Post Details

MATUMIZI YA TEHAMA SULUHISHO LA UTOAJI HAKI KATIKA KARNE YA ISHIRINI NA MOJA – JAJI MKUU

Published By:LYDIA CHURI

Na Innocent Kansha – Mahakama, Bukoba

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wote wa Mahakama kujiandaa kuingia kwenye matumizi ya tecknolojia kwa kuwa Mahakama imewekeza zaidi kwenye eneo hilo.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba mara baada ya kukamilisha ziara ya ukaguzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Nyakibimbili inalojengwa Bukoba Vijijini 2021 Jaji Mkuu aliwaambia  watumishi wa Mahakama kuwa, safari ya Mahakama kuingia kwenye matumizi ya mtandao ni sehemu ya karne ya nne ya mapinduzi ya viwanda na ya Taasisi nzima hivyo hakuna atakayeachwa nyuma.

“Nawahimiza kutumia tovuti ya Mahakama ambayo ina taarifa na nyaraka nyingi zitakozowasaidia kujielimisha ili tuweze kuendana na kasi ya utendaji wa shughuli za Mahakama mtandao”, alisema.

Alisema hivi karibuni zimetungwa kanuni za uendeshaji wa mashauri kwa kutumia Mahakama mtandao hivyo watumishi hawana budi kuzisoma na kuzielewa ili waweze kutoa maamuzi yatakayokubalika. Aliwakumbusha watumishi wa Mahakama kuwa dunia ya sasa inahitaji mtumishi anayeweza kujitafutia mwenyewe taarifa muhimu na huku akitolea mfano taarifa za mageuzi ya shughuli za Mahakama.

Jaji Mkuu aliwatoa hofu watumishi kwamba matumizi ya mtandao (TEHAMA) hayatasababisha nafasi zao za kazi kuchukuliwa bali zitabaki zilivyo isipokuwa zitarahisishwa, kwa mfano mlinzi unayezunguka na rungu kila sehemu, teknolojia hii itamtaka ukae kwenye screen ya kompyuta na kuangalia kila sehemu na endapo atamwona mtu ambaye hakupaswa kuwa kwenye eneo lake ataweza kutoa taarifa kwa polisi.

Jaji Mkuu alisema safari ya Mahakama mtandao inategemea Mhimili wa Serikali kama ambavyo mkongo wa Taifa wa mawasiliano unavyomilikiwa na serikali na ndiyo wanamiliki barabara ya mageuzi ya Mahakama mtandao hivyo tunategemea sana sera za Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. “Mahakama ni wapangaji ni lazima ifuatilie maendeleo na maelekezo yote yanayotolewa na maamuzi yanayofanywa na serikali kuhusu mtandao, alieleza Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu Prof. Juma aliwakumbusha watumishi kuwa mageuzi ya Mahakama mtandao na huduma zake hazitawatenga wananchi pia, wanapofuata huduma za utoaji haki kutoka kwa watumishi, hali kadhalika wadau wa Mahakama, wanavyo vigezo vyao wanavyotumia kuwapima kila siku.

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe. Temi Kilekamajenga akisoma ripoti ya utendaji kazi wa Mahakama Kuu kanda ya Bukoba alisema, kasi ya umalizaji wa mashauri imeongezeka kwa asilimia 100 kwa mwezi Julai, 2021. Alifafanua kuwa jumla ya Mashauri 125,760 kati ya mashauri 125,746 yaliyofunguliwa katika Mahakama ngazi zote yalisikiliwa ambapo ni sawa na asilimia 100. Taarifa hii ikilinganishwa na taarifa ya mwezi Juni umalizaji wa mashauri ulikuwa ni asilimia 99.

Alisema changamoto wanayokabiliana nayo ni kutofungwa kwa mashauri ya Mirathi. Alisema kati ya mashauri 32,673 ya mirathi yaliyopo mahakamani, mashauri 29,259 hayajafungwa. Taarifa hii ikiliganishwa na taarifa ya mwezi Juni inaonesha kuwa mashauri ambayo hayajafungwa yameongezeka kutoka 28,129 hadi 29,259.

Comments (0)

Leave a Comment