Post Details

JAJI MKUU AFUNGUA KIKAO CHA MWAKA CHA WAHE. MAJAJI WA MAHAKAMA YA RUFANI (T)

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa uelewa wa sheria, ujuzi na tabia ni mambo matatu muhimu wanayotakiwa kuwa nayo Majaji wa Mahakama ya Rufani ili yaweze kuwasaidia katika kutoa maamuzi kwenye mashauri. 

Akifungua Mkutano wa mwaka wa Majaji wa Mahakama ya Rufani wa kutathmini utendaji kazi wa Mahakama hiyo  wa mwaka 2018 na  kuweka mikakati ya kazi kwa mwaka 2019, Jaji Mkuu alisema Majaji kuwa na uelewa wa sheria na ujuzi   haitoshi pasipo kujenga tabia ya kufanya kazi kwa kasi na kwa weledi.

“Uvivu, uchonganishi, kulalamika pamoja na ubishi usio na mwelekeo ni tabia za kibinadamu zinazoweza kuathiri utendaji kazi kwa kuchelewesha upatikanaji wa haki”, alisema Jaji Mkuu.

Alisema Majaji wanao umuhimu wa kipekee katika jamii hivyo hawana budi kutoa haki kwa kufuata sheria ili wananchi waweze kuwa na imani na mfumo wa utoaji haki pamoja na utawala wa sheria.  

“Kupitia mkutano huu mtapata fursa ya kubadilishana uzoefu wa namna ya kumaliza mashauri kwa kasi kwani utoaji haki uko katika utamaduni ambao haujaandikwa popote hivyo naamini mtaibua tamaduni zitakazorahisha utoaji wa haki”.

Akizungumzia ongezeko la idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Mkuu alisema kuongezeka kwa Majaji hao kutasaidia Mahakama kupunguza changamoto ya mlundikano wa mashauri ya muda mrefu yaliyopo Mahakamani. Hivi sasa kuna Majaji 21 wa Mahakama ya Rufani ambapo awali kulikuwa na Majaji 15.

Kuhusu changamoto, Jaji Mkuu alisema Mahakama inakabiliwa na upungufu wa bajeti kwa ajili ya vikao vya kusikiliza mashauri. Alisema endapo kungekuwa na bajeti ya kutosha vikao vingi Zaidi vya mashauri vingefanyika na kumaliza mlundikano wa mashauri ya muda mrefu.

Alisema sheria imerekebishwa na kuwapa mamlaka Mahakimu na Manaibu Wasajili kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu hususan yale yanayohusu migogoro ya Ardhi ambapo hatua hii itasaidia kupunguza mashauri mahakamani. Aliongeza kuwa ili Mahakama iweze kuwatumia inahitaji kuongezewa bajeti Zaidi ya iliyopo sasa.

Mkutano wa Mwaka huu wa Majaji wa Mahakama ya Rufani pia umewashirikisha Manaibu Wasajili, wasaidizi wa kisheria wa Majaji, Makarani na watunza kumbukumbu ili waweze kusaidiana na Majaji kupanga mikakati ya kumaliza mashauri kwa wakati.

Comments (0)

Leave a Comment