Post Details

MAHAKAMA KUIMARISHA MAADILI KWA WATUMISHI WAKE

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa Mahakama ya Tanzania imeonyesha nia ya dhati katika kupiga vita vitendo vya rushwa, ukosefu wa maadili na matumizi ya lugha zisizozingatia staha. 

Akifungua warsha ya kujadili rasimu ya miongozo ya mafunzo na uendeshaji wa kamati za Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania iliyofanyika leo Kisutu jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu amesema Mahakama imelipa kipaumbele suala la kuimarisha maadili ya watumishi wake kwenye ngazi zote kama sehemu ya uwajibikaji kwa kuwa uhuru wa Mahakama unaimarika kunapokuwa na uwajibikaji na maadili.

Jaji Mkuu amesema lengo la maboresho ya Mahakama ya Tanzania halitafanikiwa endapo suala la maadili halitapewa uzito unaostahili kwani rushwa na utovu wa Maadili havina nafasi katika Mahakama inayofuata misingi ya maboresho.

Aidha, Jaji Mkuu pia aliwataka wananchi kutoa taarifa za kweli za matukio ya ukiukwaji wa maadili kwenye kamati za Maadili za Mahakama, “Jitihada dhidi ya vitendo hivi zitafanikiwa tu endapo wananchi watawasilisha taarifa za kweli za matukio ya ukiukwaji wa Maadili mbele ya Kamati za Maadili”, alisema Jaji Mkuu.

Amezitaka kamati za maadili kufanya kazi zake kwa kufuata taratibu na miongozo iliyowekwa.

Alisema dhamira ya Mahakama katika kupambana na ukiukwaji wa maadili na vitendo vya rushwa pia inaonekana wazi kwenye mikakati iliyojiwekea ikiwemo kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kupitia njia mbalimbali hasa  kusambaza mabango katika majengo ya mahakama nchi nzima.

Mabango yaliyosambazwa nchi nzima yana ujumbe maalum unaowataka  wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili.  “Kulalamika peke yake bila kutoa taarifa hakutoshi katika vita dhidi ya vitendo viovu”, alisema.

Jaji Mkuu aliwataka wadau wa Mahakama ya Tanzania na Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaohudhuria mkutano huo kupitia rasimu za miongozo na kutoa maoni yenye lengo la kuiboresha ili iweze kupunguza ama kumaliza  mapungufu yaliyopo.

Alisema Mkutano wa wadau ni muendelezo wa kuhakikisha kuwa Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011 ambayo imeleta mabadiliko makubwa ndani ya Mahakama inafanya kazi kwa manufaa ya kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama za Tanzania.

Alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama ndiyo mamlaka ya nidhamu kwa watumishi wa Mahakama wakiwemo Mahakimu katika ngazi zote Majaji, Wasajili na watumishi wengine wa Mahakama.

Jukumu kubwa la Kamati za Maadili ni kuchunguza malalamiko yanayofikishwa mbele ya Kamati husika, juu ya ukiukaji wa maadili dhidi ya watumishi wa Mahakama.

Kamati za maadili ni jicho la Tume katika kusimamia, kuendeleza na kudumisha maadili ya Utumishi wa Mahakama ili kuufanya utumishi wa mahakama uwe wenye kutukuka, kuheshimika na unaojenga Imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama. Jicho hili, linatokana na ukweli kwamba, Kamati zimepewa wajibu wa kisheria, wa kuishauri Tume kuhusu uzingatiaji wa maadili ya Utumishi ili watoe huduma iliyo bora kwa jamii ya watanzania.

Comments (2)

  • Photo Loading... Mwageni

    Asante mheshimiwa jaji mkuu umetukumbusha jambo jema la kuijenga zaidi mahakama .nashauri kuwepo mabanda ya maonesho pindi maonesho ya kitaifa yanafanyika,mfano nanenane,nk ili wananchi wapate kujifunza na kuhoji kuhusu mahakama maana hadi Sasa kunasehemu wananchi wanaogopa chombo hiki .

    11-06-2019
  • Photo Loading... Shotoli

    Hizi kamati za maadiri ya MAHAKAMA zipo wapi? Mimi na mlalamikia Naibu Msajiri wa MWANZA na makarani wawili Christopher na Edsoni naushahidi wa malalamiko yangu ninao, naomba msaada wakujua hii kamati Mwenyekiti wake ninani, maana barua za malalamiko tunapereka sijui zinachanwa! Maana hazifanyiwi kaz

    07-07-2019

Leave a Comment