Post Details

JAJI KIONGOZI AHITIMISHA ZIARA YAKE KANDA YA IRINGA: AKAGUA MRADI WA UJENZI WANGING’OMBE NJOMBE

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Viongozi wa Mahakama Mkoani Njombe kuwa na desturi ya kutembelea Magereza mara kwa mara ili kubaini changamoto mbalimbali na kuchukua hatua.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Mkoani humo katika Ukumbi wa Mahakama ya Mwanzo Makambako Aprili 08, 2019,  Mhe. Jaji Kiongozi alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa kufanya ukaguzi kwani huwezesha kuangalia mfanano wa hali halisi katika kuendesha mashauri.

“Kuna umuhimu mkubwa katika kukagua Magereza hii husaidia kubaini dosari pamoja na kutambua maeneo yenye udhaifu na kuyafanyia kazi,” alisema Mhe. Jaji Dkt. Feleshi.

Sambamba na ukaguzi wa Magereza Mhe. Jaji Kiongozi aliwataka pia kuendelea na kaguzi za Mahakama mbalimbali katika Mkoa wao ikiwa ni pamoja na kukagua rejesta za mashauri kama kumbukumbu za Mashauri na nyinginezo zinawekwa sawa.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Kiongozi aliwasisitiza Watumishi wa Mkoa huo kuendelea kutimiza majukumu yao kwa maadili ili kuilinda sura ya Mahakama kwa wananchi.

“Majaji na Mahakimu wamekasimishwa madaraka ya kutoa haki duniani hivyo si vyema madaraka haya kuyatumia kwa kujihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili, suala la ukiukwaji wa maadili halina mbadala,” alisisitiza Mhe. Jaji Kiongozi.

Mhe. Jaji Kiongozi alizungumzia pia suala ya usikilizwaji wa Mashauri ambapo alisema kuwa mbali na muda Mahakama iliyojipangia katika umalizaji wa mashauri katika ngazi mbalimbali haizuii Hakimu kumaliza kesi chini ya muda uliowekwa mfano kwa Mahakama za Mwanzo miezi sita badala yake kesi inaweza kumalizwa chini ya muda huo.

Awali, akiwasilisha taarifa ya hali ya Mahakama mkoani Njombe, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa huo, Mhe. Magdalena Nason Ntandu alisema kuwa hadi kufikia Desemba, 2018 Mahakama Mkoani Njombe zilibakiwa na mashauri, 492, kuanzia Mwezi Januari hadi Machi mwaka huu jumla ya mashauri 825 yamefunguliwa na kufikia mwezi Machi, 2019 jumla ya mashauri 891 yalisikizwa na kubaki mashauri 426.

Aidha Mheshimiwa Jaji Kiongozi amekagua mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe ambapo kwa sasa lipo katika hatua ya msingi na kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mbunifu majengo kutoka TBA, Bw. Mustafa Ndambachia jengo hilo linatarajiwa kukamilika tarehe Juni 30, 2019.  

Vilevile Mhe.Jaji Kiongozi alitembelea Mahakama ya Mwanzo Mdandu na kupata fursa ya kuongea na Wananchi wa Tarafa ya Mdandu waliofika kumlaki alipotembelea Mahakamani hapo. Wananchi hao walieleza kuridhishwa na huduma inayotolewa Mahakamani ikiwa ni pamoja na mchakato mzima wa utoaji haki na umalizaji wa mashauri kwa wakati.  

Comments (0)

Leave a Comment