisi nyingine ndani ya Serikali. Pia sheria hiyo iliwezesha kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa Mahakama, hatua ambayo imesaidia kuongeza ufanisi katika kutekeleza shughuli mbalimbali katika mfumo mzima wa utoaji haki.

Hata hivyo, baadhi ya wachangiaji wa mada hiyo, Bw. Sostenese Mayoka na Bw. Geofrey Mashafi, ambao ni Watendaji wa Mahakama na Mhe. Judith Kamala, Naibu Msajili, walielezea namna ambavyo viongozi wa Mahakama wana kazi ya kufanya katika kuuelimisha umma juu na mawazo hasi waliyonayo juu ya Mahakama kwa ujumla.

Kwa mujibu wa wachangiaji hao, kumekuwepo na mawazo potofu kwamba mwananchi wa kawaida hawezi kupata haki kirahisi kama akipeleka shauri lake mahakamani, jambo linalopelekea wananchi kukimbilia kwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wakiamini haki inaweza kupatikana kwa viongozi hao.

Mhe Kamala alieleza kuwa mawazo kama hayo hayapaswi kupewa nafasi kwa kuzingatia maendeleo makubwa ambayo yamefanywa na Mahakama katika kuweka mazingira mazuri ya utoaji haki kwa wananchi, hivyo akashauri utoaji wa elimu ya kutosha utakuwa ndiyo njia muafaka ili watanzania waelewe mambo mazuri yanayoendelea kufanyika mahakamani.

Halikadhalika, washiriki katika mafunzo hayo waliona sheria inayowapa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa mamlaka ya kuendelea kuwa wenyeviti wa kamati za maadili kwa Mahakimu kuwa ina mapungufu kwa vile inaweza kuathiri uhuru wa Mahakama.

Kwa upande wake, Mhe. Msoffe, ambaye aliwasilisha mada juu ya Maadili ya Watumishi wa Umma na Maadili ya Kimahakama alichukua muda mrefu kuwaeleza washiriki wa mafunzo hayo namna ambavyo wanapaswa kuwa na tabia njema na kuwa mfano kwa watumishi wengine waliochini yao na wananchi kwa ujumla.

Aliwakumbusha kuwa wakati wanatekeleza majukumu yao hawana budi kufanya kazi kwa bidii, kujizuia kuwa na tamaa, kujiheshimu, kufanya kazi bila upendeleo, kuepuka kupokea vijizawadi, kutoa na kupokea rushwa, kuepuka kutumia madaraka waliyonayo vibaya na kutotumia mali ya umma kwa maslahi binafsi.

Jaji huyo mstaafu pia aliwakumbusha Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama kuhusu matumizi sahihi ya taarifa za umma, kuongoza kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, taratibu na mazoea na kujiepusha kufanya mambo ya upendeleo na ubaguzi na kutotoa siri za serikali au taarifa muhimu kwa watu ambao hawahusiki.

Baadaye jioni, mwezeshaji mwingine, Bw. Malimo Manyambura, ambaye ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Tanzania aliwashirikisha Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama hao kwenye suala zima la utunzaji wa kumbukumbu mbalimbali mahakamani.

Comments (0)

Leave a Comment