Post Details

WATUMISHI WA MAHAKAMA NCHINI WATAKIWA KUTOBAGUANA

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka watumishi wote wa Mahakama nchini kutobaguana na badala yake wawasaidie Majaji na Mahakimu kuwawekea mazingira bora ya utendaji kazi ili waweze kutekeleza jukumu lao la msingi la kutoa haki.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma leo, Mtendaji Mkuu amesema Mtumishi yeyote wa Mahakama hapaswi kukwamisha shughuli za utoaji haki kwa namna yeyote ile ili wananchi wanaofika mahakamani wapate haki kwa wakati.

“Haki ya Mbinguni hutolewa na Mungu lakini haki ya hapa duniani hutolewa na Mahakama kwa maana ya Majaji na Mahakimu, hivyo tuwasaidie wenzetu watekeleze majukumu yao ya kutoa maamuzi katika mazingira mazuri”, alisema Prof. Ole Gabriel.

Aidha, Mtendaji Mkuu wa Mahakama amewataka watumishi wote wa Mahakama kutofanya dhambi ya kubaguana kazini na badala yake washirikiane na kuheshimiana katika kazi ili Watanzania waweze kupata haki.

Kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ndani ya Mahakama, Prof. Ole Gabriel amesisitiza umuhimu wa matumizi ya Tehama kwa kadri itakavyowezekana ili kurahisisha shughuli za utoaji haki.

“Hivi sasa idadi ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania kwa nchi nzima ni watu 5,835 wakati mahitaji ya watumishi ni watu 10,350, idadi ambayo kubwa kwa kuwapata wote hao lakini kwa kupitia Tehama tutaweza kufanya kazi licha ya upungufu mkubwa wa watumishi tulionao”, alifafanua Mtendaji Mkuu.

Akizungumzia suala la rushwa na ukosefu wa Maadili, Prof. Ole Gabriel amewataka watumishi wote wa Mahakama kutojihusisha na vitendo hivyo bali wawahudumie wananchi kwa uadilifu na kutumia lugha zenye staha.

“Tuwashughulike wale wachache wanaojihusisha na rushwa ili wasiwaharibu walio wengi wazuri, hao tutawasafisha, sitakuwa na utani kwenye suala linalohusu haki”, alisisitiza.

Mtendaji Mkuu amewataka viongozi wa Mahakama wa ngazi mbalimbali kutumia vizuri fedha za Umma na kuhakikisha wanasimamia kikamilifu masuala yanayohusu maslahi ya watumishi na pia kuwajali na kuwaheshimu watumishi na hasa wale wa ngazi za chini.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania anaendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama na kuungumza na watumishi wa Mahakama kwa lengo la kujitambulisha. Tayari amekagua ujenzi wa jengo la makao makuu ya Mahakama, Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo jijini Dodoma, jengo la Mahakama ya wilaya ya Bahi na Mahakama ya Mwanzo Bahi na kuzungumza na Watumishi wa Kanda ya Dodoma.

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment