Post Details

MTENDAJI MKUU MPYA WA MAHAKAMA AWATAKA WATUMISHI KUZINGATIA MAADILI

Published By:LYDIA CHURI

Magreth Kinabo na Lydia Churi- Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof, Elisante Ole Grabiel amewataka watumishi wa Mahakama kuzingatia maadili wanapotekeleza majukumu yao ili kuwezesha haki kupatikana kwa wote na kwa wakati.

Akizungumza na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Mahakama ya Tanzania mara baada ya kuapishwa na kuwasili ofisini, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha dhamira ya Mahakama ya kuwasaidia wananchi kupata haki kwa wakati.

“Mahakama ni Taasisi kubwa iliyopewa jukumu la utoaji haki hivyo tunayo kazi kubwa ya kuwasaidia wananchi kupata haki, na haki ikikosekana nchi inaweza kuvurugika”, alisema Prof. Ole Gabriel.

Ametoa wito kwa watumishi wote wa Mahakama kujenga utamaduni wa kufurahia kazi, kushirikiana na kupendana wakati wote ili waweze kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania kwa ufanisi.

“Niwahakikishie kuwa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ni moja kati ya Mipango kumi bora ya aina hiyo duniani, hivyo kazi yetu itakuwa rahisi katika kuutekeleza”, alisema Mtendaji Mkuu huku akitoa pongezi kwa Mahakama.

Aidha Mtendaji Mkuu huyo wa Mahakama ya Tanzania aliwapongeza watangulizi wake kwa kuweka misingi imara ya utendaji kazi ndani ya Mhimili wa Mhakama hivyo watumishi wa Mahakama hawana budi kuendeleza mazuri yaliyoanzishwa

“Mimi Sikuja kuja hapa kuangusha torati, bali nimekuja kuendeleza yale mazuri yaliyoanzishwa na yanayoendelea kufanyika,’’ alisema Prof. Ole Gabriel huku akiupongeza Mhimili huo kwa hatua iliyofikia.

Prof. Elisante Ole Gabriel ni Mtendaji Mkuu wa tatu wa Mahakama ya Tanzania tangu kuanzishwa kwa nafasi hiyo ndani ya Mhimili huo kwa mujibu wa Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011. Mtendaji Mkuu wa Kwanza alikuwa ni Mhe. Balozi Hussein Athuman Kattanga (Sasa Katibu Mkuu Kiongozi) ambaye alifuatiwa na Bw. Mathias Kabunduguru aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.

 

 

 

 

 

 

 

                                                                        

 

 

Comments (0)

Leave a Comment