Post Details

JAJI MKUU AWAAPISHA MAHAKIMU WAKAZI WAPYA SITA

Published By:Mary C. Gwera

 Na Faustine Kapama, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 23 Novemba, 2021 amewaapisha Mahakimu Wakazi wapya sita  na kuwataka kutoa picha halisi ya ubora wa Mahakama kwa kuishi viapo vyao katika kutekeleza kikamilifu jukumu la utoaji haki kwa wananchi.

Akizungumza katika hafla fupi ya uapisho huo iliyofanyika ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam, Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha Mahakimu hao kuwa wameapa kwa kutumia Katiba na Kitabu Kitakatifu na kuahidi kwamba watalinda Katiba, kutetea sheria na kutoa haki bila upendeleo wa aina yoyote.

“Hivyo ahadi hii inatakiwa iwe sehemu ya maisha yenu mtakayoishi kama Mahakimu na katika shughuli nyingine yoyote mtakayoifanya. Napenda kuwakumbusha kuwa kiapo chenu kisiishie hapa. Ikiwezekana siku zote jitengenezeeni nakala iwaongoze siku zote kwa sababu inatoa muhtasari wa kile ambacho kinategemewa kutoka kwenu,” Jaji Mkuu aliwaasa Mahakimu hao.

Alibainisha pia kuwa hapa Tanzania, asilimia 70 ya wanaotafuta haki wanaipata katika Mahakama za Mwanzo, hivyo Mahakimu hao wanabeba mzigo mkubwa wa utoaji haki kwa sababu wananchi wengi kituo chao cha kwanza cha kutafuta haki ni Mahakama za Mwanzo na wengi huwa hawapati nafasi ya kuonana na Majaji.

“Kwa hiyo, picha yao ya Mahakama ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo. Nawaomba mtoe picha halisi ya ubora wa Mahakama. Sisi sote tutachafuka kama mkitoa picha ambayo sio halisi ya Mahakama. Nyie ndiyo picha kwa mwananchi wa kawaida na sehemu yoyote mtakayokwenda mtaishi pamoja na jamii,” alisema.

Jaji Mkuu alikumbushia jambo jingine kuhusu ukubwa wa mamlaka waliyonayo Mahakimu kwa kuangalia sheria ambazo huwa wanazitekeleza na kwamba amri yoyote wanayoweza kutoa hugusa haki za wananchi, ikiwemo haki za binadamu za kila siku, haki za mali au haki za uhuru wao binafsi, hivyo, aliwataka kutokuchelewesha maamuzi yao yanayogusa haki hizo.

“Kwa mfano, endapo utafuata sheria kwa umakini na ukatoa haki kwa umakini na wahusika wakaridhika na kutokukata rufaa, ina maana shauri husika litaisha na haki itapatikana ndani ya muda mfupi sana. Lakini kama utatoa uamuzi ambao sio makini na ikapatikana rufaa, maana yake upatikanaji wa haki utachelewa. Kwa hiyo ukiwa makini haki itapatikana kwa haraka zaidi na usipokuwa makini yule mwananchi anayetafuta haki hiyo atasubiri mpaka Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi wake,” Mhe. Prof. Juma alisema.

Aidha, Jaji Mkuu aliwataka Mahakimu hao kuendelea kujisomea na kufuatilia mabadiliko ya sheria kadri yanavyotokea kwa sababu kila siku sheria inabadilika. Alitoa mfano wa Bunge lijalo ambapo kutakuwa na mabadiliko ya sheria kadhaa na baadhi ya mabadiliko hayo yatagusa utoaji haki mahakamani. “Tunatarajia mtafuatilia hayo mabadiliko na yakipishwa na Bunge lazima muende na hayo mabadiliko,” aliwaambia Mahakimu hao.

Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani aliwasihi Mahakimu hao wapya kuzingatia uadilifu, juhudi na kuzingatia sheria, miongozo, taratibu na kanuni mbalimbali zinazotawala nchi yetu. “Bahati nzuri ninyi wote mmekuwa watumishi wa Mahakama na mnafahamu yanayoendelea katika Mahakama ya Tazania hivi sasa. Hivyo ni matumaini yetu mtaenda kufanya kazi inayotakiwa. Hivyo, nendeni mkafanye kazi,” alisema.

Mahakimu hao wapya walioapishwa leo ni Mhe. Raymond Kweka aliyekuwa Msaidizi wa Kumbukumbu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. John Musiime ambaye alikuwa Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, Mhe. Clifford Masinde, Msaidizi wa Kumbukumbu Mwandamizi Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Haudeface Mpanju, Msaidizi wa Kumbukumbu katika Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, Martha Mabagala, aliyekuwa Msaidizi wa Ofisi Mahakama ya Mwanzo Kimara na Mhe. Protas Honono, aliyekuwa Msaidizi wa Hesabu Mahakama ya Wilaya Singida.

Viongozi wengine wa Mahakama waliohudhuria hafla hiyo ya uapisho ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kelvin Mhina, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania anayeshughulikia Mahakama za Mwanzo, Bw. Humphfrey Paya na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Bahati Chitepo.

Comments (0)

Leave a Comment