Post Details

RAIS SAMIA AMUAPISHA MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA

Published By:Mary C. Gwera

       Aahidi kushughulikia changamoto ya Magereza nchini

Na Mary Gwera, Mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan ameahidi kushughulikia changamoto ya Magereza nchini.

Akizungumza leo Agosti 21, 2021 Ikulu Dar es Salaam, mara baada ya kumuapisha rasmi Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Mabalozi wapya, Rais Samia alisema kuwa Magereza zina hali mbaya.

“Suala la changamoto ya Magereza nchini kama alivyotangulia kulizungumzia Mhe. Jaji Mkuu lipo, na sisi Serikali tumesikia na tunaahidi kulifanyia kazi,” alisema Mhe. Samia.

Kwa upande mwingine, Mhe. Rais Samia amewataka Viongozi wote aliowaapisha kufanya kazi kwa bidii, maarifa, weledi na nidhamu ya hali ya juu kwakuwa majukumu yaliyopo mbele yao ni makubwa na vilevile wanategemewa na wananchi.

Akizungumzia upande wa Mahakama, Rais Samia amemtaka Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel kuendeleza maboresho ya Mahakama yaliyopo ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

“Mahakama ndio mamlaka ya utoaji haki nchini, hivyo una kazi kubwa ya kuhakikisha unaendeleza maboresho ili kuwezesha huduma ya utoaji haki inatolewa kwa wakati,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma ameeleza azma ya Mahakama ya Tanzania ya kuwa Mahakama mtandao ifikapo mwaka 2025.

“Mhe. Rais, napenda kushukuru kwa kututeulia Mtendaji Mkuu na nimefanikiwa kupitia wasifu wake, hivyo ni imani yangu kuwa ataisaidia Mahakama kufikia azma yake ya kuwa Mahakama mtandao,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.

Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kwa kuwataka Wadau wote wa Sekta ya sheria nchini kushirikiana pamoja na Mahakama ili kufikia Mahakama mtandao.

Hali kadhalika katika hafla hiyo, Mhe. Rais amewaapisha pia Mabalozi watatu ambao ni Lt. Jen. Yakub Hassan Mohamed kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mahmoud Thabit Kombo kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia na Elsie Sia Kanza kuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.

Mhe. Rais aliwataka Mabalozi hao wapya kuendeleza ushirikiano  baina ya Tanzania na nchi hizo, kuendeleza ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa ikiwa ni pamoja na kuendeleza diplomasia ya uchumi.

Comments (0)

Leave a Comment