Post Details

KUWENI MABALOZI WAZURI WA UANDISHI WA HUKUMU; MSAJILI MKUU

Published By:Mary C. Gwera

Na Magreth Kinabo, Mahakama

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewataka Wasaidizi wa Sheria wa Majaji kuwa Mabalozi wazuri kwa wenzao baada ya kupata mafunzo kwa njia mtandao kuhusu uandikaji wa hukumu.

Akizungumza na Wasaidizi hao wa Sheria, tarehe 19 Novemba, 2021, wakati wa hafla ya kuwatunuku vyeti iliyofanyika ofisi kwake Jijini Dares Salaam, Mhe. Chuma alisema wawe tayari watakapohitajika kutoa mafunzo na ujuzi walioupata kwenye eneo hilo.

“Ni imani yangu kuwa mafunzo mliyoyapata yatawasaidia kufanya kazi zenu kwa weledi na ni chachu kwa wasaidizi wa sheria wengine na Maafisa wa Mahakama kwa ujumla,” alisema Msajili Mkuu huyo.

 Aliongeza kwa kuwashauri Maafisa hao kuwa wanapotaka kuandika hukumu ni muhimu wakafanya tafiti kwanza ili  hukumu ziwe nzuri.

Aidha, Msajili Mkuu alitoa rai kwa maafisa wote wa Mahakama kujenga tabia kushiriki mafunzo mbalimbali kwa njia ya mtandao ili kuongeza ufanisi wa majukumu yao ya kila siku.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joyce Karata mmoja wa Washiriki wa Mafunzo hayo alitoa neno la shukrani kwa niaba ya wenzake, ambapo aliushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kuwawezesha kupata mafunzo hayo ambayo yatasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Washiriki waliopata mafunzo hayo ni, Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joyce Karata, Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mahakama ya Rufani, Mhe. Khalfani Omari.Wengine ni Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe.  Happiness Ngogo na Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Yohana Ngonyani. 

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Mahakama (Judicial Institute for Afrika) yalihusu utafiti wa kisheria, uandishi wa hukumu, namna bora ya kuandika hukumu, njia mbalimbali za kufanya utafiti wa sheria, namna bora ya kuboresha hukumu, maadili ya Maafisa wa Mahakama na uhusiano wake kwa Wasaidizi wa Majaji.

Mada nyingine ni namna bora ya kulinda mahusiano na Majaji wanaowasaidia, pia jinsi ya kuzitambua hisia zao na za wengine na umuhimu wake katika utendaji kazi, aina mbalimbali za uandishi wa hukumu na mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kuandaa hukumu na matarajio ya Majaji kutoka kwa Wasaidizi wao wa kisheria na jinsi ya kuandaa hotuba.

Comments (0)

Leave a Comment