Post Details

MAJAJI WAKUU WATANO WA NCHI ZA KUSINI MWA AFRIKA WAKUTANA DAR ES SALAAM

Published By:Mary C. Gwera

Mkutano wa Kamati ya Uongozi wa Kongmano la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini mwa Afrika (Southern African Chief Justice’s Forum) umefanyika jijini Dar es salaam Tanzania chini ya Mwenyekiti wa kongamano hilo ambaye ni Jaji Mkuu wa Malawi Mhe. Andrew Nyirenda.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Majaji wakuu wanne kutoka nchi za Kusini mwa Afrika ambazo ni pamoja na Malawi, Zambia, Namibia, Seychelles na Tanzania ambayo ndiyo ilikuwa mwenyeji wa Mkutano huo.

Akizungumza kuhusu Kongamano la Majaji Wakuu wa nchi za kusini mwa Afrika, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Kongamano hilo, Jaji Mkuu wa Malawi Mhe. Andrew Nyirenda alisema malengo makuu ya kongamano hilo ni kujadili  maendeleo ya Mahakama za kusini mwa Afrika, kuimarisha na kulinda utawala wa sheria katika  nchi hizo pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama za nchi zilizo wananchama wa kongamano hilo.

Alisema kupitia kongamano hilo, agenda maalum huzungumzwa ikiwemo kuimarisha mawasiliano na majadiliano kati ya Mahakama za nchi zilizo kusini mwa Afrika ili Mahakama hizo ziwe na maendeleo ya pamoja. Alisema kupitia kongamano hilo wanahamasisha kuwepo kwa utawala wa sheria kwa kuwa Mahakama ni ndicho chombo chenye jukumu la kusimamia utawala wa sheria.

Kwa mujibu wa Mhe. Jaji Nyirenda, Kongamano hilo pia huboresha ustawi wa watumishi wa Mahakama kazini wakiwemo Majaji, Mahakimu pamoja na  watumishi wengine wa Mahakama zilizo kwenye nchi za kusini mwa Afrika.

Kuhusu mafanikio yaliyofikiwa na Kongamano hilo, Mwenyekiti huyo alisema kumekuwa na maendeleo hasa kwa upande wa Sheria kwani baadhi ya sheria na kanuni zimeweza kufanyiwa mabadiliko katika baadhi ya nchi zilizo kwenye umoja huo. Aliongeza kuwa mafaniko mengine yaliyofikiwa kutokana na kuwepo kwa Kongamano hilo ni pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali yakiwemo ya uongozi.

Kuhusu umuhimu wa Kongamano la Majaji Wakuu wa nchi za kusini mwa Afrika, Jaji Mkuu Mhe. Nyirenda alisema uhumimu wake umeonekana hasa baada ya  kuimarika kwa kazi za kila siku za Mahakama katika maeneo nchi hizo na pia wameweza kubadilishana uzoefu katika masuala ya sheria na pia kutatua changamoto mbalimbali zinazozikabili Mahakama zao kwa pamoja.

Comments (0)

Leave a Comment