Post Details

JAJI MKUU AMUAPISHA PROFESA ELISANTE KUWA KATIBU WA TUME YA MAHAKAMA

Published By:Mary C. Gwera

-Katibu Mstaafu naye aagwa rasmi na Tume

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo amemuapisha rasmi Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kufuatia kustaafu kwa aliyekuwa Katibu wa Tume hiyo, Bw. Mathias Kabunduguru.

Hafla hiyo fupi ya uapisho wa Katibu wa Tume imefanyika leo Septemba 10, 2021 katika Ofisi ndogo za Bunge zilizopo jijini Dar es Salaam huku hafla ikiwa imehudhuriwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Makamishna wa Tume hiyo, Katibu Mstaafu, Naibu Katibu wa Tume hiyo pamoja na Watumishi wa Tume.

Akizungumza mara baada ya kuapishwa rasmi, Prof. Ole Gabriel alimuhakikishia Jaji Mkuu pamoja na Viongozi wote wa Mahakama kuwa atajitahidi kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano ‘team work’ kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa na Mahakama pamoja na Tume yanafikiwa.

“Naomba niwahakikishie kuwa nitatumia nguvu zangu zote, uwezo wangu nilionao kuhakikisha kuwa tunafanya kazi kwa pamoja na kufikia matarajio tuliyo nayo hususani katika suala la kutoa haki kwa wakati kwa wananchi,” alisema Profesa.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mstaafu wa Tume hiyo, Bw. Mathias Kabunduguru alimkaribisha Katibu mpya huku akimdokeza masuala kadhaa ambayo Tume inakabiliwa nayo ikiwa ni pamoja na upungufu wa Watumishi ambapo idadi ya Watumishi iliyopo kwa sasa ni 16 na mahitaji halisi ni Watumishi 34.

Hata hivyo; Prof. Ole Gabriel ameahidi kushughulikia suala hilo la upungufu wa Watumishi kwa kufanya taratibu stahiki ili kuongeza idadi ya watumishi wa Tume hiyo ili kuipa nguvu zaidi Tume yenye mamlaka makubwa kitaifa ya kuisimamia Mahakama nchini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, Jaji Kiongozi, Mhe. Dkt. Feleshi, Msajili Mkuu, Mhe. Wilbert Chuma na Naibu Katibu wa Tume, Bi. Enziel Mtei walimshukuru Bw. Kabundunguru kwa kufanya kazi kwa kushirikiana kipindi chote alichokuwa Mahakama na Tume vilevile walimkaribisha Katibu mpya wa Tume na kumuahidi kushirikiana nae bega kwa bega katika kutekeleza majukumu yake.

Kufanyika kwa tukio hili la uapisho ni kwa mujibu wa Sheria namba nne (4) ya mwaka 2011 ya Uendeshaji wa Mahakama kifungu cha 16 (ii) ambacho kinamtaka Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye ndiye Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, kumuapisha  Mtendaji Mkuu wa Mahakama kuwa Katibu wa Tume hiyo.

Comments (0)

Leave a Comment