Post Details

VIONGOZI WA MAHAKAMA SPORTS WAKUTANA NA MTENDAJI MKUU

Published By:LYDIA CHURI

Na Innocent Kansha - Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, leo Septemba 17, 2021, amekutana na uongozi wa Mahakama Sports ofisini kwake, Mahakama ya Rufani Jijini Dar es Salaam na ameahidi kuwapa ushirikiano wa hali na mali ili kuboresha ushiriki kwenye michezo inayoandaliwa na sekta mbalimbali nchini kwani michezo ni sehemu ya kujenga afya ya mwili na akili.

Katika mazungumzo yake na viongozi hao, Prof. Ole Gabriel hakusita kuonesha hisia zake kwa kutamka bayana kuwa yeye ni mwana michezo na anapenda sana michezo, hivyo atahakikisha Mahakama ya Tanzania inakuwa na timu bora na zenye ushindani wa kweli katika michezo mbalimbali.

“Kama mwaka huu mtashiriki katika michezo ijayo, itategemea na bajeti iliyopo. Hivyo mnatakiwa kutoa uwakilishi kwenye kila mchezo wenye washiriki wachache. Mwaka ujao nitashirikiana na viongozi wengine wa ndani ya Mahakama ili kuongeza bajeti kwa ajili ya kuimarisha ushiriki katika michezo,” alisema.

Hata hivyo, Mtendanji Mkuu huyo aliwataka viongozi hao, kwa kupitia uongozi wa Mahakama ya Tanzania, kuona uwezekano wa kuomba kuwa na viwanja vya michezo katika jiji la Dodoma ili Mahakama Sports iwe na wigo mpana wa kushiriki michezo yote katika mashindano mbalimbali.

Mwenyekiti wa Mahakama Sports, Bw. Wilson Dede, alimwambia Mtendaji Mkuu kuwa Mahakama Sports imekuwa ikishiriki katika michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa wavu pamoja na kuvuta kamba.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, mwaka 2014 Mahakakama Sports iliposhiriki kwa mara ya mwisho kwenye michezo ya SHIMIWI ilifanikiwa kunyakua vikombe vitatu katika michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete na kuvuta kamba, ambapo washiriki walishika nafasi ya tatu kwa kila mchezo.

Hata hivyo, Bw. Dede alibainisha changamoto wanayokabiliana nayo katika kuboresha ushiriki wa michezo mbalimbali, ikiwemo ufinyu wa bajeti ambayo haikidhi ushiriki wa michezo yote. Mwenyekiti huyo aliyeambatana na Katibu wake, Bw. Rorbert Tende, alibainisha pia kuwa Mahakama Sports ina changamoto ya ukosefu wa viwanja vya kufanyia mazoezi.

“Kwa sasa kwa kushirikiana na uongozi wa Mahakama tumeomba viwanja katika Shule ya Sheria kwa Vitendo. Ni Matumaini yetu kuwa wafanyakazi wote wa Mahakama watapata nafasi ya kushiriki katika michezo yote kama tutaruhusiwa kufanyia mazoezi katika viwanja hivi,” alisema.

Mwenyekiti huyo alimweleza Mtendaji Mkuu pia kuwa Mahakama Sports siyo tu ina washiriki kutoka Makao Makuu jijini Dar es Salaam, bali kuna wanamichezo wengine wengi katika kila Kanda wenye timu za michezo mfano; Bukoba, Mbeya, Mwanza, Musoma na Kanda zingine za Mahakama Kuu ya Tanzania

Comments (0)

Leave a Comment