Post Details

BALOZI MSTAAFU MASILINGI AMTEMBELEA MSAJILI MKUU WA MAHAKAMA

Published By:Mary C. Gwera

  • Aipongeza Mahakama kwa maboresho, hususani matumizi ya TEHAMA

Balozi Mstaafu wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Wilson Masilingi, ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika, hususani katika eneo la matumizi ya TEHAMA, ambayo imerahisisha utoaji wa haki kwa wananchi.

Balozi Masilingi ametoa pongezi hizo leo Septemba 15, 2021 alipomtembelea Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Wilbert Chuma, na kufanya mazungumzo naye juu ya suala zima la mabadiliko na maboresho yanayoendelea katika Mahakama ya Tanzania.

“Mahakama imefanya maboresho mbalimbali katika suala zima la utoaji haki, hivyo ni vyema kuendelea kutangaza maboresho hayo kwenye vyombo vya habari ili wananchi waweze kuyafahamu. Sio kwamba nawasifia tu pia mimi mwenyewe ni shuhuda wa maboresho hayo ambapo nimetumia Mfumo wa Mawakili Tanzania ujulikanao kama ‘TAMS’ na kufanikiwa kuhuisha leseni yangu ya Uwakili ndani ya muda mfupi,” alisema.

 Balozi Masilingi aliongeza kuwa kwa muda mrefu baadhi ya watu wamekuwa wakielekeza shutuma mbaya kwa Mahakama na kusahau kuwa kuna mambo mazuri yameshafanyika, ambayo yanahitaji kupongezwa.

“Wakati sasa umefika wa kupongeza jitihada hizi na maboresho mbalimbali ambayo Mahakama ya Tanzania imefanya na inaendelea kufanya katika kuhakikisha kuwa huduma ya utoaji haki kwa wananchi inapatikana kwa wakati,” alisema. Aidha, Balozi Masilingi alishauri watumishi wa umma kuwa wavumilivu, kuheshimu mamlaka na kuwa waadilifu katika kazi zao.

Kwa upande wake Msajili Mkuu wa Mahakama alimshukuru Balozi Masilingi kwa kutembelea Mahakama ya Tanzania na kumwomba kuwa Balozi mzuri  wa maboresho aliyoyashuhudia.

“Mimi nashauri kwamba kutokana na uzoefu ulionao, ni vema ukatumia nafasi ya uwakili kuwasaidia na kuwaelimisha wananchi kuhusiana na masuala mbalimbali ya kijamii na kimahakama,” Mhe. Chuma alimweleza Balozi Masilingi, ambaye baada ya kustaafu serikalini kama Balozi ameamua kuendelea na Uwakili wa Kujitegemea

Balozi Masilingi aliwahi kuwa Mtumishi wa Mahakama kama Hakimu ambapo alishika nyadhifa mbalimbali za kiutawala katika Mhimili huo ikiwemo kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi. Kwa upande wa Serikali, Balozi Masilingi amewahi kushika nyazifa mbalimbali, ikiwemo kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora).

Comments (0)

Leave a Comment