Post Details

VIONGOZI WA MAHAKAMA WATAKIWA KUIBUA WATUMISHI WANAOFANYA VIZURI

Published By:Mary C. Gwera

Viongozi wa Mahakama, Kanda ya Mbeya wametakiwa  kuwatambua watumishi wanaofanya kazi kwa kujituma na kwa weledi na kutoa taarifa kwa mamlaka za juu za Mahakama ili watumishi hao waweze kuteuliwa katika nafasi za juu kwa ustawi wa Mahakama.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Mbeya kwa nyakati tofauti, Aprili 09, 2019 Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi aliyepo ziarani katika Kanda hiyo alisema jukumu la Watendaji ni pamoja na kuwaibua Watumishi wanaofanya vizuri.

Mhe. Jaji Kiongozi alisema kuwa jukumu la viongozi ni kuibua Watendaji wazuri katika kila eneo na endapo mtumishi anabainika kutekeleza majukumu yake kwa weledi ni vyema uongozi ukatambua na kutoa taarifa ili kuteuliwa katika nafasi za juu.

“Endapo mtumishi anabainika kutekeleza majukumu yake kwa weledi ni vyema uongozi ukatambua na kutoa taarifa ili kuteuliwa katika nafasi za juu, hivyo nawasihi Watumishi kila mmoja kwa nafasi yake kutimiza majukumu yake kwa weledi bila chuki, fitina na majungu,” alieleza Mhe. Jaji Dkt. Feleshi.

Aidha Mhe. Jaji Kiongozi aliwataka watumishi kuwa wabunifu, kujipa thamani, kujitambua wao wenyewe na kutambua umuhimu wao kwa Mahakama ya Tanzania. 

Hata hivyo;  Mhe. Jaji Kiongozi amewapongeza watumishi wa Mahakama Kanda ya Mbeya kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii .

Sambamba na hilo, Mhe. Jaji Kiongozi aliwasisitiza kushirikiana katika utendaji kazi ili kuboresha huduma zitolewazo na Mahakama na kusaidiana katika kutatua changamoto mbalimbali za kiutumishi kwa manufaa ya wananchi.

“Mfano ushirikiano unavyoweza kuwa ni pale inapotokea kituo kimoja kimezidiwa mashauri hivyo kuhitaji nguvu kutoka kituo kingine kwenda kupunguza na hata kumaliza mzigo wa kazi katika kituo husika,” alisisitiza Mhe. Jaji Kiongozi.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Dkt. Feleshi aliwataka Mahakimu wenye uwezo wa kutumia kompyuta watumie ujuzi huo kuchapa mienendo na hukumu ili kuweza kuongeza kasi ya utoaji wa nakala za hukumu badala ya kutegemea Makarani ambao idadi yao haitoshelezi.

Akiwa katika jengo la Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Feleshi aliwataka viongozi pamoja na watumishi kuendelea kuitunza miundombinu ya kisasa iliyofungwa katika jengo hilo.

Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama Kanda ya Mbeya, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda hiyo,  Mhe. Jaji Robert Makaramba alisema kuwa amefanikiwa kufanya ukaguzi wa Mahakama zote katika Kanda hiyo isipokuwa moja na inaendelea kufanya vizuri katika suala la uondoshaji wa mashauri.

Katika kudumisha ushirikiano kati ya Mahakama na Serikali, katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo, kwa nyakati tofauti Mhe. Jaji Kiongozi alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mbeya pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Rungwe na kuwataka Viongozi hao kwa nafasi zao kuendeleza ushirikiano.

Katika mazungumzo na Viongozi hao wa mkoani Mbeya, Mhe. Jaji Kiongozi aliwataka pia kuendelea kuwaelimisha Wananchi juu ya mipaka ya kiutendaji kazi kati ya Serikali na Mahakama ili wanapokuwa na jambo linalotakiwa kutatuliwa na Mahakama waweze kufika mahakamani bila kuchelewa.

“Naomba pia muwahimize Wapelelezi kukamilisha kwa haraka upelelezi wa kesi mbalimbali ili Mahakama iweze kuondosha mashauri kwa wakati, nakumbusha pia kutumia Kamati za Maadili ya Mahakimu za Mkoa na Wilaya ili kupata taarifa za Mahakimu wanaojihusisha na Vitendo vya utovu wa maadili ili hatua stahiki zichukuliwe na Mahakama,” aliwaeleza Viongozi hao kwa nyakati tofauti.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake katika Kanda hiyo mbali na kuzungumza na Watumishi Mhe. Jaji Kiongozi alifanya ukaguzi katika miradi ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Rungwe pamoja na Mahakama ya Mwanzo Uyole ambayo miradi yote inatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu.

Comments (2)

  • Photo Loading... tiff_059

    Tena ikiwezekana wapewe motisha ili kuwapa moyo wa kuendelea kufanya kazi

    10-04-2019
  • Photo Loading... Mr. Kamendu

    Hakika hili ni jema, motisha huleta moyo wa kufanya kazi zaidi

    14-04-2019

Leave a Comment