Post Details

MSAJILI MKUU ASISITIZA WELEDI NA UWAZI KAZINI

Published By:LYDIA CHURI

Na Stanslaus Makendi- Mahakama Kuu, Dodoma

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, amewataka watumishi wa Mahakama kote nchini kuzingatia weledi na uwazi wanapotekeleza majukumu yao ya utoaji haki ili kujenga dhana chanya ya uadilifu kwa wananchi.

Mhe, Chuma alitoa wito huo Oktoba 8, 2021 alipokuwa akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Kongwa na Mahakama ya Mwanzo Kongwa katika ziara ya kikazi kukagua shughuli mbalimbali za utoaji haki. Amewasisitiza watumishi wote kutekeleza kikamilifu maagizo na maelekezo yanayotolewa na viongozi wa Mahakama ya Tanzania.

Msajili Mkuu alichukua nafasi hiyo pia kuwataka watumishi katika Mahakama hizo kuimarisha ushirikiano baina yao pamoja na Taasisi au vyombo vingine kwa kufuata utaratibu uliopo ili kutoathiri utendaji kazi wa Mhimili wa Mahakama.

Katika ziara yake ya siku moja kukagua shughuli za Mahakama katika Wilaya ya Kongwa, Mhe. Chuma amewasisitizia watumishi hao kuhuisha mara kwa mara taarifa za mashauri kwenye Mfumo wa Kusajili na Kuratibu Mashauri kwa njia ya Kieletroniki (JSDS II) ili kurahisisha utendaji kazi wa Mahakama na kuwa na taarifa zinazowezesha uongozi kufanya maamuzi.

Mhe. Chuma aliwapongeza watumishi wote kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya na kubainisha kuwa ni vyema watumishi wote wakaelewa maendeleo na maboresho makubwa yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania, hivyo kuwa sehemu ya kuhabarisha umma na kusimamia utekelezaji wake.

Katika ziara hiyo, Msajili Mkuu pia alipata nafasi ya kumtembelea Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Remedius Emmanuel, na kumwelezea umuhimu wa kushirikiana katika kutoa elimu kwa Umma ili wananchi waelewe taratibu za Mahakama na huduma zake, hususani katika eneo la mirathi, ndoa na talaka ambalo bado lina changamoto nyingi.

Alisema kuwa kumekuwepo na changamoto nyingi katika mashauri hayo, ikiwemo wasimamizi wa mirathi kuchelewa kufunga mirathi mahakamani, kugeuka na kujiona ni warithi halali, hivyo kujimilikisha mali kinyume na taratibu.

Msajili Mkuu pia alimwomba Mkuu wa Wilaya huyo kuendelea kusimamia vyema Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama katika ngazi ya wilaya kwa lengo la kuimarisha maadili ya Maafisa hao na kudumisha ushirikiano usioathiri mipaka ya kazi za Mahakama na Taasisi zingine.

Habari hii imehaririwa na Faustine Kapama

Comments (0)

Leave a Comment