Post Details

VIKAO VYA KWANZA MAHAKAMA YA RUFANI VYAZINDULIWA MUSOMA

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, leo Oktoba 18, 2021 amezindua vikao vya  Mahakama ya Rufani vinavyofanyika kwa mara ya kwanza katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma na kusisitiza matumizi ya TEHAMA katika usikilizaji wa mashauri ili kuokoa muda wa Mahakama na wateja, hasa katika karne hii ya 21.

Akizungumza katika uzinduzi wa vikao vitakavyodumu kwa wiki tatu, Prof. Juma amesema kuwa matumizi ya TEHAMA katika shughuli za Mahakama inazingatia pia maelekezo ya Rais wa Jamhuri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Vituo Jumuishi sita vya Utoaji Haki nchini ambapo alielekeza Wizara ya Mawasiliano na Mtendaji Mkuu wa Mahakama kuwasiliana ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa mtandao utakaorahisisha upatikanaji wa huduma za kimahakama.

Alisema kuwa Mahakama ya Rufani imekuja Kanda ya Musoma  kwa ajili ya kusogeza huduma ya utoaji haki kwa umma na kuongeza kuwa kutokana na wingi wa mashauri yaliyopo majopo zaidi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani yanahitajika kufika Musoma ili kusikiliza mashauri hayo. Hivyo amesema usikilizaji wa mashauri unaweza kuendeshwa kwa njia ya mtandao kwa kuwa jengo la Mahakama Kuu Musoma limefungwa vifaa vya TEHAMA ili kukabiliana na changamoto hiyo.

“Siku hizi tunaweza kusikiliza mashauri tukiwa Dar es Salaam kwa kuwa jengo hili limefungwa vifaa vya TEHAMA. Rufaa na maombi yasisubiri ujio wa Majaji. Tuwe tayari kukubali matumizi ya TEHAMA kwasababu yanasaidia kusogeza huduma kuliko kusubiri kwa muda mrefu ambapo wananchi wanaumia sana. Matumizi ya TEHAMA huwapunguzia wananchi usumbufu, gharama za kufuata huduma mbali na kupoteza muda na badala yake kuwa na muda mwingi zaidi wa kuzalisha mali’’ alisema Jaji Mkuu.

Amebainisha kuwa ili kukabiliana na changamoto zinazaowakabili wananchi wa maeneo mengine ambao wanahitaji majengo mapya au ukarabati mkubwa, Mahakama ya Tanzania kwa kupitia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano imetambua baadhi ya maeneo na ujenzi wa Mahakama za Wilaya umeanza, mfano katika Wilaya za Songwe, Kakonko, Buhigwe, Uvinza, Kyerwa, Misenyi, Same, Mwanga, Tanganyika, Kaliua, Butiama na Rorya.

Akizungumzia usikilizaji wa mashauri, Mhe. Jaji Mkuu alisisitiza pia matumizi ya usuluhishi na upatanishi kama njia mbadala na muhimu katika kutatua migogoro ya wananchi, jambo ambalo litasaidia au kupunguza wingi wa mashauri yanayosajiliwa mahakamani, hivyo kuokoa muda wa wananchi wa kutafuta haki.

Katika maneno yake ya utangulizi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. John Rugalema Kahyoza, alimshukuru Mhe. Jaji Mkuu kwa kuamua Kanda hiyo iwe ni mojawapo ya vituo vya Mahakama ya Rufani. “Ujio wa Mahakama ya Rufani ni faraja kubwa sana kwa wananchi wa Mkoa wa Mara ambao wamekuwa wakitumia muda mrefu wakifuata huduma hii Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza,” alisema.

Akitoa takwimu za mashauri yaliyopo katika Kanda yake, Mhe. Kahyoza alisema kuwa hadi sasa kuna jumla ya mashauri  321 ya Mahakama ya Rufani, ikiwemo yale ya jinai 171, mashauri ya madai 132, maombi ya madai 16 na ombi moja (1) la jinai. Hivyo aliwasilisha ombi la kuongezwa kwa vikao vya Mahakama ya Rufani  katika Kanda hiyo.

Mapema kabla ya uzinduzi wa kikao hicho, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Jaji Ferdinand Wambali na Mhe. Jaji Lilian Mashaka walipata nafasi ya kulitembelea jengo la Mahakama Kuu, Musoma na kuridhishwa na ujenzi wake pamoja na miundombinu iliyopo na kuupongeza uongozi wa Kanda hiyo kwa usimamizi mzuri.

Comments (0)

Leave a Comment