Post Details

KABUNDUGURU AKABIDHI RASMI OFISI KWA MRITHI WAKE

Published By:Mary C. Gwera

-Atoa rai kwa Watumishi wa umma kujituma kwa maendeleo ya Taifa

Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru leo amemkabidhi rasmi Ofisi Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel aliyeapishwa Agosti 21, 2021 baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika wadhifa huo.

Akizungumza kabla ya makabidhiano hayo yaliyofanyika leo Septemba 08, 2021, Bw. Kabunduguru ametoa wito kwa Watumishi wa Mahakama na Watumishi wa umma kwa ujumla kufanya kazi kwa kujituma kwa maendeleo ya Taifa.

“Harakati za kujenga Taifa zinahitaji ushiriki wa Watumishi wake ili kufikia azma ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla, hivyo natoa wito kwa watumishi walioko kazini kuwajibika ipasavyo ili kujenga Taifa,” alisema.

Alisema kuwa Utumishi wa umma umelenga katika kutoa huduma kwa umma, hivyo ni muhimu watumishi kuendelea kuwahudumia vyema wananchi.

 Kwa upande wa Mahakama, Mtendaji Mkuu huyo mstaafu alimuhakikishia Mtendaji Mkuu wa Mahakama kuwa Mahakama ipo katika hali nzuri huku akimuomba kuendeleza maboresho yaliyopo na ambayo yapo kwenye michakato mbalimbali.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Ole Gabriel alimshukuru Bw. Kabunduguru kwa mapokezi mazuri, vilevile kumpongeza kwa kazi nzuri ya kutumikia Taifa na Mahakama katika utumishi wake.

“Napenda nikushukuru Kaka yangu kwa mapokezi mazuri na zaidi ya yote nikushukuru kwa kazi nzuri kwa Mahakama, nami nikuhakikishie kuwa sikuja hapa kutengua torati bali kukamilisha torati, pale mlipoishia watangulizi wangu nami nitaendeleza,” alisema Mtendaji Mkuu.

Aliongeza pia atashughulikia yale yote aliyoelekezwa na Mhe. Rais kuhusu kuboresha maslahi ya watumishi, mirathi ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, matumizi ya TEHAMA mahakamani na mengineyo.

Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amemuhakikishia kumpa ushirikiano Mtendaji Mkuu wa Mahakama, vilevile amemshukuru Bw. Kabunduguru kwa utumishi wake mahakamani na kumuomba kutosita kutoa msaada kwa Mahakama pale atakapohitajika.

Prof. Elisante Ole Gabriel ni Mtendaji Mkuu wa tatu wa Mahakama ya Tanzania tangu kuanzishwa kwa nafasi hiyo ndani ya Mhimili huo kwa mujibu wa Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011. Mtendaji Mkuu wa Kwanza alikuwa ni Mhe. Balozi Hussein Athuman Kattanga (Sasa Katibu Mkuu Kiongozi) ambaye alifuatiwa na Bw. Mathias Kabunduguru ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria.

Comments (0)

Leave a Comment