Post Details

VIONGOZI WA MAHAKAMA KUU KANDA MPYA YA MUSOMA, WARIPOTI RASMI: WAJITAMBULISHA KWA MKUU WA MKOA

Published By:Mary C. Gwera

Kufuatia tangazo la Serikali Na. 112 la tarehe Februari 01, 2019 la uanzishwaji wa Mahakama Kuu Kanda za Kigoma na Musoma, Aprili 05, 2019 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mhe. Jaji John Kayoza ameripoti na kukabidhiwa rasmi kituo hicho.

Mhe. Jaji Kahyoza aliambatana na Mhe. Jaji Zefrine Galeba pamoja na Naibu Msajili wa Kanda hiyo, Mhe, Mary Moyo ambapo pia walipata nafasi ya kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa  wa Mara na kukutana na Kaimu wake Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Bw. Vicent Naano.

Katika  mazungumzo yao, Mkuu huyo wa Wilaya alisema, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mara wamefurahishwa na ujio wao kwani sasa kero za wananchi kwenda Mwanza kutafuta haki zao zimefika ukomo.

“Wananchi wengi walikuwa wakifika katika ofisi yangu kuomba nauli za kwenda Mahakama Kuu Mwanza umbali wa Km 223 kufuatilia mashauri yao yaliyopo katika Kanda hiyo,” alieleza Mhe. Naano.

Aidha; Mhe. Naano alielezea changamoto mbalimbali zilizopo katika Mkoa huo kama vile uwepo wa mashauri mengi ya mauaji, ubakaji, ukatili wa kijinsia, uonevu kwa wajane na yatima, ukosefu wa madalali wa Mahakama pamoja na changamoto ya utoaji wa ushahidi. 

Akikabidhi kituo hicho, Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Mwanza, Mhe. Jaji Sam Rumanyika ambaye Kanda yake imekuwa mlezi wa Kanda mpya ya Musoma kwa muda mrefu alionyeshwa  kufurahishwa na Kanda mpya ya Musoma na kusema kuwa Kanda hiyo ni zao la Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Rumanyika aliwaasa Watumishi wa Kanda hiyo kuendeleza ushirikiano ule waliokuwa wakiutoa katika Kanda ya Mwanza, na pia aliwaambia watumishi kuwa wamepata kiongozi bora na sio bora kiongozi.

Naye Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Jaji Kahyoza alimshukuru Jaji Rumanyika kwa kuilea Musoma katika kipindi chote na kumuomba asichoke kutoa msaada pale atakapohitajika kwani mzazi hawezi kumtupa mwana.

Aidha; Mhe. Jaji Kahyoza alisema, hadi sasa tayari zaidi ya mashauri 100 yameshafunguliwa katika Masijala ya Mahakama Kuu Musoma iliyopo katika Ofisi za Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma kwa muda na mashauri hayo yatasikiliziwa Musoma.

“Mashauri haya pamoja na mashauri yote yaliyofunguliwa kuanzia 01/02/2019 yatasikiliziwa Musoma, ila kwa yale mashauri ambayo yalifunguliwa Mwanza kabla ya tarehe hiyo yatasikilizwa hukohuko na Jaji Galeba atabaki Mwanza akiyashughulikia akimaliza ndipo atakuja Musoma kuungana nami pamoja na Msajili ambao wao watakuwepo kituoni rasmi kuanzia tarehe Aprili 10, 2019,” alieleza Mhe. Jaji Kahyoza.

Katika mazungumzo yake Mhe, Jaji Mfawidhi huyo alisema kuwa kauli mbiu ya Mahakama Kuu Musoma itakuwa ni Mahakama ya watu, mteja kwanza (Peoples' Centric Judiciary).

“Tuwahudumie wateja wetu kwa moyo na matatizo au changamoto zetu za ndani zisiathiri shughuli za utoaji haki kwa wateja wetu,” alisisitiza Mhe. Jaji Kahyoza.

Naye Mhe, Jaji Galeba alisema, ukiondoa misikitini, makanisani na mahekaluni ni Mahakamani pekee ndiko mtu anatarajia kupata Amani, suluhu na haki ya kweli na hivyo kwa ujio wao aliwaomba watumishi wote kuwa wamoja ili kumfanya mwananchi aone Mahakama ni sehemu salama ya kukimbilia.

Katika ujio wake Mhe, Jaji Mfawidhi alitembelea na kukagua miradi ya ujenzi inayoendelea ya Mahakama Kuu Musoma na nyumba za Waheshimiwa Majaji. 

Comments (1)

  • Photo Loading... zachariamaseke@gmail.com

    Very nice

    08-04-2019

Leave a Comment