Post Details

JAJI MKUU ATAJA VIGEZO VILIVYOMUIBUA JAJI SIYANI KUWA JAJI KIONGOZI

Published By:LYDIA CHURI

Lydia Churi na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, ameaninisha vigezo vilivyotumika kupendekeza jina miongoni mwa Majaji 85 wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa Jaji Kiongozi, ikiwemo kutimiza sifa zote za kikatiba, unyenyekevu, busara, na uelewa mpana wa mambo ya Mahakama.

Akizungumza katika hafla fupi ya uapisho uliofanywa leo Oktoba 11, 2021 Ikulu jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu alimpongeza Jaji Mustapher Siyani kwa kuteuliwa kuwa Jaji Kiongozi na kwamba ametimiza sifa zote za Katiba za kuweza kushika nafasi hiyo.

Ameeleza kuwa kuna vigezo ambavyo vilitumiwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kabla ya kumshauri Mhe. Rais katika uteuzi huo kwa kuzingatia kuwa Jaji Kiongozi ni mshauri Maalumu wa Jaji Mkuu na anabeba mzigo mkubwa wa kusimamia Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama zote za chini.

“Ukiangalia idadi ya Mahakama Kuu ambapo kuna vituo 17 na divisheni nne za Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi 29, Mahakama za Wilaya 139 na Mahakama za Mwanzo 960, kazi yako kwa kweli siyo nyepesi, kwa sababu wewe ndiye msimamizi mkuu wa hayo maeneno na kila siku unatakiwa kujua kitu gani kinaendelea katika ngazi hizi zote za Mahakama,” Prof. Juma alimwambia Jaji Kiongozi huyo mpya.

Prof. Juma amesema kuwa kutokana na majukumu hayo mazito, Tume ya Utumishi wa Mahakama ilikuwa na vigezo mbalimbali ilivyokuwa inaviangalia, ikiwemo uelewa mpana wa Mahakama na tamaduni zake za ndani kwa kuzingatia kuwa katika taasisi yoyote, mambo mengi huwa yamejificha.

“Ni kama vile barafu, siku zote unaona ncha lakini uzito wa barafu huuoni. Mimi naamini wewe unafahamu ndani ya barafu na unaifahamu Mahakama. Ukifahamu undani wa Mahakama utakuwa katika nafasi nzuri sana ya kufanya maboresho. Hiyo ilikuwa ni sifa ambayo  wewe na wengine ambao mlipelekwa kwa Mhe. Rais ulikuwa umeitimiza,” alisema.

Vile vile Jaji Mkuu alimweleza Jaji Kiongozi mpya kuwa anatakiwa kuelewa Mahakama sio kisiwa, ambacho hakiingiliani au hakishirikiani na Mihimili mingine. Alisema kuwa Jaji Kiongozi anapaswa kuelewa mipaka ya Mahakama na mipaka ya Mihimili mingine, ikiwemo changamoto zilizopo.

“Unatakiwa uwe na busara, umri wako ni mdogo, wewe ni kiongozi. Utaongoza watu ambao wana umri mkubwa zaidi yako, (hivyo) busara, hekima, utu na  ubinadamu ni jambo ambalo kiongozi yoyote katika nafasi yako anatakiwa kuwa nayo,” alisema Jaji Mkuu.

Kwa mujibu wa Prof. Juma, Jaji Kiongozi anapaswa pia kuelewa Mahakama inapokwenda kwa vile wakati mwingine Majaji na Mahakimu huandika hukumu bila kujua dunia inayowazunguka, ambapo baada ya kutekeleza majukumu yao ya kutoa haki hudhani kwamba wajibu wao umeishia hapo, ilihali nchi na Mahakama hufanya mambo mengine ambayo watu wengi hawayafahamu.

“Kwa hiyo wewe ni jukumu lako kutukumbusha sisi Majaji wapi dunia inakwenda na wapi Mahakama inakwenda ili tuelewe, kwa sababu usipoelewa nchi yako inakwenda wapi utakuwa siku zote kazi yako wewe ni kukosoa yale ambayo yanafanyika,” alisema.

Prof. Juma alimkumbusha dhana ya  safari ya kwenda Mahakama Mtandao ambayo anapaswa kuielewa vizuri kwa vile jambo hilo ni dhahiri kwa kuzingatia vigezo ambavyo Mahakama ya Tanzania imejiwekea ikiwemo kufanya uwekezaji mkubwa katika TEHAMA. “Sasa ni wakati wa kufanya uwekezaji ule uzae matunda. Wewe ni msimamizi ambaye ni muhimu sana katika hilo,” alisema.

Jaji Mkuu pia alitoa wito kwa Mhe. Siyani kuwa na uwezo wa kujenga umoja, kwa sababu katika kila taasisi huwa kuna mashindano yenye mwelekeo wa kutaka kujua nani alimaliza Chuo Kikuu kwanza, nani alipata ‘Division One,’ nani alifaulu kibahati bahati.

“Kwa hiyo, kuna kule kudharauliana, kada nyingine inajiona kuwa bora zaidi ya nyingine. Sasa wewe kazi yako ni kujenga umoja baina ya watumishi wote kwa sababu kila mmoja ni muhimu katika kufikia malengo ya Mahakama,” alisema Jaji Mkuu, huku akimshauri Mhe. Siyani kuwa na shauku ya kujifunza ili kuongezea kiwango chake cha elimu, jambo ambalo ni jema na sifa ya uongozi.

Hata hivyo, Prof. Juma alitoa angalizo kuwa sifa kama hiyo isiwe zaidi ya kuheshimu taaluma, kwa sababu mtu anaweza kuwa amesoma sana na kudharau taaluma zingine ambazo zinafanikisha kazi yake. Kwa hiyo, Jaji Mkuu alimshauri Jaji Kiongozi mpya kuwa mnyenyekevu siku zote na kusikiliza utaalamu uliopo kwa kuzingatia kuwa kuna utaalamu mwingi ndani ya Mahakama.

Jaji Mkuu pia alimwelekeza Mhe. Siyani kusimamia vilivyo nguzo zote tatu za Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania. Amezitaja nguzo hizo kama Utawala bora, Uwajibikaji na Usimamizi wa rasilimali; Upatikanaji wa haki kwa wakati na Kuimarisha imani ya wananchi, kwa sababu bila imani ya wananchi ushirikiano wa wadau wengine, Mahakama inakuwa haina faida.

Katika hafla hiyo, Mhe, Rais Samia alimuapisha pia aliyekuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Omar Othman Makungu kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya  Muungao wa Tanzania. Kwa mujibu wa Prof. Juma, Mhe. Makungu amekuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar kwa zaidi ya miaka 10.

“Karibu sana Mahakama ya Rufani ambapo kazi kubwa ni kusimamia sheria na utatupa ladha ya Sheria za Zanzibar ambazo zitatusaidia ili wananchi wote wa Tanzania waweze kufahamu sheria za Zanzibar,” alisema Jaji Mkuu.

Alitoa pongezi pia kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga mpya, Mhe. Sofia Mjema, ambaye kwa nafasi yake ni mdau mkubwa wa Mahakama. “Ninaamini utakapofika Shinyanga, Jaji Mfawidhi na watendaji wengine wa Mahakama watakutembelea na kukujulisha kuhusu changamoto mbalimbali ambazo Mahakama inakumbana nazo,”alisema.

 

Comments (0)

Leave a Comment