Post Details

NINYI NI MOYO, INJINI YA MAHAKAMA: JAJI KIONGOZI AWAAMBIA WASAJILI WAPYA

Published By:LYDIA CHURI

Na Faustine Kapama na Lydia Churi, Mahakama

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani leo tarehe 25 Novemba, 2021 amewaapisha Naibu Wasajili 27 na kuwataka kutimiza majukumu yao kikamilifu ili kuchochea maendeleo ya Mahakama na utoaji wa haki kwa wananchi kwa wakati.

Akizungumza baada ya uapisho huo uliofanyika katika ukumbi namba moja wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, Mhe. Siyani aliwafananisha wateule hao kama injini au moyo ambayo ni muhimu katika kusukuma maendeleo yanatotakiwa kufanyika mahakamani.

“Mahakama itawategemea sana ninyi, kama Naibu Wasajili nitawafananisha na vitu viwili. Kama tunazungumzia chombo cha usafiri, ninyi ni injini au mashine inayowezesha chombo kile kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, na kama nitawafananisha na viumbe hai ninyi ni moyo,” aliwaambia wateule hao.

Kwa mujibu wa Jaji Kiongozi, hakuna kati ya chombo cha usafiri au kiumbe hai ambacho kinachoweza kwenda sehemu moja kutoka sehemu nyingine kama injini au moyo haufanyi kazi. Hivyo, aliwataka viongozi hao kutimiza majukumu yao kikamilifu, kuwa  mfano wa uwajibikaji na kudhihirisha uwezo wao kwa kufanya kazi kwa bidii.

“Onyesheni kwamba baada ya miaka mingi  ambayo mmeitumikia Mahakama ya Tanzania sasa ni wakati mwafaka kwenu wa kuteuliwa kuwa Naibu Msajili na waliofanya uteuzi huo hawakukosea,” Mhe. Siyani alisema.

Jaji Kiongozi aliwahimiza Naibu Wasajili hao kwenda kusimamia uboreshaji wa huduma za Mahakama kwa vile wote wanafahamu welekeo ambao Mahakama ya Tanzania inakwenda kuwa Mahakama Mtandao. “Kuweni madereva wa safari hiyo ya uboreshaji kuelekea Mahakama Mtandao. Mnajua miaka mitatu tangu sasa itakapofika 2025 tunapaswa kuondokana na matumizi ya karatasi. Teknolojia inapaswa kuwa ndiyo msingi wetu wa kufanya kazi na watakaosimamia au kuwa madereva wetu ni ninyi,” aliwaambia wateule hao.

Aidha, Jaji Kiongozi aliwakumbusha kuwa wanakwenda katika masjala mbalimbali, ambazo zina mashauri na baadhi ya masjala hizo zina mlundikano, hivyo wanawajibika kwa kushirikiana na Majaji na Mahakimu kuhakikisha Mahakama inaondokana na mlundikao au mashauri yanayokaa muda mrefu mahakamani.

“Hapa kuna dhana kwamba Msajili hana nafasi ya kusaidia kuondokana na mlundikano. Ukweli ni kwamba mipango yote itakayowezesha masjala moja kuondokana na mlundikano inaanzia kwa Naibu Msajili aliyepo kwenye masjala hiyo. Kwa hiyo, kama kutakuwa na Kanda au Mahakama ya chini ina mlundikano wa mashauri, mtu wa kwanza anayepaswa kutazamwa ni Naibu Msajili kwa sababu yeye ndiye msimamizi,” alisema.

Aliwakumbusha pia kurejea nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Jaji Mkuu na ofisi ya Jaji Kiongozi ambazo zinatoa maelekezo mbalimbali ya namna wanavyotakiwa kutekeleza majukumu yao, hivyo aliwaonya kutokusherekea uteuzi walioupata kwa sababu kazi wanayokwenda kuifanya siyo nyepesi, hivyo wanapaswa kujiandaa kuchapa kazi.

Hata hivyo, Mhe. Siyani aliwapongeza wote kwa uteuzi walioupata ambao umefuata na kuzingatia utendaji wao wa kazi na kwamba wote walioteuliwa wanalistahili na hapakuwa na upendeleo wowote. Aliwaambia kuwa wamepewa majukumu makubwa, hivyo Mahakama inategemea vingi kutoka kwao.

“Mmekula kiapo cha kuwa Naibu Msajili na  wote mlipitia usaili ambao unahusu, yanayotarajiwa kutoka kwenu kama Naibu Wasajili. Kwa kufaulu kwenu usaili ule, dhana iliyopo ni kwamba tayari wengi wenu mnafahamu majukumu yanayowakabili mbele yenu. Jukumu kubwa ni usimamisi wa Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na Mahakama zote. Nendeni mkasome majukumu ya Naibu Msajili ambayo yameaanishwa vizuri, myaelewe na kisha mkafanye kazi,” aliwaasa viongozi hao wa Mahakama.

Akizungumza katika hafla hiyo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alisema kuwa kupatikana kwa Manaibu Wasajili hao kulitokana na mchakato mrefu ambao ulihusisha kwa mara ya kwanza usaili na wote walioapishwa waliweza kupita vikwazo vyote, hivyo wanastahili kushika wadhifa huo.

“Ninyi ni miongoni mwa wengi ambao, kwa namna moja au nyingine, walitamani kuwepo hapa leo. Lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kuwa miongoni mwa wateule. Labda niseme kwamba kwa wale ambao walitamani kuwepo ni wakati mzuri wa kutafakari na kuweza kujipanga upya na kuchapa kazi kwa bidii,” alisema.

Hafla ya uapisho huo ilihudhuriwa pia na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma, Majaji mbalimbali wa Mahakama Kuu ya Tanzania, akiwemo Jaji Mfawidhi Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kelvin Mhina, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi , Wasajili na Watendaji mbalimbali kutoka Mahakama Kuu.

Comments (0)

Leave a Comment